Mheshimiwa Eng. Evarist.
Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Mheshimiwa Mariam Lugaila -
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,
Dkt. Yohana Budeba, Naibu Katibu
Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Mkurugenzi wa Utafiti,
Mafunzo na Ugani- Mifugo na Uvuvi,
Mtendaji Mkuu LITA,
Mkurugenzi Mkuu-TALIRI,
Wanahabari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana siku ya leo
tukiwa na afya njema. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi
mziwa wa Taasisi hizi mbili za TALIRI na LITA kwa kunipa heshima ya kuweka jiwe
la msingi na kufungua kituo cha mafunzo ya mifugo vilivyopo hapa Mabuki.
Nimefarijika zaidi kuja hapa leo kuifanya kazi hii kutokana na kuvutiwa na
utekelezaji mzuri wa miradi hii ambayo niliiona nilipotembelea kituo hiki kwa
mara ya kwanza, mara tu baada ya kuteuliwa Waziri mwenye dhamana, Mwezi Januari
mwaka huu. Hongereni sana
kwa kazi nzuri.
Ndugu Mkuu wa Mkoa,
kwanza napenda kuupongeza sana
Uongozi wa TALIRI na LITA kwa jitihada zao za kuongoza shughuli za Utafiti na
Utoaji wa mafunzo ya mifugo katika Taasisi zetu. Sanjari nah ii, napenda
kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH kwa kufadhili ujenzi wa majengo haya ya
maabara ya nyama, Darasa na Ukumbi wa Mitihani tunayoweka mawe ya msingi leo.
Pia namshukuru Mkurugenzi wa COSTECH kwa ufadhili wa mafunzo ya Shahada za
Uzamili na Uzamivu kwa watafiti wetu 24 (20 MSc na 4 PhD)
waliofadhiliwa/wanaofadhiliwa na Serikali kupitia COSTECH katika Vyuo vikuu
tangu mwaka 2010/2011 na miradi 15 ya utafiti wa mfugo na uvuvi inayoendelea
katika Taasisi zetu nchini.
Ndugu Mkuu wa Mkoa,
kazi ninayofanya ya kuweka mawe ya msingi na ufunguzi wa kituo hiki cha mafunzo
leo hii inaashiria jitihada za Serikali katika kupanua na kuimarisha shughuli
za utafiti na utoaji wa mafunzo ya mifugo hapa nchini. Kwa kutambua umuhimu
huo, Serikali imeanzisha Taasisi (TALIRI na Wakala (LITA) ili kuongeza ufanisi
katika utafiti na utoaji mafunzo ya mifugo hapa nchini. Aidha, uwekaji wa jiwe
la msingi na ufunguzi wa jingo vimekuja wakati muafaka. Hii ni kutokana na
kupanuka kwa huduma za utafiti na mafunzo ya mifugo katika mikoa yote ya Kanda
ya Ziwa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Geita na Simiyu ambayo kwa pamoja
ina jumla ya Wilaya 32. Hii pia ni kwa kutambua kuwa idadi kubwa ya mifugo
inapatikana katika mikoa hii.
Ndugu
Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, nimeelezwa kuwa kutokana na mabadiliko ya muundo wa
Wizara na Idara zake, Kituo hiki kimehama mara mbili. Mwaka 1994 ambapo kituo
kilihama kutoka Malya na kwenda Ukiliguru na mwaka 2005 kikahamishwa na kuja
hapa kilipo sasa yaani Mabuki. Kwa sababu hiyo kituo hakikuwa na majengo yake
wala eneo la kufanyia utafiti na shughuli nyingine pamoja na miundombinu
mingine hali iliyochangia kuchelewa usimamizi wa shughuli za utafiti hadi
ilipofika mwaka 2008. Nina imani kuwa baada ya hapa, Taasisi itatumia
kikamilifu eneo walilopatiwa na Wizara ambalo lina ukubwa wa takribani hekta
1,000 kwa shughuli mbalimbali za utafiti wa mifugo kwa ufanisi. Hii ikiwa ni
pamoja na hekta 10 zilizotengwa kwa ajili ya majengo ya Ofisi, makazi na
miundombinu mbalimbali ya kiutafiti. Ni imani yangu kuwa maeneo haya na
rasilimali zake zitatumika na kulindwa kikamilifu kwa maslahi ya Taifa.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu,
ninafahamu kuwa TALIRI inatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya utafiti kwa fedha kutoka Serikalini kupitia Tume ya Taifa ya
Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Hii ni pamoja na ujenzi wa maabara ya nyama
ambayo tunaweka jiwe la msingi leo na nyumba mbili za watumishi hapa TALIRI-
Mabuki, kazi ambayo ilianza mwaka 2012/2013. Ninafahamu kuwa TALIRI Mabuki
ilipata jumla ya Tshs. Milioni mia nne na hamsini na tano (455,000,000/=)
kutoka COSTECH kwa ajili ya ujenzi wa maabara na nyumba tatu (3) za watumishi
za daraja la pili. Nafahamu pia kuwa tayari jumla ya shilingi 435,959,945.00
zimekwishatolewa kwa ajili ya maabara (Tshs. 69,863,370.00 ns Tshs
270,096,575.00) kwa ajili ya maandalizi ya awali na ujenzi wa nyumba tatu (3)
za watumishi za daraja la pili na nina imani zimetumika tayari kwa kazi
zilizokusudiwa.
Aidha,
nina taarifa kuwa ujenzi wa maabara umekamilika kwa asilimia 98% na nyumba
umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95%. Napenda kuwapongeza kwa mara nyingine
kwa uadilifu na uwajibikaji mzuri. Nachukua fursa hii kuiomba COSTECH kumalizia
sehemu ya fedha ambazo hazijatumwa kwenu ili kuweza kukamilisha ujenzi huu
pamoja na kununua vifaa kwa ajili ya maabara hii.
Ndugu Mkuu wa Mkoa,
najua kuna changamoto za kukosa umeme, maji na vifaa vya maabara katika kituo
hiki na gharama za awali zinakadiriwa kuwa shilingi milioni 21.7 kwa ajili ya
kuweka umeme na maji. Niendelee kumuomba Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH atusaidie
tena kufadhili katika kazi hii. Ama kwa hakika COSTECH tutawakumbuka kwa kazi
nzuri waliyoifanya lakini pia wanaimarisha wajibu wao kama
wadau muhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini. Pamoja na hilo , ninaiagiza TALIRI
ifanye utaratibu wa kupata gharama halisi za vifaa na mashine muhimu za maabara
hii ili iweze kufanya uchunguzi wa kisayansi inavyotakiwa. Ni wakati muafaka
kwa watafiti waliopo kutumia ubunifu wa kuandika miradi ya utafiti
itakayojumuisha kuimarisha maabara hii kwa ufadhili wa fedha za ndani na nje ya
Tanzania .
Ndugu
Wakurugenzi, kama sote tunavyofahamu,
upatikanaji wa fedha za utafiti na vitendea kazi ni changamoto kubwa kwa
Taasisi na vituo vya utafiti na mafunzo ya mifugo katika kukidhi matarajio ya
wadau katika sekta ya mifugo. Gharama kubwa zinahitajika kuchunguza, kuendesha
na kusimamia shughuli za utafiti na mafunzo ikiwa ni pamoja na kuhifadhi na
kuendeleza koo bora za mifugo kwa wafugaji, uhimilishaji, uzalishaji wa mbegu
za malisho, kufundisha wataalam wa mifugo na gharama za kawaida za uendeshaji
wa kazi za kila siku kwa vituo vyetu. Pamoja na juhudi za Serikali, nawaagiza
watafiti na wakufunzi waliopo kufanya juhudi kubwa za kuandika miradi na
machapisho mengi iwezekanavyo kutafuta fedha na mahitaji mengine ktuoka mifuko
na fursa mbalimbali zitolewazo ndani na njea ya nchi ili kupunguza utegemezi
kutoka Serikali kuu.
Ndugu Mkuu wa Mkoa,
Kimataifa bado tunakabiliwa ba tatizo la ufugaji usio na tija kubwa huku
ukilalamikiwa kutokana na uharibifu wa mazingira, migogoro na watumiaji wengine
wa ardhi kama vile wakulima na wahifadhi wa wanyamapori. Wafugaji wetu bado
wamezingirwa na umaskini mkubwa licha ya idadi kubwa ya mifugo nchini. Takwimu
zinaonesha kuwa Tanzania
ina ng’ombe milioni 22.8, mbuzi
milioni 15.6, Kondoo milioni 7.0, nguruwe milioni 2.01 na kuku milioni 58. Ni kupitia tafiti nzuri takwimu
zinaweza kuleta utajirisho mkubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Wageni Waalikwa,
kwa sasa Wizara yetu ina changamoto ya kudhibiti/kuzuia uvamizi wa maeneo ya
mashamba unaofanywa na wananchi wanaozunguka mashamba ya Taasisi zenu. Wananchi
hawa huchunga mifugo shambani bila idhini nah ii inahatarisha afya na usalama
wa mifugo ya Taasisi pamoja na uharibifu wa miundombinu. Ni vyema Taasisi zenu
zikatafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na changamoto hii kwa kushirikiana na
uongozi wa Wilaya husika ili utatuzi huu uwe na amani.
Aidha,
nachukua fursa hii kuagiza ukamilishaji wa upimaji na upatikanaji wa hati
miliki kwa maeneo yote nchini yanayomilikiwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi yakiwemo yale yaliyopo chini ya Taasisi na Vituo vyake. Kazi hii
ifanywe mapema iwezekanavyo ili kupunguza migogoro iliyopo kwa sasa na ambayo
inaweza kujitokeza kwa siku za usoni.
Ndugu
Mkuu wa Mkoa, upanuzi na ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha mafunzo ya mifugo
Mabuki ni moja ya ahadi zilizotolewa na Serikali Bungeni kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Hivyo napenda kuwajulisha kuwa ahadi hiyo
tunaitekeleza na tutaendelea kuzitekeleza kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
Hata hivyo, ni vyema kuwakumbusha kuwa miundombinu ya majengo hugharimu
Serikali fedha nyingi. Hivyo basi ningependa kuwaasa muendelee kuitunza
miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ndugu
Mkuu wa Mkoa na Wageni waalikwa, kwa muda mrefu
Serikali kuu imekuwa ikigharimia ka kiasi kikubwa mafunzo ya mifugo kwa wagani
ili wakasimamie sekta ya mifugo. Kazi hiyo kwa sasa inatekelezwa na Wakala na
sekta binafsi. Serikali kuu itabaki na jukumu la kutoa miongozo na sera
zinazohusiana na uendeshaji wa sekta ya mifugo nchini. Wote tunajua umuhimu wa
mafunzo kwa maendeleo ya Taifa hili na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi
mbalimbali za utoaji wa mafunzo hapa nchini kwa Taasisi za Umma na za binafsi.
Ndugu
Mkuu wa Mkoa, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi ilitoa ahadi Bungeni ya kupunguza pengo la wagani 11,303 wa
mifugo wanaohitajika vijijini hivi sasa. Nina furaha kuwa ahadi hiyo tutaweza
kuitimiza katika muda muafaka. Ujenzi wa majengo ya Bweni linaloweza kuchukua
wanafunzi 56 na Ukumbi unaoweza kutumiwa na wanafunzi 100 kwa wakati mmoja
katika kituo cha Mabuki kunafanya Wakala wa mafunzo (LITA) kuongeza uwezo wa
kudahili wanafunzi 2,300 kwa mwaka. Ongezeko la idadi ya wanafunzi katika
Kampasi za LITA kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza pengo la wagani lililopo
ili kufikia lengo la kuwa afisa ugani mmoja wa mifugo kwa kila Kata na kila
Kijiji.
Ndugu
Mkuu wa Mkoa, Serikali ilianzisha Wakala wa Mafunzo
ya Mifugo ikitegemea mambo kutoka kwenu ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi
ya Serikali. Kwa sababu hiyo, naomba kutoa nasaha zangu kwa Jumuiya ya Chuo kwa
ujumla kama ifuatavyo:
§ Chuo
kiendeshwe kibiashara kwa kuanzisha miradi ambayo tazalisha na kujiendesha kwa
faida. Natambua kuwa mafunzo ya mifugo yanahitaji kuwa na aina mbalimbali za
wanyama kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Kwa mtazamo huo ni budi kufuga na
kutunza wanyama katika kiwango cha hali ya juu ili wanafunzi waweze kujifunza
kuwa ufugaji kibiashara unawezekana na kuwa unaqweza kupunguza umasikini na
kuchangia Pato la Taifa.
§ Uongozi
wa Chuo ujitahidi kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa ujumla ili kuendana na
taaluma inayotolewa. Aidha, ni vyema Chuo kikajipanga kuanza mchakato wa
kuandika miradi mbalimbali ambayo inaweza kufanywa kituoni. Miradi hiyo itaweza
kuwasaidia kupunguza utegemezi wa ruzuku toka Serikalini.
Ndugu
Mkuu wa Mkoa, pamoja na kutoa mafunzo ya mifugo kwa
wagani, lakini pia kituo hiki cha LITA wakishirikiana na TALIRI watafute mbinu
ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wafugaji wanaozunguka eneo hili la Mabuki. Hapa
nigeomba uongozi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kupiita Halmashauri zao kukaa
pamoja na Uongozi wa Taasisi hizi mbili kuona namna Wilaya zitakavyoweza
kutumia miundombinu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi hizi katika
kuwahudumia wafugaji. Nina imani wafugaji wetu wakipatiwa stadi za ufugaji bora
wa mifugo wataweza kuinua kipato chao na
Taifa kwa jumla. Ninapenda kusisitiza kuwa utoaji wa mafunzo kwa wafugaji uwe
ni wa kudumu kwa kuwa hii ni njia rahisi ya kuwafikia walengwa.
Aidha, ningependa kuwaasa watumishi wa
Taasisi hizi na watu wengine wote mlio hapa kuwa UKIMWI ni janga kwa Taifa
letu. Ugonjwa huu umepunguza sana
nguvu kazi ya Watanzania kwa kuathiri rika zote. Nawataka wote mzingatie
maadili mema na ushauri wa wataalamu wa afya na viongozi wa Dini ili tuweze
kuondokana na janga hili kwani utashi wa kuepukana na ugonjwa huu uko mikononi
mwa kila mmoja wetu.
Wageni
waalikwa, mabibi na mabwana, naomba nihitimishe kwa
kutoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza, COSTECH na wadau mbalimbali kwa
kuendelea kushirikiana na TALIRI na LITA ili Taasisi hizi ziweze kufanya
utafiti na kutoa mafunzo kwa wanafunzi na wafugaji. Aidha, nawatakia kila la
kheri watafiti, wakufunzi, Wafanyakazi, Wanachuo na Jamii yote inayozunguka
Taasisi za Mabuki katika kazi zenu za kila siku.
Kwa kumalizia napenda kuwatakia safari njema
wageni wote waalikwa mliofika kwenye uwekaji wa mawe ya mzingi katika majengo
haya ya TALIRI-Mbuki na LITA-Mabuki pamoja na uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo ya
Mifugo. Mungu awaongoze ili msafiri salama na kuzikuta familia zenu zikiwa
salama.
Kwa
pamoja tunaweza, kila mtu atimize wajibu wake.
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA
Post A Comment: