February 2015
Kuni News Blog. Habari, matukio na uchambuzi wa makala.
MKUU WA MKOA WA MWANZA MWENYE SHATI JEUSI, MAGESA MULONGO, AKIONESHWA KITU NA MKUU WA WILAYA YA NYAMAGANA WAKATI WA MOJA YA ZIARA YAKE MKOANI HUMO.
Wazee katika Mkoa wa Mwanza, wamemshauri Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kuanza kulima zao la alizeti ili kuuwezesha mkoa huo kuinuka kuichumi kutokana na hali mbaya ya mazao kama pamba kupoteza umaarufu kwenye sekta ya uchumi wa mkoa huo.
Wakizungumza katika kikao kilicho wakutanisha wazee hao na mkuu wa mkoa hivi karibuni katika hoteli ya Mwanza, wazee hao walisema kutokana na hali isiyoridhisha kwa zao kama pamba ambalo ndilo lilikuwa zao kuu la uchumi wa mkoa huu kupoteza umaarufu ni vema sasa jamii ikabadilika na kuhamishia nguvu zake kwenye zao la alizeti.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake, aliyekuwa Mkuu wa kwanza  wa wilaya ya Ilemela, Jared John Gachocha, alisema, haoni sababu ya mkoa wa Mwanza kushindwa kutilia mkazo zao la alizeti ambalo gharama zake za uzalishaji ni nafuu zaidi ukilinganisha na pamba.” Mh. Mkuu wa mkoa mimi nadhani kipindi hiki tushughulike kufa na kupona kwenye alizeti, sioni kwa nini wenzetu wa Singida watupite katika hili, zao la alizeti ni rahisi mno kulilima halina usumbufu halihitaji mbolea nyingi, haliitaji maji mengi na maandalizi yake kwakweli ni rahisi lakini pia faida yake ni kubwa” alisema na kuongeza kuwa “hali hiyo itasaidia mkoa kujitosheleza kwa mafuta lakini pia kuweza kuuza kwa watu wengine.
Mbali ya zao la alizeti wazee hao pia walimuasa mkuu huyo wa mkoa, kuelekeza nguvu zaidi kwenye masuala ya ufugaji, wakisema kuwa tupo nyuma sana katika masuala ya mifugo huku wakitolea mfano nchi ya Kenya kwamba Ng’ombe anauwezo wakutoa maziwa lita hadi 20 tofauti na Tanzania, hali inayo walazimu wazee hao kumuasa mkuu wa mkoa kuwataka wafugaji kuachana na ufugaji wa kizamani na badala yake watafute mitamba itakayoweza kuleta tija kwa wafugaji. “Ni ukweli usiopingika kwamba hapa kwetu kumpata ng’ombe anayeweza kukupatia lita 10 za maziwa ni nadra sana hivyo tuwashawishi wakulima waweze kutafuta mitamba ambayo itakuwa niya kisasa ili waweze kukuza uchumi wao lakini uchumi wa mkoa kwa ujumla.
Awali akizungumza mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kabla yakuanza kupokea maoni ya wazee hao, alisema mkoa wa Mwanza wenye watu Milioni mbili na laki saba na mia saba sabini na mbili mia tano na tisa, huku mkoa ukiwa unachangia Trioni 4.9 katika pato la taifa, Watu wake  milioni moja uchumi wao unategemea zaidi katika Sekta ya Uvuvi, “Wazee wangu nimewaiteni tusaidiane kuongoza mkoa huu, mkoa huu ni mkubwa na changamoto tulizo nazo ni nyingi” alisema Mulongo na kuongeza kuwa, “kati ya watu mil. 2.7, watu Milioni moja wanategemea ziwa kuanzia mvuvi ziwani hadi mparuaji na mchuuzi mdogo mdogo wa mtaani sasa hali ya ziwa letu kwa upande wa uzalishaji sio salama sana, tuna kwendaje lazima tujipange kisawasawa alisema Mulongo.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza toka amewasili mkoa wa Mwanza, ameweka utaratibu wakukutana na watu wa makundi mbali mbali mkoani hapa ili kufahamu changamoto ambazo zipo ili waweze kuzitatua kwa kushirikiana kwa pamoja, makundi ambayo tayari yamekutana na mkuu huyo wa mkoa hadi sasa ni pamoja na, Wananchi wa kawaida kwa kuzungumza nao kwenye mikutano ya hadhara na kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi, Wafanya biashara wadogo ambao alifanikisha kufanyika kwa uchaguzi wao, wakuu wa taasisi za umma zilizoko mkoani hapa, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na asasi zisizo za kiraiya.
Mkoa wa Mwanza ni mkoa wa pili kwa uchangiaji wa pato la taifa kwa asilimia 9.15%  ukitanguliwa na Mkoa wa Dar Es Salaam, huku wastani wa pato la mwananchi wa kawaida ikiwa ni Tshs. 910,824  kwa mwaka.