Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka watendaji katika mkoa wa Mwanza kuhakikisha watoto wote waliofaulu darasa la saba katika Mkoa wa Mwanza, wanajiunga kidato cha kwanza katika kipindi cha wiki moja kuanzia hivi sasa, huku akiwanya wanaoshindwa kusambaza dawa za wadudu wa pamba kwa wakati.


Kutoka kushoto ni Mayala Simon, Ndaki Mussa, Yasinta Zingula na Rebecca George.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Kwimba, kufuatia Shule moja wilayani humo kuwa na wanafunzi wanne (4) tu, miongoni mwa 127 waliopaswa kuijiunga kidato cha kwanza mwaka huu wa 2014 katika Shule ya Sekondari Walla.


Kwa mujibu habari ambazo mtandao huu umezipata, taarifa hiyo ya kutoripoti kwa wanafunzi zilipatikana mara baada ya Mkuu huyo wa Mkoa kufika katika shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa Solla unaotekelezwa kwa fedha za Serikali kiasi cha shilingi Milioni 359,299,750/=.

Habari zilisema wakati mkuu huyo wa Mkoa akiwa katika matayarisho yakuanza safari ya kuondoka katika eneo hilo ndipo alipofahamishwa kuwa Miongoni mwa watoto waliopaswa kujiunga katika shule hiyo ya Walla ni wanafunzi wane tu ndio walioripoti, ambao hata mtandao huu ulibahatika kupata picha ya watoto hao.

Akioneshwa kukerwa na tabia hiyo Ndikilo alisema, “Ndugu zagu kwa mtaji huu wa kuwaweka watoto nyumbani ni ishara kwamba itakuwa vigumu sana kulikomboa Taifa na ujinga”, alisema na kuongeza kwamba hata suala la imani za kishirikina haziwezi kuisha kama hatutaki watoto wetu waende shule na kuelimika.

Aliongeza kuwa ni lazima wazazi wafikirie zaidi kuwarithisha watoto wao Elimu na sio Ardhi wala fedha, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwaangamiza badala ya kuwaokoa “Kwa hiyo ndugu zangu lazima.. lazima!! Tuone umuhimu wa kuwapa watoto wetu Elimu badala ya kufikiria kuwarithisha mashamba kwakuwa mwisho wa siku watayauza, kama ni pesa watazila zitakwisha lakini unapo wekeza katika ubongo wa mtoto  ni ukweli kwamba, utakuwa umemsaidia……! “lakini pia wewe kama mzazi utaweza kupata Kilo ya sukari kama msaada kutoka kwa mtoto wako”.

Takwimu Wilayani humo zinaonesha miongoni mwa watoto 13,286 walio andikishwa darasa la kwanza mwaka 2007 ni watoto 7547 ndio waliofanya mtihani wadarasa la saba mwaka 2013 huku watoto 5739 waliacha shule kwa sababu mbali mbali zikiwamo mimba na utoro na kuifanya Wilaya hiyo kushika nafasi ya sita katika Mkoa wa Mwanza kwa kupata ufaulu wa asilimia 52.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa ametumia ziara hiyo, kuwahimiza watoa huduma wa ugani kuhakikisha wakulima wanapatiwa dawa za kunyunyuzia kwenye mashamba ya Pamba ili kuwaepusha wakulima kupata hasara.

Alisema hayo wakati alipokuwa akikagua shamba la Pamba la bwana Shija Kanga na bi Christina Makula katika kijiji cha Kilyaboya Wilayani humo. “Kabla sijaonndoka nipate taarifa ya wakulima hawa ambao wametuimia nguvu zao nyingi katika kilimo na sasa nguvu hizo zinataka kuachwa wapate hasara kwa sababu ya dawa za Pamba” alisema Ndikilo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza yupo Wilayani humo kwa ziara ya siku mbili katika kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo, kufanya mikutano ya hadhara na kusikilza kero zinazo wakabili.

Katika siku yake ya kwanza Wilayani humo, alipokea taarifa ya Wilaya, kukagua shamba la Pamba Kilyaboya, Kukagua mradi wa umeme wa Jua, kukagua mradi wa Maji chini ya mpango wa BRN na kuweka jiwe la msingi pamoja na kufanya mkutano wa hadhara ambapo alijibu kero mbali mbali za wananchi na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi zile zilizo hitaji majibu ya kina.

Katika siku yake ya pili Wilayani humo Mkuu huyo wa mkoa anatazamiwa, kuweka jiwe la msingi katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Wilaya, kukagua mashamba ya Mpunga ya Mahiga na kukagua mradi wa Kilimo cha umwagiliaji katika Mradi wa Mahiga, kukagua mradi wa maji kutoka ziwa Viktoria, nyumba ya Mwalimu, vyoo vya walimu na kuweka jiwe la msingi katika shule ya Sekondari Bupamwa na kisha kukagua mradi wa Zahanati Hungumalwa na kisha kufanya mkutano wa hadhara na majumuisho kabla ya kurejea jijini Mwanza.
Axact

Post A Comment: