April 2015
Kuni News Blog. Habari, matukio na uchambuzi wa makala.


Ndugu waandishi wa habari karibuni katika kikao hiki muhimu ambacho ninatarajia kupitia kwenu taarifa hii itaufikia Umma wa watanzania kwa wepesi na kwa haraka (The power of media).

Ndugu zangu waandishi wa habari, mwaka huu wa 2015 Mkoa wetu wa Mwanza umepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa sherehe za Madhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa. Awali Mkoa wa Mwanza ulipewa heshima hii mwaka 2007, ambapo Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa mgeni rasmi na kwa bahati ya pekee Mkoa wa Mwanza unapata fursa nyingine tena  ya kuwa na Mhe. Rais akiwa anahitimisha kipindi chake cha Uongozi wa miaka kumi. Kwetu sisi wana Mwanza kwetu sisi hii ni heshma kubwa sana.

Tunategemea maadhimisho haya kuwa na uzito wa kipekee yakilinganishwa na yale ya mwaka 2007 kwani utakuwa ni wakati mzuri kwa Mkoa wetu kujitathimini hatua tuliyopiga hadi hivi sasa lakini pia kuagana na Rais wetu.

Ndugu waandishi wa habari , Kauli mbiu kwa mwaka huu wa 2015 ni “MFANYAKAZI JIANDIKISHE, KURA YAKO INATHAMANI KWA MAENDELEO YETU”  Kauli mbiu hii inawakumbusha wafanyakazi kuona umuhimu wa kura zao katika kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu hapo baadae, kwani kupitia sanduku la kura mfanyakazi ataweza kujikomboa kwa kuchagua viongozi watakaoleta tija kwenye utendaji lakini pia kuboresha maslahi yao. Rai yangu nawaomba wafanyakazi wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha lakini pia watumie haki yao ya msingi ya kwenda kupiga kura na kuwachagua viongozi wao kwenye maeneo yao pindi muda utakapofika.

Aidha maadhimisho haya kwa mwaka 2015, yanaratibiwa na Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, na Ujenzi (TAMICO) chini ya usimamizi wa shirikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini TUCTA kwa kushirikiana na Uongozi wa Serikali Mkoa wa Mwanza.

Aidha maadhimisho haya yataenda  sambaba na maonesho ya huduma zinazotolewa na  Wafanyakazi na bidhaa wanazo zalisha na yatakayofanyika katika viwanja vya Furahisha kwa  muda wa siku tano kuanzia tarehe 25,Aprili hadi 30,Aprili, 2015

Nichukue wasaa huu, kuwaalika wadau wote wanaohitaji kufanya maonesho ya shughuli zao kujitokeza na kupata mabanda ya kufanya maonesho hayo.

Aidha tunawatangazia wananchi wa Mkoa wa Mwanza , Mikoa jirani na watanzania kwa ujumla kutenga muda wao kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza, kujielimisha na kupata huduma zinazotolewa na Serikali, mashirika na makampuni mbalimbali hapa nchini.

Ndugu waandishi wa habari, nipende kuwahakikishia wananchi kwamba hadi sasa maandalizi kwa ajili ya sherehe hizo yanaendelea vizuri. Wadau mbalimbali watakaoshiriki katika maadhimisho hayo wamepelekewa mialiko na wengine wamesha thibitisha kushiriki. Tunawaomba hata wale ambao mialiko yetu bado haijawafikia kama wako tayari wawasiliane nasi kwani nafasi bado zipo.

Sambamba na hilo tunawasihi waajiri waendelee na zoezi la uteuzi wa wafanyakazi hodari, ununuzi wa sare kutoka kwenye vyama vyao, lakini pia wawaruhusu wafanyakazi kushiriki katika maadhimisho hayo, kwani hiyo ni siku yetu yakujitathimini na kuona hali zetu za utendaji kazi.

Ndugu waandishi wa habari, katika  siku ya kilele kutakuwa na Matembezi ya mshikamano yatakayo anzia kwenye Ofisi za wafanyakazi zilizopo karibu viwanja vya Nyamagana kuelekea  kwenye viwanja vya CCM-Kirumba mapema saa 2.00 kamili asubuhi na kupokelewa na Mgeni Rasmi.

Nirudie tena kuwaomba tumieni kalamu zenu kuufikishia umma taarifa hii kwani tunaamini katika nguvu ya vyombo vya habari mtaweza kuufikia umma kwa haraka na kwa ukubwa zaidi.

 

Asanteni sana.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

YUSUPH SIMBAULANGA

MWENYEKITI WA TUCTA MKOA

MWANZA