MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU SALVA RWEIMAM. |
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa hiyo jana ikirejea taarifa zilizomnukuu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba akisema: “Ikulu imetutupia virago.”
Jaji Warioba alikaririwa akilalamikia jinsi yeye na makamishna wa tume, walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari kwa haraka bila kusubiri siku waliyokuwa wamepanga kufanya makabidhiano.
Taarifa ya Ikulu ilisema kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinasema shughuli za tume zinakoma baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba
Ilifafanua kuwa Jaji Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, 2014 na siku iliyofuata Machi 19, 2014 na kwa mujibu wa Sheria Rais alitia saini tangazo la Serikali kuvunja tume hiyo.
Ilisema tangu mwanzo wajumbe, mwenyekiti, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli zake, hivyo kwa mtu “kujitia ameisahau siku hiyo ni kiwango cha juu sana cha unafiki.”
“Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo.
Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema tangu Tume ilipovunjwa, haikuwa tena na kazi ya kuandaa ripoti au Rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha.
Kuhusu muda wa kuandika ripoti ya makabidhiano, taarifa hiyo ilihoji kuwa tangu Desemba 30, mwaka jana sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, ilishindwa nini kuiandaa wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali.
Kurudisha magari
Kuhusu wajumbe kutakiwa kurudisha magari Ikulu, taarifa hiyo imekiri ikitoa sababu kuwa kazi ya tume ilikuwa imemalizika na kwamba magari hayo yanatakiwa kupelekwa kwenye Bunge la Katiba mjini Dodoma.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na mmoja wa wajumbe, Profesa Mwesiga Baregu wameungana na Jaji Warioba wakieleza kutofurahishwa na jinsi Serikali ilivyowatendea.
Jaji Ramadhani alisema wenzake walipokutana Jumatano iliyopita, yeye alikuwa Arusha na dereva aliyekuwa akimwendesha kwenye gari la tume alimwarifu kuwa gari hilo linatakiwa kurejeshwa, hivyo akamruhusu atekeleze alivyoagizwa.
“Nimeingia Dar es Salaam Jumamosi saa 11:00 jioni, gari nililokuwa natumia lilichukuliwa nikiwa Arusha na niliporejea sasa natumia gari langu mwenyewe,” alisema Jaji Ramadhan.
Kwa upande wake Profesa Baregu alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuvunja tume hiyo zimewafanya wajihisi kama wahaini.
Profesa Baregu alisema, “Heri yetu wengine lakini kwa mzee wetu (Warioba) kutokana na kuwa Waziri Mkuu mstaafu, analindwa na walinzi wanaopata maelekezo kutoka kwa Serikali ambayo imetuondoa kwenye kazi iliyotukabidhi kisheria kama wahalifu, sifahamu hatima yake.”
Alisema Jumatano iliyopita wajumbe wote wa tume walikutana wakakubaliana Ijumaa wakabidhi vifaa mbalimbali yakiwamo magari lakini alipoingia kwenye gari lake kurudi nyumbani, dereva akamfahamisha kuwa wameelekezwa siku inayofuata asubuhi magari yote yapelekwe Ikulu.
Alisema hali ilikuwa mbaya kwa waliokuwa wakiishi na familia zao kwenye nyumba walizokuwa wamepangiwa kwa ajili ya kazi za tume, kwani walitakiwa wazirejeshe mara moja lakini kwa kuwa zilikuwa zimelipiwa mpaka Machi 31 wakaachwa wakabaki mpaka siku hiyo.
Alipoulizwa kama ameitwa Dodoma kutoa ufafanuzi wa Rasimu yao, Profesa Baregu alisema: “Tuliyotendewa tunahisi tunachukuliwa kama wahaini, leo niitwe Dodoma niende kwa imani gani? Sijaitwa na hata ningeitwa nisingeenda.”
Kukabidhi ofisi
Naibu Katibu wa Tume, Kashmir Kyuki alithibitisha jana kuwa makabidhiano kati ya Tume na Serikali yamekamilika.
Kyuki ambaye pia ni Mwandishi Mkuu wa Sheria Tanzania, alisema hata madeni ya Tume yamekabidhiwa kwa Serikali na wameafikiana na Wizara ya Katiba na Sheria itangaze kuwa yapo chini yake, ili kuwaondolea hofu wadai.
Alizungumzia suala la aliyekuwa mjumbe, John Nkolo aliyeugua wakati tume ikiendelea na kazi, alisema pia limekabidhiwa kwa Katiba Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.
“Tumewaeleza kuwa tuna mgonjwa tuliyekuwa tukimuhudumia, ataendelea kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ajira serikalini kwa sababu aliugua akitumikia Serikali, watamuhudumia tu,” alisema Kyuki.
CHANZO-MWANANCHI.
Post A Comment: