BISMARK ROCK MWANZA. |
Ndugu Wananchi napenda kuwataarifu
kupitia vyombo vya habari juu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka
2014 ambayo Mkoa wa Mwanza umechaguliwa kuandaa maadhimisho hayo kitaifa.
Ndugu Wananchi, Maadhimisho ya Siku
ya mazingira Duniani hufanyika kuanzia tarehe 01 hadi 05 ya mwezi Juni kila
Mwaka. Maadhimisho haya huwa na Kauli mbiu iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili kuhimizana
juu ya umuhimu wa uhifadhi wa Mazingira yetu.
Kwa mwaka huu 2014, shirika la Umoja
wa mataifa linalo shughulikia mazingira limetangaza Kaulimbiu ya maadhimisho
hayo kuwa ni “RAISE YOUR VOICE BUT NOT
THE SEA LEVEL” kwa tafsiri ni “CHUKUA
HATUA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI. Kitaifa, kauli mbiu yetu ni ”TUNZA MAZINGIRA ILI KUKABILIANA NA MABADILIKO
YA TABIANCHI.
Ndugu wananchi
Kama nilivyotanguliwa kusema, Mkoa wa
Mwanza umeteuliwa kuwa mwenyeji wa kitaifa, wa maadhimisho ya siku ya Mazingira
Duniani mwaka huu. Katika juma hilo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwa ni
pamoja na kufanya usafi katika maeneo yote, kuhamasisha wananchi kuhusu
utunzaji wa Mazingira kwa njia ya
Makongamano, kupanda miti, kuzoa takataka, maonesho ya utunzaji na mazingira,
kuondoa magugu katika Ziwa Victoria na ufugaji wa nyuki pamoja na kufanya ziara
kwenye maeneo tofauti yanayo jishughulisha na utunzaji wa mazingira ikiwemo
viwanda.
Ndugu wananchi,
Ufunguzi wa maadhimisho haya kitaifa
utafanyika tarehe 02 Juni, 2014 kuanzia saa 1.00 asubuhi katika Viwanja vya
Furahisha, Ufunguzi huo utafanywa na Waziri nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira Mheshimiwa Dkt, Binilith Mahenge na siku ya kilele itakuwa tarehe 05 Juni, 2014
ambapo Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
Ndugu wananchi,
Shughuli zitakazo fanyika siku ya
tarehe 05 Juni 2014 (Siku ya kilele) ni
pamoja na:- kukabidhi vyeti kwa wadau mbali mbali wa mazingira, zawadi na tuzo
ya Rais ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na zawadi nyinginezo kwa
washindi wa kuhifadhi mazingira.
Ndugu waandishi wa habari,
Natambua kwamba ninyi ni wadau
wakubwa sana wa mazingira hasa katika jukumu lenu la kuuelimisha umma, juu ya
umuhimu wa kutunza mazingira, kwa nafasi ya pekee niwaombe muweze kuipeleka
taarifa hii kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani ili waweze
kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Furahisha kwa muda wote ambao elimu
kuhusu utuzaji wa mazingira itakuwa ikitolewa na wadau mbali mbali.
Aidha
Mkoa unategemea kupokea Wageni wa Kitaifa na Kimataifa, ambao watatembelea viwanda na kuona utunzaji wa Mazingira na
jinsi ya kutenga taka ngumu na zisizo ngumu.
Nichukue fursa hii kutoa rai kwa
wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi na kushirikiana na wageni wetu kama
ilivyo ada ya Wana Mwanza. Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi na kuwalaki
wageni wote watakao tufikia katika juma zima kuanzia tarehe 01 hadi 05 Juni
2014. Kama ilivyo desturi yetu wana Mwanza tuonyeshe ukarimu wetu kwa wageni
wetu na pindi watakapo ondoka waikumbuke Mwanza.
Nimalizie kwa kusema nawashukuru sana
kwa kuitika wito wangu.
“TUNZA MAZINGIRA, KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI”
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.
IMETOLEWA NA MKUU WA MKOA WA MWANZA.
Post A Comment: