Ndugu Kaimu Katibu Tawala
wa Mkoa wa Mwanza,
Ndugu wajumbe wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa,
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya
Nyamagana,
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,
Ndugu Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza,
Ndugu Mkurugenzi wa Jiji la
Mwanza,
Ndugu Mkurugenzi wa
Hospitali ya Rufaa Bugando,
Waheshimiwa Madiwani mliopo
hapa,
Ndugu Mkurugenzi wa kiwanda
cha kuzalisha dawa,
Waandishi wa habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali
ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kufika
katika siku ya leo tukiwa wazima na wenye afya tele.
Vilevile
nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Prince
Pharmaceutical, kwa kuwa na wazo la kuwekeza katika mkoa wetu wa Mwanza,
sisi kama wana Mwanza tunaona dhamira yetu ya kuvutia wawekezaji wengi sasa inatimia
kwani mtakumbuka ni hivi karibuni tulikuwa na kongamano kubwa kabisa la
uwekezaji kwa kanda hii ya ziwa, mkoa wa Mwanza ukiwa ni mwenyeji wa kongamano
hilo lililofanyika katika Hoteli ya Malaika iliyoko Mkoani hapa kwa lengo la
kuvutia wawekezaji kama Prince Pharmaceuticals.
Ndugu wananchi,
Labda
ni rejee kidogo
alichokisema
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohamed Gharib Bilali
katika hotuba yake ya Ufunguzi wakati wa kongamano hilo, kwamba “nia ya Serikali ni kuweka mazingira mazuri
na ya kuvutia na kuona watu wengi
wanakuja kuwekeza katika kanda hii”. Sasa hili ambalo ndugu zetu wa Kings Pharmaceutical,
mmelifanya ni moja ya matunda hayo, mazingira ni mazuri, fursa za kibiashara
zipo na hali ya Ulinzi na Usalama ni ya kuridhisha ndio maana mkapata msukumo
wa kuja kuwekeza. Hongereni sana .
Ndugu wananchi,
Katika
mkoa wa Mwanza na kanda ya Ziwa kwa ujumla, kwa muda mrefu tumekuwa hatuna
kiwanda cha kutengeneza dawa katika eneo letu. Hali hii imefanya Kanda ya ziwa kutegemea
dawa kutoka sehemu zingine kama vile Dar es Salaam na nje ya nchi, jambo ambalo
limeongeza gharama sana kwa serikali na hata wananchi wanaofanya biashara ya
dawa kwa ujumla wao, vile vile kutokuwepo na kiwanda kumekuwa kukiathiri upatikanaji wa dawa kwa wakati katika vituo
vyetu vya kutolea huduma za Afya. Hivyo ni imani yangu kwamba, uwepo wa kiwanda
hiki kitakuwa mkombozi kwa mkoa wetu wa Mwanza na wananchi wa kanda ya ziwa kwa
ujumla hasa ukizingatia kuwa, Mwanza imekuwa kitovu cha biashara kwa nchi za
maziwa makuu.
Ndugu wananchi,
Pengine
sasa tuone faida za kuwepo kwa kiwanda hiki katika mkoa wetu wa Mwanza.
Tumeelezwa kuwa kiwanda kitakuwa na seksheni nne (4) za uzalishaji dawa yaani
seksheni ya utengenezaji wa dawa za maji (syrup), Malai (ointments), poda (powder),
na viambukuzi (antiseptics). Ambazo zote hizi zitatoa ajira kwani tunajua fika
Idadi ya wakaazi wa Mkoa wa Mwanza kwa sasa wapatao Milioni 2.7 kwa mujibu wa sensa
ya mwaka 2012, na ongezeko la wananchi wetu kwa kiwango cha asilimia 3% kwa
mwaka, ni ushahidi tosha kwamba serikali na wadau wengine wanayo dhima ya
kuhakikisha ongezeko hilo linakwenda sambamba na upatikanaji wa ajira. Sasa basi,
wenzetu wa Prince pharmaceutical, wametuonesha kwa vitendo kwa kuanzisha
kiwanda hiki, ambacho baada ya kuanza kazi kitakuwa na uwezo wa kuajiri
wafanyakazi wapatao 50 hadi 100 lakini mbali na ajira hizo, katika uchumi kuna kitu
kinaitwa multiply effect ambapo, uwepo wa kiwanda kutasaidia kuongeza kipato
cha mtu mmojammoja, mapato kwa serikali ambayo yatasaidia mkoa wa Mwanza
kuongeza ukuaji wa kasi ya uchumi na kuchangia katika pato la Taifa ambalo
Mwanza kwa sasa inashika nafasi ya pili katika uchangiaji wa pato la Taifa. Ni
imani yangu kuwa Kiwanda hiki si tu kitazalisha ajira ajira, bali kitakuwa
mstari wa mbele katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii (Coperate Social
Responsibility) ambazo pia zitainufaisha jamii inayozunguka kiwanda hiki.
Ndugu wananchi,
Pamoja
na nia nzuri ya kuanzishwa kwa kiwanda hiki, napenda nisisitize na kutoa
tahadhari ifuatayo. Katika uzalishaji wenu wa dawa, tafadhali kumbukeni kuwa
wananchi wetu ni masikini sanalakini pamoja na umasikini wao wanahitaji kuwa na
afya bora ili waweze kufanya shughuli za kujiletea maendeleo. Kwa hali hiyo,
hakikisheni mnatengeneza dawa ambazo zina ubora unaotakiwa lakini kwa bei
ambayo hata mwananchi wa kawaida anaimudu. Najua, kama kiwanda mtahitaji kupata faida, lakini
utengenezaji wa faida hiyo usiwaumize wananchi kwa kuwatengenezea dawa zisizo
na ubora (dawa feki) ama kuwauzia wananchi dawa zilizopitwa na muda wa matumizi
(expired) kwa kuwabadilishia lebo za tarehe za kuisha kwa muda wa matumizi ya
dawa hizo.
Tumearifiwa hapa kwamba wenzetu hawa wa Prince
Pharmaceutical watazalisha dawa zao kwa kufuata viwango vya kimataifa vya ubora
(Good Manufacturing Practices –GMP), rai yangu ni kwamba jambo hilo
ni jema na liwe kwa vitendo. Tunajua upo
ushindani wa kibiashara kwenye soko kutoka ndani na nje ya nchi, lakini ni
imani yangu kwamba mkizalisha dawa zenye ubora na mkaziuza kwa bei nzuri,
mtaweza kushinda ushindani kwenye soko, maana waswahili husema …..“kizuri
chajiuza, kibaya chajitembeza”.
Aidha,
napenda nichukue fursa hii kuwaagiza Mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA)
kuhakikisha ubora na viwango vinafuatwa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
katika kiwanda hiki kwani hivi karibuni tumeshuhudia matukio ya uwepo wa dawa
bandia, sasa hatutaki hiyo itokee katika mkoa wetu.
Ndugu wananchi,
Ulinzi
wa kiwanda hiki ni muhimu sana, rai
yangu kwa wananchi wa maeneo haya na
Mkoa wa Mwanza kwa ujumla, ni lazima tuelewe ulinzi wa kiwanda hiki
ni wetu sote, asitokee mtu miongoni mwetu mwenye nia mbaya ya kuhujumu kiwanda hiki. Kwani kwa kufanya hivyo,
tutakuwa tumemsononesha sana mwekezaji, lakini pia
kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na mtawakatisha
tamaa wawekezaji wengine waliokuwa na nia ya kuja kuwekeza katika mkoa wetu.
Sambamba
na hilo ,
mwekezaji pia anapaswa afahamu kwamba ana wajibu wa kuilinda jamii inayo mzunguka
hususani katika suala la utunzaji wa mazingira. Anao wajibu wa kuhakikisha
usalama na maslahi ya wafanya kazi wake.
Lakini kama hiyo haitoshi kwa zile ajira
ambazo zinaweza kufanywa na wananchi wa maeneo haya, ni vema wakapewa
kipaumbele kwanza na sio kwenda kuleta wageni toka nje ya nchi
ili waje kufanya kazi ambazo wanajamii wa hapa wana uwezo wa kuzifanya. Wazungu
wana msemo usemao (charity begins at home).
Ndugu wananchi,
Kabla
sijamalizia hotuba yangu hii. Ninapenda kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuiga
mfano wa ndugu zetu hawa wa Prince
Pharmaceutical, kwani ni ya yetu ni kuona Makampuni mbali mbali yanakuja
kuwekeza katika mkoa wetu wa Mwanza. Vile vile, mimi kama mtumishi wenu wa Serikali
katika Mkoa huu niwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha wakati wote
na msisite kufika ofisini kwangu pindi
mtakapo ona kuna ulazima wa kufanya hivyo, nasema milango iko wazi kwangu mimi
mwenyewe, lakini pia kwa wasaidizi wangu kupitia katibu Tawala wa Mkoa wa
Mwanza.
Baada
ya kusema hayo, niwashukuru tena uongozi wa kiwanda hiki pamoja na wote ambao
tumekuja kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda hiki cha Prince
Pharmaceuticals.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.
Post A Comment: