Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia masuala ya kisiasa Jeffrey Feltman amesema katika kikao cha
Baraza la Usalama kwamba ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi
unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu umekuwa
na taathira hasi kwa mazungumzo kati ya Wapalestina na Israel.
Akielezea hali inavyojiri katika Mashariki ya
Kati, Feltman amesema, mazungumzo ya kusaka amani kati ya Palestina na Israel
baada ya kupita miezi minne tangu yaanze yamefikia katika hali tete ambapo
pande mbili zinajadili maudhui muhimu. Ameongeza kwamba, mwenendo wa mazungumzo
hayo unakwamishwa na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo
wa Magharibi likiwemo eneo la Quds Mashariki na kwamba Umoja wa Mataifa
unafuatilia kadhia hiyo kwa wasiwasi mkubwa. Afisa huyo wa UN ameeleza kwamba, maafisa
wa juu wa kimataifa akiwemo Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa
mara nyingine wamesisitiza msimamo wao kwamba vitongoji vya walowezi wa
Kizayuni si halali na kubainisha kuwa, ujenzi huo unakinzana na sheria za
kimataifa na unakwamisha mwenendo wa amani.
Feltman amesema, maafisa wa Umoja wa Mataifa
wanataka Israel isimamishe mara moja ujenzi huo na kusisitiza ulazima wa
kuundwa nchi huru ya Palestina kama njia pekee ya kustawishwa amani na usalama
wa eneo hilo.
Sisitizo la jamii ya kimataifa kuwa ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina ni kinyume cha
sheria na kwamba hatua hiyo ya Israel ni pingamizi kwa mwenendo wa amani, kwa
mara nyingine limeweka wazi utambulisho usio wa amani wa utawala huo na
kukinzana kwake na sheria na kanuni za kimataifa.
Ijapokuwa malalamiko ya kimataifa dhidi ya siasa
za kupenda kujitanua za Israel hasa ujenzi wa vitongoji yameongezeka, lakini
utawala huo ghasibu bila kujali malalamiko hayo unaendeleza hatua hizo kutokana
na uungaji mkono wa madola ya Magharibi hasa Marekani. Matamshi yaliyotolewa na
Waziri wa Nyumba wa Israel yanaonesha kuwa, Tel Aviv sio tu haijasimamisha
ujenzi wa vitongoji kwenye maeneo ya Palestina bali pia inaendelea kujenga
nyumba mpya na kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huku mazungumzo hayo
yakiendelea. Auri Ariel amesema kuwa, sehemu kubwa ya ujenzi wa vitongoji vya
utawala huo katika maeneo tofauti ya Palestina haikusimamishwa na bado
unaendelea hata wakati wakati huu wa mazungumzo. Hii ni katika hali ambayo,
Bunge la Israel limetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli hizo.
Kung'ang'ania Israel kujenga vitongoji hivyo
licha ya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa ni kinyume cha sheria, kunabainisha
kwamba utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu hauheshimu sheria na
maazimio ya kimataifa na unaendeleza siasa hizo za kujitanua ili ufikie malengo
yake haramu.
Lengo la utawala wa Kizayuni la kujenga vitongoji vya walowezi katika maeneo ya
Wapalestina ni kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa maeneo hayo na
kuyafanya yawe na sura ya Kizayuni ili uendelee kukalia kwa mabavu maeneo
tofauti ya Palestina. Vilevile Israel kwa kujenga vitongoji hivyo vya walowezi
wa Kizayuni, inakusudia kuyatenganisha maeneo ya Palestina ili izuie kivitendo
kuundwa nchi huru ya Palestina.
Itakumbukwa kuwa suala la kuundwa nchi huru ya
Palestina linahesabiwa kuwa ni haki ya mwanzo kabisa na isiyokuwa na shaka ya
wenyeji wa asili wa ardhi ya Palestina, haki ambayo inasisitizwa pia na
viongozi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Jeffrey Feltman.
Post A Comment: