Na Rajab Ramah, Nairobi.
Utengaji wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) katika utekelezaji wa mipango ya muungano kunaweza
kusababisha kuvunjika kwa jitihada za muungano kamili wa kanda, wachambuzi
wasema.
Kutoka kushoto kwenda
kulia, Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza na Rais
wa Tanzania Jakaya Kikwete wakitembea pamoja wakati walipowasili kwenye mkutano
wa kawaida wa 14 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huko Nairobi
tarehe 30, 2012. [Tony Karumba/AFP]
Wakuu wa usalama kutoka Uganda, Kenya na
Rwanda walikutana mjini Kigali, Rwanda mapema mwezi huu ambapo walitia saini
mkataba wa usalama na ulinzi kurahisisha harakati za raia na watalii za kutoka
sehemu moja kwenda nyingine katika kanda unaolenga kuongeza biashara kati ya
mpaka wa nchi moja na nyingine.
Mkutano huo wa tarehe 9 Januari wa maofisa
wa jeshi, polisi, upelelezi na uhamiaji umefuatia uanzishwaji wa visa ya pamoja ya
utalii na nchi hizo tatu ambayo ilianza rasmi tarehe 1 Januari.
Hii ilikuwa ni mara ya nne viongozi hao wa Uganda, Kenya na Rwanda kufanya
makubaliano kuhusu masuala ya muungano pasipo ushiriki wa Tanzania
na Burundi, ambazo pia ni mwanachama wa muungano huo wa nchi tano.
Tanzania na Burundi hazikuhudhuria mkutano
uliofanyika Uganda na Kenya mwezi Agosti mwaka uliopita, au mkutano uliofanyika huko Kigali
mwezi Oktoba 2013.
Tanzania ililalamika kutengwa katika
mazungumzo, na rais Jakaya Kikwete alisema, "Wameunda umoja wa
hiari. Nani ambaye hana hiari?"
Kuvunjika
Jumuiya ya Afrika Mashariki siku zijazo?
Katika Mkutano wake wa Kawaida wa 15 wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Wakuu wa Nchi huko Kampala mwezi Novemba mwaka
jana, viongozi walisema watajitolea kufanya kazi pamoja, lakini wachambuzi wa
mambo wanasema kuwa hakuna uwezekano wa kutokea hilo.
"Nina wasiwasi kama wakuu wa nchi tatu
-- Museveni, Kenyatta na Kagame -- walikuwa makini wakati wa mkutano kuhusu
ahadi yao ya kusaidia wanachama wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika
shughuli zao kwa sababu kinyume na azimio lao walikuwa Rwanda peke yao,"
alisema Rais wa Chama cha Sheria Afrika Mashariki (EALS) James Aggrey Mwamu.
"Huo ni uthibitisho wa kutosha kwamba wanajitoa kufanya kazi bila ya Tanzania
na Burundi."
Makubaliano ya pande tatu ni tishio kwa
mtangamano wa kanda kwa kuwa yanazitenga kwa makusudi Tanzania na Burundi,
alisema.
"Kile tunachokiona kinachoitwa hatua
ya 'muungano wa hiari' ni ujengaji wa wingu la wasiwasi na jambo baya miongoni
mwa nchi wanachama ambavyo vinaweza kuchochea mgawanyiko na kupanda mbegu ya
kutoelewana ikisababisha kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama
ilivyofanya mwaka 1977," Mwamu aliiambia Sabahi. "Kwetu sisi,
'muungano huo wa hiari' haukubaliki kwa kuwa ni kinyume na mkataba ambao
uliiunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Kushindwa kwa nchi zote wanachama kuungana
katika mipango ya pamoja kisiasa na kimaendeleo ni sawa na kuiacha kanda
isambaratike, alisema.
"Kwa sasa kanda inakabiliwa na
changamoto nyingi zikianzia katika kukosa utulivu wa kisiasa, uharamia na
ugaidi, kwa hiyo, [hatutarajii] kuwatenga wengine na kuhisi kwamba tutafanikiwa,"
Mwamu alisema, akiwaomba viongozi wa kanda kushauriana mara kwa mara ili
wasiendelee kufanya makosa.
Mgawanyiko
wadhoofisha mshikamano wa kanda
Ingawa kujumuika pamoja kunachukuliwa kuwa
bora na viongozi wa kanda walio wengi, Tanzania imepata sifa ya kutoharakisha
masuala ya mtangamano na Burundi inachukuliwa kama nchi isiyo na chochote cha
kutoa, alisema George Omondi, mwandishi wa habari wa gazeti la The East African
anayeandika kuhusu masuala ya kanda.
"Tanzania imekuwa ikiibua masuala ya
umiliki wa ardhi, shirikisho la kisiasa na uraia ambavyo inataka mwongozo ulio
wazi, lakini washirika wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, badala ya kukaa
chini kutatua hili, wanaliona kama dalili ya kuleta mvutano," Omondi
aliiambia kuninews"Wamechagua njia iliyo rahisi zaidi, ambayo ni
kujitenga, [na] ambayo sio sahihi."
"Burundi inaonekana kama mshirika
masikini ambaye hana thamani katika mtangamano hivyo wanachagua kuipuuza
wakisahau kwamba nchi ina watu zaidi ya milioni 9 ambayo inaweza kwa urahisi
kuwa soko kwa bidhaa za Kenya, Uganda au hata Rwanda," alisema.
Manu Chandaria, mfanyabiashara wa Kenya na
mwenyekiti wa Kundi la Comcraft ambalo linazalisha bidhaa za chuma, plastiki na
aluminiamu katika Afrika Mashariki, alisema mgawanyiko wa hivi karibuni utadhoofisha
ufanikishaji wa malengo ya mtangamano wa kanda yaliyowekwa.
"Sisi katika sekta ya biashara
tunahisi kuwa kuvunjika tena au kujitenga kutaanzisha vikwazo vipya katika
biashara," Chandaria aliiambia kuninews. "Kila nchi inaanzisha na
kutumia mifumo yake tofauti ya biashara … itakuwa ni pigo kwa biashara huria
ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo muda wote huu."
Ili kufurahia kikamilifu faida inayotokana
na umoja wa forodha na itifaki ya soko la pamoja, na kukamilisha uanzishaji wa
fedha ya pamoja na shirikisho la kisiasa, alisema viongozi wa kanda hiyo
wanapaswa kuvumiliana na kuwa tayari kushughulikia masuala ya msingi.
Kuiacha nchi moja nyuma kutazuia mchakato
mzima, alisema.
"Tunachokiona ni kutokuwa na uvumilivu
kwa baadhi ya viongozi. Hatuwezi kudhani kwamba tutaendelea kwa kuwaacha wale
walioibua maswali kuhusu mchakato," alisema Chandaria. "Wangepaswa
kukaa na kujaribu kutatua matatizo yaliyoibuliwa na Tanzania badala ya kuamua
kuendelea."
EAC
imeungana na ni yenye malengo, asema Kandie
Kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya
Masuala ya Afrika Mashariki Kenya Phyllis Kandie alipinga hisia za kujitenga,
akisema muungani wa EAC utafanyika kama ilivyopangwa.
"Sitapenda kuingizwa katika mjadala
huo 'muungano wa hiyari', lakini ninachoweza kukueleza ni kwamba sisi ni
muungano kama tulivyokuwa awali na kwamba tuna malengo ya kufanikisha misingi
ya EAC," Kandie aliiambia Sabahi.
Katika kujibu swali la iwapo mikutano ya
nchi hizo tatu zinapingana na mkataba wa EAC, alisema, "Uganda, Kenya na
Rwanda wanatumia utengano wa nchi kadhaa ambayo imeelezwa katika mkataba."
Utengano huo ni msingi katika Kifungu cha 7
cha Mkataba wa EAC, ambacho kinaruhusu maendeleo katika umoja miongoni mwa
kundi dogo la wajumbe katika muungano mkubwa katika maeneo tofauti na katika
kasi tofauti.
Hata hivyo, chini ya kifungu hicho, nchi
wanachama ambazo zinataka kuendeleza kwa haraka bado zinatakiwa kuwafahamisha
wajumbe wengine, ambalo halijafanyika katika suala hili, kwa mujibu wa Mwamu.
Jaribio la kumpata Katibu Mkuu wa EAC
Richard Sezibera kwa ajili ya maoni halikufaulu
Post A Comment: