Mfuko
wa Penshini wa LAPF kwa watumishi wa umma na wasio watumishi wa umma umetoa
elimu kwa Waajiriwa waliopo katika Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza huku
wakiwataka watumishi kujisikia fahari kujiunga na mfuko huo kwani ndio mfuko
pekee nchini wenye kutoa mafao bora na kwa wakati.
Akitoa
elimu kwa watumishi hao meneja wa LAPF kutoka makao makuu Abubakar Ndwata
amesema kutokana na ubora wao, ndio maana watu wameendelea kuwaamini na katika
mwaka wa 2013 walifanikisha kuwaunganisha wateja wapatao elfu kumi na moja(11,000)
jambo ambalo wao wanalitaja kama ni mafanikio makubwa kuyafikia ndani ya
kipindi cha mwaka mmoja.
Katika
hatua nyingine Ndwata amesema Tanzania ndio nchi pekee yenye sera ya mifuko ya
hifadhi ya jamii katika nchi zilizopo Afrika mashariki na kati na hii inatokana
na Tanzania kuridhia mikataba mbali mbali kama ule wa ILO namba 102 sera ya hifadhi ya mifuko ya jamii
ya mwaka 2003 pamoja na sheria zilizoanzisha mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwapo
ile iliyo anzisha LAPF ya mwaka 2006.
Awali
akifungua mafunzo hayo Katibu tawala msaidizi wa seksheni ya Utawala na
rasilimali watu, Bibi Crescencia Shayo, aliwataka watumishi kuwa huru kujiunga
na mfuko wanao utaka bila ya kulazimishwa “ Kwa hivi sasa kwa mujibu wa sera ya
mifuko ya hifadhi ya jamii kila mtu anaye ajiriwa anayo hiyari ya kujiunga na
mfuko anaoutaka hivyo basi mtumishi awe huru kuchagua mwenyewe na wapi anataka
kujiunga na ninyi wenye mifuko kila mmoja abakie kueleza uzuri au ubaya wa
mfuko anaotoka” alisema na kuongeza haipendezi kuanza kunyang’anyana wateja kwa
njia ambazo sio halali mathalani kutumia rushwa nk.”.
Mfuko
wa LAPF ulioanza mwaka 1944 chini ya iliyokuwa serikali ya Kikoloni ya Tanganyika
ilikuwa kwa ajili ya wafanyakazi wa chini maakida na makarani kwa lengo la
kuwawezesha kujiwekea akiba ulibadilishwa na kuwa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa
sheria namba 9 ya 2006 kufuatia mabadiliko ya kanuni ya kukokotoa mafao ya
uzeeni sawa na yale yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Serikali kuu.
Post A Comment: