Articles by "HOTUBA."
Showing posts with label HOTUBA.. Show all posts
Kuni News Blog. Habari, matukio na uchambuzi wa makala.
Waziri Sitta akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake katika Bunge la Bajeti jana linaloendelea Jijini Dodoma.


Waziri Sitta pamoja na Naibu wake Mhe. Abdulla Juma Abdulla wakifuatilia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ushirikiano jana Bungeni Dodoma.


Baadhi ya Wabunge wa EALA wakifuatilia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano jana Bungeni Dodoma


Naibu Waziri Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Abdulla Juma Abdulla akijibu hoja za wabunge kuhusu Wizara yake wakati wa uwasilishaji bajeti jana Bungeni Dodoma


Uongozi wa Wizara ya Ushirikiano katika picha ya pamoja mara baaada ya kupitishwa kwa Bajeti yao.
(Picha zote na Maelezo na: Ofisa habari wa Wizara hiyo Antony Ishengoma)

no image
Kuni News Blog. Habari, matukio na uchambuzi wa makala.
Mheshimiwa Eng. Evarist. Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Mwanza

Mheshimiwa Mariam Lugaila - Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,

Dkt. Yohana Budeba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,

Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani- Mifugo na Uvuvi,

Mtendaji Mkuu LITA,

Mkurugenzi Mkuu-TALIRI,

Wanahabari,

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

 

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana siku ya leo tukiwa na afya njema. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi mziwa wa Taasisi hizi mbili za TALIRI na LITA kwa kunipa heshima ya kuweka jiwe la msingi na kufungua kituo cha mafunzo ya mifugo vilivyopo hapa Mabuki. Nimefarijika zaidi kuja hapa leo kuifanya kazi hii kutokana na kuvutiwa na utekelezaji mzuri wa miradi hii ambayo niliiona nilipotembelea kituo hiki kwa mara ya kwanza, mara tu baada ya kuteuliwa Waziri mwenye dhamana, Mwezi Januari mwaka huu. Hongereni sana kwa kazi nzuri.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, kwanza napenda kuupongeza sana Uongozi wa TALIRI na LITA kwa jitihada zao za kuongoza shughuli za Utafiti na Utoaji wa mafunzo ya mifugo katika Taasisi zetu. Sanjari nah ii, napenda kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH kwa kufadhili ujenzi wa majengo haya ya maabara ya nyama, Darasa na Ukumbi wa Mitihani tunayoweka mawe ya msingi leo. Pia namshukuru Mkurugenzi wa COSTECH kwa ufadhili wa mafunzo ya Shahada za Uzamili na Uzamivu kwa watafiti wetu 24 (20 MSc na 4 PhD) waliofadhiliwa/wanaofadhiliwa na Serikali kupitia COSTECH katika Vyuo vikuu tangu mwaka 2010/2011 na miradi 15 ya utafiti wa mfugo na uvuvi inayoendelea katika Taasisi zetu nchini.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, kazi ninayofanya ya kuweka mawe ya msingi na ufunguzi wa kituo hiki cha mafunzo leo hii inaashiria jitihada za Serikali katika kupanua na kuimarisha shughuli za utafiti na utoaji wa mafunzo ya mifugo hapa nchini. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeanzisha Taasisi (TALIRI na Wakala (LITA) ili kuongeza ufanisi katika utafiti na utoaji mafunzo ya mifugo hapa nchini. Aidha, uwekaji wa jiwe la msingi na ufunguzi wa jingo vimekuja wakati muafaka. Hii ni kutokana na kupanuka kwa huduma za utafiti na mafunzo ya mifugo katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Geita na Simiyu ambayo kwa pamoja ina jumla ya Wilaya 32. Hii pia ni kwa kutambua kuwa idadi kubwa ya mifugo inapatikana katika mikoa hii.

 

Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, nimeelezwa kuwa kutokana na mabadiliko ya muundo wa Wizara na Idara zake, Kituo hiki kimehama mara mbili. Mwaka 1994 ambapo kituo kilihama kutoka Malya na kwenda Ukiliguru na mwaka 2005 kikahamishwa na kuja hapa kilipo sasa yaani Mabuki. Kwa sababu hiyo kituo hakikuwa na majengo yake wala eneo la kufanyia utafiti na shughuli nyingine pamoja na miundombinu mingine hali iliyochangia kuchelewa usimamizi wa shughuli za utafiti hadi ilipofika mwaka 2008. Nina imani kuwa baada ya hapa, Taasisi itatumia kikamilifu eneo walilopatiwa na Wizara ambalo lina ukubwa wa takribani hekta 1,000 kwa shughuli mbalimbali za utafiti wa mifugo kwa ufanisi. Hii ikiwa ni pamoja na hekta 10 zilizotengwa kwa ajili ya majengo ya Ofisi, makazi na miundombinu mbalimbali ya kiutafiti. Ni imani yangu kuwa maeneo haya na rasilimali zake zitatumika na kulindwa kikamilifu kwa maslahi ya Taifa.

 

Ndugu Mkurugenzi Mkuu, ninafahamu kuwa TALIRI inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya utafiti kwa fedha kutoka Serikalini kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Hii ni pamoja na ujenzi wa maabara ya nyama ambayo tunaweka jiwe la msingi leo na nyumba mbili za watumishi hapa TALIRI- Mabuki, kazi ambayo ilianza mwaka 2012/2013. Ninafahamu kuwa TALIRI Mabuki ilipata jumla ya Tshs. Milioni mia nne na hamsini na tano (455,000,000/=) kutoka COSTECH kwa ajili ya ujenzi wa maabara na nyumba tatu (3) za watumishi za daraja la pili. Nafahamu pia kuwa tayari jumla ya shilingi 435,959,945.00 zimekwishatolewa kwa ajili ya maabara (Tshs. 69,863,370.00 ns Tshs 270,096,575.00) kwa ajili ya maandalizi ya awali na ujenzi wa nyumba tatu (3) za watumishi za daraja la pili na nina imani zimetumika tayari kwa kazi zilizokusudiwa.

 

Aidha, nina taarifa kuwa ujenzi wa maabara umekamilika kwa asilimia 98% na nyumba umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95%. Napenda kuwapongeza kwa mara nyingine kwa uadilifu na uwajibikaji mzuri. Nachukua fursa hii kuiomba COSTECH kumalizia sehemu ya fedha ambazo hazijatumwa kwenu ili kuweza kukamilisha ujenzi huu pamoja na kununua vifaa kwa ajili ya maabara hii.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, najua kuna changamoto za kukosa umeme, maji na vifaa vya maabara katika kituo hiki na gharama za awali zinakadiriwa kuwa shilingi milioni 21.7 kwa ajili ya kuweka umeme na maji. Niendelee kumuomba Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH atusaidie tena kufadhili katika kazi hii. Ama kwa hakika COSTECH tutawakumbuka kwa kazi nzuri waliyoifanya lakini pia wanaimarisha wajibu wao kama wadau muhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini. Pamoja na hilo, ninaiagiza TALIRI ifanye utaratibu wa kupata gharama halisi za vifaa na mashine muhimu za maabara hii ili iweze kufanya uchunguzi wa kisayansi inavyotakiwa. Ni wakati muafaka kwa watafiti waliopo kutumia ubunifu wa kuandika miradi ya utafiti itakayojumuisha kuimarisha maabara hii kwa ufadhili wa fedha za ndani na nje ya Tanzania.

 

Ndugu Wakurugenzi, kama sote tunavyofahamu, upatikanaji wa fedha za utafiti na vitendea kazi ni changamoto kubwa kwa Taasisi na vituo vya utafiti na mafunzo ya mifugo katika kukidhi matarajio ya wadau katika sekta ya mifugo. Gharama kubwa zinahitajika kuchunguza, kuendesha na kusimamia shughuli za utafiti na mafunzo ikiwa ni pamoja na kuhifadhi na kuendeleza koo bora za mifugo kwa wafugaji, uhimilishaji, uzalishaji wa mbegu za malisho, kufundisha wataalam wa mifugo na gharama za kawaida za uendeshaji wa kazi za kila siku kwa vituo vyetu. Pamoja na juhudi za Serikali, nawaagiza watafiti na wakufunzi waliopo kufanya juhudi kubwa za kuandika miradi na machapisho mengi iwezekanavyo kutafuta fedha na mahitaji mengine ktuoka mifuko na fursa mbalimbali zitolewazo ndani na njea ya nchi ili kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, Kimataifa bado tunakabiliwa ba tatizo la ufugaji usio na tija kubwa huku ukilalamikiwa kutokana na uharibifu wa mazingira, migogoro na watumiaji wengine wa ardhi kama vile wakulima na wahifadhi wa wanyamapori. Wafugaji wetu bado wamezingirwa na umaskini mkubwa licha ya idadi kubwa ya mifugo nchini. Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina ng’ombe milioni 22.8, mbuzi milioni 15.6, Kondoo milioni 7.0, nguruwe milioni 2.01 na kuku milioni 58. Ni kupitia tafiti nzuri takwimu zinaweza kuleta utajirisho mkubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

 

Wageni Waalikwa, kwa sasa Wizara yetu ina changamoto ya kudhibiti/kuzuia uvamizi wa maeneo ya mashamba unaofanywa na wananchi wanaozunguka mashamba ya Taasisi zenu. Wananchi hawa huchunga mifugo shambani bila idhini nah ii inahatarisha afya na usalama wa mifugo ya Taasisi pamoja na uharibifu wa miundombinu. Ni vyema Taasisi zenu zikatafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na changamoto hii kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya husika ili utatuzi huu uwe na amani.

 

Aidha, nachukua fursa hii kuagiza ukamilishaji wa upimaji na upatikanaji wa hati miliki kwa maeneo yote nchini yanayomilikiwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi yakiwemo yale yaliyopo chini ya Taasisi na Vituo vyake. Kazi hii ifanywe mapema iwezekanavyo ili kupunguza migogoro iliyopo kwa sasa na ambayo inaweza kujitokeza kwa siku za usoni.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, upanuzi na ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha mafunzo ya mifugo Mabuki ni moja ya ahadi zilizotolewa na Serikali Bungeni kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Hivyo napenda kuwajulisha kuwa ahadi hiyo tunaitekeleza na tutaendelea kuzitekeleza kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Hata hivyo, ni vyema kuwakumbusha kuwa miundombinu ya majengo hugharimu Serikali fedha nyingi. Hivyo basi ningependa kuwaasa muendelee kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa na Wageni waalikwa, kwa muda mrefu Serikali kuu imekuwa ikigharimia ka kiasi kikubwa mafunzo ya mifugo kwa wagani ili wakasimamie sekta ya mifugo. Kazi hiyo kwa sasa inatekelezwa na Wakala na sekta binafsi. Serikali kuu itabaki na jukumu la kutoa miongozo na sera zinazohusiana na uendeshaji wa sekta ya mifugo nchini. Wote tunajua umuhimu wa mafunzo kwa maendeleo ya Taifa hili na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za utoaji wa mafunzo hapa nchini kwa Taasisi za Umma na za binafsi.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilitoa ahadi Bungeni ya kupunguza pengo la wagani 11,303 wa mifugo wanaohitajika vijijini hivi sasa. Nina furaha kuwa ahadi hiyo tutaweza kuitimiza katika muda muafaka. Ujenzi wa majengo ya Bweni linaloweza kuchukua wanafunzi 56 na Ukumbi unaoweza kutumiwa na wanafunzi 100 kwa wakati mmoja katika kituo cha Mabuki kunafanya Wakala wa mafunzo (LITA) kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi 2,300 kwa mwaka. Ongezeko la idadi ya wanafunzi katika Kampasi za LITA kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza pengo la wagani lililopo ili kufikia lengo la kuwa afisa ugani mmoja wa mifugo kwa kila Kata na kila Kijiji.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, Serikali ilianzisha Wakala wa Mafunzo ya Mifugo ikitegemea mambo kutoka kwenu ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya Serikali. Kwa sababu hiyo, naomba kutoa nasaha zangu kwa Jumuiya ya Chuo kwa ujumla kama ifuatavyo:

§ Chuo kiendeshwe kibiashara kwa kuanzisha miradi ambayo tazalisha na kujiendesha kwa faida. Natambua kuwa mafunzo ya mifugo yanahitaji kuwa na aina mbalimbali za wanyama kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Kwa mtazamo huo ni budi kufuga na kutunza wanyama katika kiwango cha hali ya juu ili wanafunzi waweze kujifunza kuwa ufugaji kibiashara unawezekana na kuwa unaqweza kupunguza umasikini na kuchangia Pato la Taifa.

 

§ Uongozi wa Chuo ujitahidi kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa ujumla ili kuendana na taaluma inayotolewa. Aidha, ni vyema Chuo kikajipanga kuanza mchakato wa kuandika miradi mbalimbali ambayo inaweza kufanywa kituoni. Miradi hiyo itaweza kuwasaidia kupunguza utegemezi wa ruzuku toka Serikalini.

 

Ndugu Mkuu wa Mkoa, pamoja na kutoa mafunzo ya mifugo kwa wagani, lakini pia kituo hiki cha LITA wakishirikiana na TALIRI watafute mbinu ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wafugaji wanaozunguka eneo hili la Mabuki. Hapa nigeomba uongozi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kupiita Halmashauri zao kukaa pamoja na Uongozi wa Taasisi hizi mbili kuona namna Wilaya zitakavyoweza kutumia miundombinu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi hizi katika kuwahudumia wafugaji. Nina imani wafugaji wetu wakipatiwa stadi za ufugaji bora wa mifugo  wataweza kuinua kipato chao na Taifa kwa jumla. Ninapenda kusisitiza kuwa utoaji wa mafunzo kwa wafugaji uwe ni wa kudumu kwa kuwa hii ni njia rahisi ya kuwafikia walengwa.

 

Aidha, ningependa kuwaasa watumishi wa Taasisi hizi na watu wengine wote mlio hapa kuwa UKIMWI ni janga kwa Taifa letu. Ugonjwa huu umepunguza sana nguvu kazi ya Watanzania kwa kuathiri rika zote. Nawataka wote mzingatie maadili mema na ushauri wa wataalamu wa afya na viongozi wa Dini ili tuweze kuondokana na janga hili kwani utashi wa kuepukana na ugonjwa huu uko mikononi mwa kila mmoja wetu.

 

Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, naomba nihitimishe kwa kutoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza, COSTECH na wadau mbalimbali kwa kuendelea kushirikiana na TALIRI na LITA ili Taasisi hizi ziweze kufanya utafiti na kutoa mafunzo kwa wanafunzi na wafugaji. Aidha, nawatakia kila la kheri watafiti, wakufunzi, Wafanyakazi, Wanachuo na Jamii yote inayozunguka Taasisi za Mabuki katika kazi zenu za kila siku.

 

Kwa kumalizia napenda kuwatakia safari njema wageni wote waalikwa mliofika kwenye uwekaji wa mawe ya mzingi katika majengo haya ya TALIRI-Mbuki na LITA-Mabuki pamoja na uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mifugo. Mungu awaongoze ili msafiri salama na kuzikuta familia zenu zikiwa salama.

 

Kwa pamoja tunaweza, kila mtu atimize wajibu wake.

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
no image
Kuni News Blog. Habari, matukio na uchambuzi wa makala.
Ndugu Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,

Ndugu wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,

Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,

Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,

Ndugu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,

Ndugu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,

Ndugu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Bugando,

Waheshimiwa Madiwani mliopo hapa,

Ndugu Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa,

Waandishi wa habari,

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana.

 

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kufika katika siku ya leo tukiwa wazima na wenye afya tele.

Vilevile nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Prince Pharmaceutical, kwa kuwa na wazo la kuwekeza katika mkoa wetu wa Mwanza, sisi kama wana Mwanza tunaona dhamira yetu ya kuvutia wawekezaji wengi sasa inatimia kwani mtakumbuka ni hivi karibuni tulikuwa na kongamano kubwa kabisa la uwekezaji kwa kanda hii ya ziwa, mkoa wa Mwanza ukiwa ni mwenyeji wa kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Malaika iliyoko Mkoani hapa kwa lengo la kuvutia wawekezaji kama Prince Pharmaceuticals.

Ndugu wananchi,

Labda ni rejee kidogo

alichokisema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohamed Gharib Bilali katika hotuba yake ya Ufunguzi wakati wa kongamano hilo, kwamba “nia ya Serikali ni kuweka mazingira mazuri na ya kuvutia na  kuona watu wengi wanakuja kuwekeza katika kanda hii”. Sasa hili ambalo ndugu zetu wa Kings Pharmaceutical, mmelifanya ni moja ya matunda hayo, mazingira ni mazuri, fursa za kibiashara zipo na hali ya Ulinzi na Usalama ni ya kuridhisha ndio maana mkapata msukumo wa kuja kuwekeza. Hongereni sana.

Ndugu wananchi,

Katika mkoa wa Mwanza na kanda ya Ziwa kwa ujumla, kwa muda mrefu tumekuwa hatuna kiwanda cha kutengeneza dawa katika eneo letu. Hali hii imefanya Kanda ya ziwa kutegemea dawa kutoka sehemu zingine kama vile Dar es Salaam na nje ya nchi, jambo ambalo limeongeza gharama sana kwa serikali na hata wananchi wanaofanya biashara ya dawa kwa ujumla wao, vile vile kutokuwepo na kiwanda kumekuwa kukiathiri  upatikanaji wa dawa kwa wakati katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya. Hivyo ni imani yangu kwamba, uwepo wa kiwanda hiki kitakuwa mkombozi kwa mkoa wetu wa Mwanza na wananchi wa kanda ya ziwa kwa ujumla hasa ukizingatia kuwa, Mwanza imekuwa kitovu cha biashara kwa nchi za maziwa makuu.  

 

Ndugu wananchi,

Pengine sasa tuone faida za kuwepo kwa kiwanda hiki katika mkoa wetu wa Mwanza. Tumeelezwa kuwa kiwanda kitakuwa na seksheni nne (4) za uzalishaji dawa yaani seksheni ya utengenezaji wa dawa za maji (syrup), Malai (ointments), poda (powder), na viambukuzi (antiseptics). Ambazo zote hizi zitatoa ajira kwani tunajua fika Idadi ya wakaazi wa Mkoa wa Mwanza kwa sasa wapatao Milioni 2.7 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, na ongezeko la wananchi wetu kwa kiwango cha asilimia 3% kwa mwaka, ni ushahidi tosha kwamba serikali na wadau wengine wanayo dhima ya kuhakikisha ongezeko hilo linakwenda sambamba na upatikanaji wa ajira. Sasa basi, wenzetu wa Prince pharmaceutical, wametuonesha kwa vitendo kwa kuanzisha kiwanda hiki, ambacho baada ya kuanza kazi kitakuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi wapatao 50 hadi 100 lakini mbali na ajira hizo, katika uchumi kuna kitu kinaitwa multiply effect ambapo, uwepo wa kiwanda kutasaidia kuongeza kipato cha mtu mmojammoja, mapato kwa serikali ambayo yatasaidia mkoa wa Mwanza kuongeza ukuaji wa kasi ya uchumi na kuchangia katika pato la Taifa ambalo Mwanza kwa sasa inashika nafasi ya pili katika uchangiaji wa pato la Taifa. Ni imani yangu kuwa Kiwanda hiki si tu kitazalisha ajira ajira, bali kitakuwa mstari wa mbele katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii (Coperate Social Responsibility) ambazo pia zitainufaisha jamii inayozunguka kiwanda hiki.

 Ndugu wananchi,

Pamoja na nia nzuri ya kuanzishwa kwa kiwanda hiki, napenda nisisitize na kutoa tahadhari ifuatayo. Katika uzalishaji wenu wa dawa, tafadhali kumbukeni kuwa wananchi wetu ni masikini sanalakini pamoja na umasikini wao wanahitaji kuwa na afya bora ili waweze kufanya shughuli za kujiletea maendeleo. Kwa hali hiyo, hakikisheni mnatengeneza dawa ambazo zina ubora unaotakiwa lakini kwa bei ambayo hata mwananchi wa kawaida anaimudu. Najua, kama kiwanda mtahitaji kupata faida, lakini utengenezaji wa faida hiyo usiwaumize wananchi kwa kuwatengenezea dawa zisizo na ubora (dawa feki) ama kuwauzia wananchi dawa zilizopitwa na muda wa matumizi (expired) kwa kuwabadilishia lebo za tarehe za kuisha kwa muda wa matumizi ya dawa hizo.

 Tumearifiwa hapa kwamba wenzetu hawa wa Prince Pharmaceutical watazalisha dawa zao kwa kufuata viwango vya kimataifa vya ubora (Good Manufacturing Practices –GMP), rai yangu ni kwamba jambo hilo ni jema na liwe kwa vitendo.  Tunajua upo ushindani wa kibiashara kwenye soko kutoka ndani na nje ya nchi, lakini ni imani yangu kwamba mkizalisha dawa zenye ubora na mkaziuza kwa bei nzuri, mtaweza kushinda ushindani kwenye soko, maana waswahili husema …..“kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza”.

Aidha, napenda nichukue fursa hii kuwaagiza Mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA) kuhakikisha ubora na viwango vinafuatwa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika kiwanda hiki kwani hivi karibuni tumeshuhudia matukio ya uwepo wa dawa bandia, sasa hatutaki hiyo itokee katika mkoa wetu.

Ndugu wananchi,

Ulinzi wa kiwanda hiki ni muhimu sana, rai yangu kwa wananchi wa maeneo haya  na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla, ni lazima tuelewe ulinzi wa  kiwanda hiki  ni wetu sote, asitokee mtu miongoni mwetu mwenye nia mbaya ya  kuhujumu kiwanda hiki. Kwani kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumemsononesha sana mwekezaji, lakini pia kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika  kuwaletea maendeleo wananchi wake na mtawakatisha tamaa wawekezaji wengine waliokuwa na nia ya kuja kuwekeza katika mkoa wetu.

Sambamba na hilo, mwekezaji pia anapaswa afahamu kwamba ana wajibu wa kuilinda jamii inayo mzunguka hususani katika suala la utunzaji wa mazingira. Anao wajibu wa kuhakikisha usalama na maslahi ya wafanya kazi wake.

 Lakini kama hiyo haitoshi kwa zile ajira ambazo zinaweza kufanywa na wananchi wa maeneo haya, ni vema wakapewa kipaumbele  kwanza  na sio kwenda kuleta wageni toka nje ya nchi ili waje kufanya kazi ambazo wanajamii wa hapa wana uwezo wa kuzifanya. Wazungu wana msemo usemao (charity begins at home).

 

Ndugu wananchi,

Kabla sijamalizia hotuba yangu hii. Ninapenda kutoa wito kwa wawekezaji wengine kuiga mfano wa ndugu zetu hawa wa Prince Pharmaceutical, kwani ni ya yetu ni kuona Makampuni mbali mbali yanakuja kuwekeza katika mkoa wetu wa Mwanza. Vile vile, mimi kama mtumishi wenu wa Serikali katika Mkoa huu niwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha wakati wote na  msisite kufika ofisini kwangu pindi mtakapo ona kuna ulazima wa kufanya hivyo, nasema milango iko wazi kwangu mimi mwenyewe, lakini pia kwa wasaidizi wangu kupitia katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.

Baada ya kusema hayo, niwashukuru tena uongozi wa kiwanda hiki pamoja na wote ambao tumekuja kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda hiki cha Prince Pharmaceuticals.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.