Taasisi ya Benjamin W. Mkapa HIV/AIDS (BMAF) iliyoanzishwa mwaka 2006 na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin W. Mkapa, imekuwa mstari wa mbele kuchangia juhudi za Serikali kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuimarisha huduma za afya, hususan katika maeneo ya vijijini na yenye mazingira magumu. Mradi mmojawapo unaotekelezwa na Taasisi ni wa “Mkapa Fellows” wa miaka mitano (2013- 2017) ambao unafikia Halmashauri 15 zilizopo katika mikoa ya Shinyanga, Kagera, Simiyu, Rukwa na Zanzibar.


          Kitaifa Kanda ya Ziwa imetambulika kuwa na vifo vingi vya akina mama wajawazito ikiwa na wastani wa akina mama 500 wanafariki kila mwaka, pamoja na kuwa na asilimia 40 tu ya wakina mama wajawazito wanajifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya. Pia kanda hii ina maambukizi ya ukimwi ya asilimia 4.8 pamoja na uhaba mkubwa wa watumishi wa afya wa asilimia 39. Aidha ukiwa kama mwananchi, mfanyabiashara au mtanzania, tunapenda kushirikiana nawe katika kupunguza changamoto hizi katika Kanda ya Ziwa kupitia mradi wa Mkapa Fellows.


Taasisi ya BMAF itafanya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya program ya Mkapa Fellows awamu ya pili siku ya Jumamosi tarehe 23 Agosti 2014 kwenye ukumbi wa hotel ya JB Belmont hapa jijini Mwanza. Harambee hiyo itaendeshwa katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na Taasisi na mgeni rasmi wa shughuli hiyo, atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda.
                                         
                                      

Pamoja nae ataambatana na muasisi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa. Lengo kuu la harambee hii ni kukusanya kiasi kisichopungua Tshs milioni 500 kutoka kwa wadau mbalimbali kutoka mikoa ya kanda ya ziwa.

Harambee hii inategemea kuhudhuriwa na wastani wa waalikwa na wadau 150 wanaotokea katika mikoa sita iliyopo kanda ya ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara na Kagera. Miongoni mwa wageni watakao hudhuria harambee hii ni pamoja na wafanyabiashara, wabunge na viongozi wa serikali

         Taasisi inachukuwa furasa hii kutoa shukrani kwa mashirika na makampuni mbalimbali ambayo yamefadhili hafla hii ya chakula cha jioni ambao ni Anglo Ashanti, NSSF, Bank M, Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Ndege Insurance na Nyanza Bottling Ltd. Wengine waliofadhili hafla hii ni pamoja na Montage Limited, Afya Radio, Clouds FM, Isamilo Lodge, JB Belmont.na Shirika la PPF.
               

Imetolewa na:

         Kitengo cha MawasilianoTaasisi ya Benjamin William Mkapa

                S. L. P 76274

                Dar es Salaam

                Barua pepe : info@mkapahivfoundation.org

                Simu namba: 0762 558857 
    Tarehe: 22nd August 2014

                 



Axact

Post A Comment: