Mnyika |
Tarehe 3 Januari 2013 kwa kutumia kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge nimetaka Wizara ya Maji inipatie nakala ya ripoti ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotekelezwa kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 jijini Dar es salaam.
Nimetaka
ripoti hiyo ili kubaini matumizi ya dola milioni 164.6 zinazoelezwa kutumika
katika mradi huo maarufu kama wa ‘mabomba ya mchina’ kwa kuwa mpaka sasa mwaka
2013 sehemu kubwa ya mabomba yaliyowekwa wakati wa mradi huo katika Jiji la Dar
es salaam hayatoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati
wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika
matumizi.
Pamoja na
kutaka ripoti ya utekelezaji wa mradi huo, nimetaka pia nakala ya ripoti ya
ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys
kuhusu mradi huo.
Nimetaka pia
kupatiwa ripoti za ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kwa Kampuni ya Maji Dar es salaam- DAWASCO (Dar es salaam Water Supply
and Sewerage Company) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka-DAWASA (Dar es
Salaam Water Supply and Sewerage Authority) kwa mwaka miaka mitatu ya 2009/10,
2010/2011, 2011/2012 ili kuweza kufuatilia hatua zinazostahili kuchukuliwa.
Aidha kwa
kutumia kifungu hicho hicho cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya
Bunge, katika barua yangu kwa katibu wa Bunge niliyoiwasilisha leo tarehe
3 Januari 2013 nimetaka kupatiwa nakala za mikataba yote ya miradi
inayotekelezwa hivi sasa ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ili kuendelea
kufanya kazi ya kibunge ya kuishauri na kuisimamia serikali kueupusha kasoro
zilizojitokeza katika miradi ya miaka iliyopita kujirudia hivi sasa.
Kati ya
mikataba niliyotaka kupatiwa ni ile ya miradi ya miundombinu inayoendelea
kujengwa na mikopo iliyopatikana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu huyo ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam 2011-2013
ambao uliwasilishwa katika Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 na kuridhiwa
kutekelezwa ukihitaji jumla ya shilingi bilioni 653.85; ambao utekelezaji wake
unasuasua.
Izingatiwe
kwamba Jiji la Dar es salaam lina adha ya maji ya muda mrefu ambayo kila mkazi
wa jiji hili ana wajibu wa kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi hivyo mwaka 2013
utumike kuongeza msukumo wa uwajibikaji katika sekta ya maji ambayo ni muhimu
kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Pamoja na
kuwa matokeo ya sensa ya mwaka 2012 kiwilaya na kimikoa bado hayajatangazwa,
Jiji la Dar es salaam linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni nne; hivyo
ni sawa na takribani asilimia kumi ya watanzania wote milioni 44.9 waliotangazwa.
Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada
mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 51 baada ya uhuru
tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.
Pamoja na kero ya mgawo wa maji hali hii imesababisha
ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea
kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei
ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.
Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya
asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na
hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata
katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka
haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala
ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za
usoni.
Hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa
maji taka zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya
watu katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la
tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani.
Kwa nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2010
Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika
Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka; hivyo
uamuzi wa kutumia sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge na kazi zingine za
kibunge nitakazozifanya mwaka huu wa 2013 zitaongeza uwajibikaji katika sekta
ya maji kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Imetolewa mtandaoni tarehe 4 Januari 2013
Post A Comment: