MKUU WA MKOA WA MWANZA MHANDISI EVARIST NDIKILO PICHANI
(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.)

HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA MHE. ENG. CHRISTOPHER KAJORO CHIZA (MB), KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA CHA NCU (1984) LTD, ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MKUTANO WA BUTIMBA CHUO CHA UALIMU MWANZA TAREHE 04/04/2014, ILITOLEWA NA MKUU WA MKOA WA MWANZA EVARIST NDIKILO KWA NIABA YA WAZIRI.
·        Ndugu Mwenyekiti wa Nyanza Cooperative Union (NCU),

·        Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Simiyu na Geita,

·        Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mwanza, Simiyu na Geita,

·        Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Busega, Geita na Nyang’wale,

·        Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mwanza,

·        Mrajis wa Vyama vya Ushirika,

·        Wajumbe wa Bodi ya Uongozi ya NCU,

·        Wajumbe wa Mkutano Mkuu,

·        Wageni Waalikwa,

·        Mabibi na Mabwana.

 

Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kunipa nafasi ya kufungua mkutano wenu. 

 

Ndugu Mwenyekiti;

Kwanza ninawapongeza kwa juhudi mlizofanya za kuwezesha chama chenu kuajiri watendaji wakuu kwa nafasi za Meneja Mkuu na Mhasibu Mkuu.  Ninatarajia Uongozi wenu utafanya juhudi za kujaza nafasi zingine za Wakuu wa Idara kwa mujibu wa Muundo wa watumishi wa  chama chenu.

 

Ndugu Mwenyekiti, Ninawapongeza tena kwa kuwezesha kukaguliwa hesabu za chama chenu katika kipindi cha miaka minne (4) mfululizo hadi kuishia tarehe 31 Machi 2013. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutokaguliwa hesabu ndani ya Miezi mitano tangia kufungwa kwa Mwaka wa fedha ni kuvunja Sheria kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013.  Kitendo cha kutokaguliwa hesabu za chama ndani ya miezi mitano, hufanya uongozi wa Bodi kuondoka madarakani na kutoruhusiwa kugombea Uongozi kwa miaka sita kwa mujibu wa Sheria Mpya ya Vyama Ushirika.

 

Ndugu Mwenyekiti, katika hesabu zilizokaguliwa, pia kuna taarifa ya Ukaguzi wa Uongozi (Management Audit), hii ikiwa na maana ya hoja za ukaguzi wa Uongozi.  Uongozi wenu hauna Budi kujibu hoja zote za Ukaguzi kama zilivyoainishwa kwenye taarifa ya Ukaguzi wa Uongozi.

 

Ndugu Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Mpya ya Vyama vya Ushirika Na. 6, ya Mwaka 2013, Uongozi wenu unatakiwa kuwasilisha taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za miaka 2009/2010, 2010/2011, 2011/2012 na 2012/2013 na taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na taarifa ya Ukaguzi na Uongozi kwenye Mkutano Mkuu huu wa leo ikiwa ni pamoja na majibu ya hoja za ukaguzi.  Uongozi wenu utatakiwa kutoa maelezo ya kwanini Chama chenu kimepata Hati Chafu ya Ukaguzi wa Hesabu “Adverse Opinion” kwa wanachama.  Pia Uongozi wenu utatakiwa kutoa maelezo ni kwa nini Chama chenu kimeendeshwa kwa hasara kwa miaka yote minne (4) ya hesabu zilizokaguliwa kama inavyoonekana kwenye hesabu za mapato na matumizi za miaka 2009/2010, 2010/2011, 2011/2012 na 2012/2013.  Hivyo ni matarajio yangu kuwa, katika agenda za Mkutano Mkuu huu, moja ya Agenda  iwe ni ya kujadili hesabu zilizokaguliwa na taarifa ya Ukaguzi wa Uongozi.

 

Ndugu Mwenyekiti, Chama chenu hakijapata mkopo wa Ununuzi wa Pamba na kuendesha shughuli za chama ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wanachama katika kukusanya mazao yao ikiwemo zao la pamba, kuchambua na kulitafutia soko.  Hapa pia uongozi wenu utatakiwa kutoa maelezo ni kwa nini chama chenu kimeshindwa kupata mkopo toka vyombo mbali mbali vya fedha.

 

Ndugu Mwenyekiti, Suala la Ulinzi wa mali za chama, lilikwisha tolewa awali na Mhe. Waziri Stephen M. Wasira (Mb), katika Mkutano Mkuu wa Chama uliofanyika tarehe 31/03/2009 katika Ukumbi wa Benki Kuu Mwanza.  Mhe. Waziri alieleza wazi kuwa kamwe chama kisitoe mwanya wa wajanja wachache kutumia udhaifu unaojitokeza katika usimamizi wa shughuli za chama.  Kumejitokeza katika usimamizi wa shughuli zenu hasa kwenye Ubia wa Kiwanda cha Manawa ambako chama chenu kina asilimia 67%. Kiwanda kinadaiwa na mbia, kiasi cha Tshs. 528/= milioni na hivyo NCU (1984) Ltd kuonekana inadaiwa kwa tafsiri za kawaida haiingii akilini, ni vipi mbia akadai mbia mwenzake wakati shughuli zinaendeshwa kwa pamoja. Mhe. Waziri Stephen M. Wasira (Mb)  alielekeza chama kuajiri Mwanasheria mwenye uwezo wa kutetea katika kesi zenu za mali zilizoko kwenye mahakama na vile vile kuendeleza mahusiano ya karibu na Wanasheria wa Mkoa na  Wizara katika kulinda mali za Chama chenu.  Mhe. Waziri alisisitiza pia kufuatilia kesi zote zilizoko mahakamani ikiwemo mgogoro wa jengo la “ Transport”, ghala la Igogo ili haki ipatikane juu ya mali hizi.  Sambamba na mali za Igogo na Transport, vile vile uongozi wenu uangalia juu ya mali za kiwanda NCU Eror (Double Oil Refinery Plant), Nyumba za watumishi tatu zilizouzwa za Isamilo, Eneo la Mkonge/Dengu lililoko Igogo na viwanja vya Vick fishi.

 

Ndugu Mwenyekiti,


MOJA YA MASHAMBA YA PAMBA YANAYO
PATIKANA WILAYANI KWIMBA.

Katika juhudi zenu za kupata mkopo benki ya TIB inaonesha wazi kuwa benki ya TIB imewapatia sharti la kuunda kampuni tanzu ya kuendesha shughuli za NCU (1984) Ltd. Kimsingi kuunda kampuni Tanzu ni jambo linalokubalika ingawa kampuni Tanzu hiyo itakuwa vyema ikaandikishwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.

 



MKUU WA MKOA WA MWANZA AKIKAGUA
MOJA YA SHAMBA LA PAMBA WILAYANI KWIMBA.
Ndugu Mwenyekiti, Kuhusiana na Serikali kufuta madeni, ni suala ambalo linabidi kuangaliwa kwa makini, sababu ya deni la chama kuwepo.  Kwani Chama hiki kimekwisha futiwa madeni kwa awamu tatu tofauti.  Awamu ya kwanza ni ya mwaka 1991 katika Serikali ya Awamu ya pili, ambapo Serikali ilichukua na kufuta madeni ya Vyama vya Ushirika nchini kwa kiasi cha 37.3 bilioni.  Awamu ya pili chama chenu pia kilifutiwa madeni ya iliyokuwa benki ya NBC.  Awamu ya tatu ni katika Serikali ya Awamu ya nne (4) ambapo chama kilifutiwa na kulipiwa madeni ya NSSF na malimikizo ya mishahara ya watumishi. Hivyo  kwa sasa Serikali inabidi itafakari na kujua chanzo cha madeni ya chama chenu.

 

Ndugu Mwenyekiti, Ili chama chenu kiondokane na madeni, chama chenu hakina budi kuendeshwa kwa medani ya kisasa ikiwa ni pamoja na chama chenu kuwa na mpango Mkakati wa Miaka Mitatu.  Mpango Mkakati ni dira ya maendeleo ya Union katika kuwawezesha wanachama kukuza uchumi wao ambayo ndiyo matarajio yao.  Hivyo ni matarajio yangu Uongozi wenu utawasilisha Mpango Mkakati angalau wa miaka mitano kwenye mkutano huu ili kuwapa fursa wanachama kujadili mpango wenyewe.

 

Ndugu Mwenyekiti, Kwa kumalizia naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa fursa ya kipekee kuungana na wanaushirika wenzangu wa Mwanza katika kutekeleza demokrasia ya Vyama vya Ushirika ya kukutana na kujadili maendeleo ya chombo chenu.  Matumaini yangu ni kwamba baada ya Mkutano huu wajumbe mtaendeleza uelewa kuhusu wajibu mlionao katika kujenga upya NCU na Vyama  Wanachama ili viwe vyombo vya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa ujumla. Ninawashukuru sana na sasa ninatamka rasmi kuwa Mkutano wenu wa Ishirini na Nne (24) nimeufungua.

 

 

Asanteni kwa kunisikiliza
Axact

Post A Comment: