HAPA TIMU ZIKIKAGULIWA NA MGENI RASMI, TIMU HIZO ZILITOKA SARE YA GOLI 1-1 |
Mashindano ya UMISETA, kwa Mkoa wa Mwanza yamefunguliwa rasmi hapo jana na Kaimu katibu Tawala mkoa wa Mwanza Ndaro Kulwijira huku akiwaasa vijana hao wa Sekondari kucheza kwa kuzingatia nidahamu ya hali ya juu.
Zaidi soma katika Hotuba yake aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa michezo hiyo.
HOTUBA YA KAIMU KATIBU TAWALA WA MKOA WA MWAZA
WAKATI WA KUFUNGUA MASHINDANO YA NGAZI YA MKOA YA MICHEZO YA SHULE ZA
SEKONDARI TANZANIA (UMISSETA) NSUMBA SEKONDARI TAREHE 22 MEI, 2014
Katibu
Tawala Msaidizi wa Mkoa Elimu - Mwalimu Hamis Maulid
MaafisaElimu
wa Halmashauri
Mameneja
Viongozi
wa Vyama vya Michezo Mkoa
Wanamichezo
Ndugu
Wananchi; na
Wapenda
Michezo Wote.
Napenda kuchukua fursa hii
kukushukuru Katibu Tawala Msaidizi ambaye ni AfisaElimu wa Mkoa, na Viongozi
wenzako katika Seksheni ya Elimu kwa kunialika kufungua Mashindano haya ya Umoja
wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Nimeupokea mwaliko huu kwa furaha
kwa vile umenipa fursa ya pekee kuwaona na kuzungumza na hadhara hii ya
Wanafunzi Wanamichezo na Walimu wao. Aidha, nitumie fursa hii kuupongeza
Uongozi wa Nsumba na jumuia yote kwa maandalizi mazuri ya mazingira kwa ajili
ya mashindano haya. Ahsanteni sana!
Ndugu Viongozi na Vijana
Wanamichezo,
Leo tumebahatika kujumuika hapa
kupitia Utamaduni wa Michezo. Kwa utaratibu huu, ni dhahiri kwamba tunapata
nafasi ya kujenga Umoja wa Kitaifa wa Wanamichezo kupitia Michezo hii ya
UMISSETA kuanzia ngazi ya Vijana wetu wa Shule za Sekondari. Ni kweli kwamba
Michezo ni Burudani, lakini kwa sasa kutokana na mabadiliko ya Mazingira ya
Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii, Michezo ni Kipaumbele katika kutoa pia Ajira kwa
Vijana wetu, kukuza Biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano. Kwa mfano,
Nchi za wenzetu za Ulaya na Marekani, Nigeria, Togo, Ivory Coast, Cameroon
zinatumia kikamilifu nafasi hii ya Michezo kujitangaza Kisiasa na Kiuchumi.
Ndugu Wanamichezo,
Natambua
kwamba ninyi ni Wanafunzi ambao mnahitaji kukuza Taaluma na Vipaji vyenu. Moja
ya nafasi hizo ni Michezo. Ili Michezo iendelee kukua Nchini, ni lazima Ukuzaji
wa Vipaji vya Michezo uanzie Mashuleni. Ndiyo maana Michezo ni sehemu ya Mtaala
wa Masomo yenu. Kama ambavyo tunawataka mfanye bidii sana katika masomo yenu,
fanyeni bidii pia na kukuza Vipaji vyenu katika Michezo mbalimbali.
Ndugu Wanamichezo,
Michezo inatufundisha Ushindani wa
Kistaarabu, Ushindani unaozingatia Sheria na Kanuni, Ushindani unaojenga
urafiki badala ya uhasama; Ushindani unaoleta Upendo badala ya Chuki na
Ushindani unaoleta Amani badala ya Shari. Kwa sababu hiyo Mwanamichezo wa leo
anayo nafasi ya kupata mafundisho muafaka na hazina ya uzoefu mkubwa wa
Ushindani wa Kistaarabu kutoka kwenye Michezo, vitu ambavyo vinaweza kumfanya
kuwa Mtanzania bora wa kesho. Mwanamichezo anakubali ama Kushindwa au Kushinda.
Waswahili husema“Asiyekubali Kushindwa Si Mshindani”.
Wanamichezo bora ni Watu Wasikivu,
wenye nidhamu na Watiifu. Ninyi Vijana ambao ndio Viongozi wa kesho wa Taifa
letu mnahitaji sana kujijengea nidhamu na maadili ya hali ya juu ili muweze
kuendana na hali ya maisha ya ushindani yatakayokuwa yanawakabili. Nidhamu,
inamuwezesha Mtu kufanya kazi zake kwa mpangilio mzuri unaofuata Taratibu zote
za kazi kwa wakati. Hii ndiyo njia ya uhakika ya kufikia malengo yoyote yale na
kupata mafanikio.
Aidha, kwa njia ya Michezo,
nidhamu Shuleni itaongezeka na matarajio yetu ni kuwa nidhamu hiyo itajitafsiri
pia katika matokeo mazuri kwenye Taaluma. Matarajio ni kuwa, Wanafunzi watakuwa
na mahusiano mazuri zaidi kati yao na Walimu wao na wale wote wanaopata
Burudani ya Michezo. Ama tunatarajia kuwa wataendelea kuwa Watu wenye Nidhamu
katika Utu Uzima wao, ili hatimaye tuwe na Taifa la Watu wenye nidhamu ya
kutolewa mfano.
Ndugu Wanamichezo,
Tangu zama za kale Michezo ilikuwa
ni sehemu ya Maisha ya Jamii. Jamii moja ilijipambanua na Jamii nyingine
kutokana na ushupavu na ushujaa wake katika Michezo. Dhana hiyo ya kale bado
inaendelezwa kupitia Sera ya Michezo kwa njia ya kisasa zaidi. Sera ya
Maendeleo ya Michezo inayaainisha madhumuni ya Michezo wakati huu kuwa ni: Kujenga na kuimarisha Afya Bora kwa wote; Kujenga Tabia ya Ushirikiano, Upendo, Undugu
na Uzalendo; Kujenga Uhusiano, Uelewano
na Mshikamano Kitaifa; Kujenga Moyo wa Kishujaa na Kujihami na Kukuza
Ukakamavu, Ujasiri na Kujiamini; Kuburudisha;
Kulitambulisha na kulitangaza Taifa letu nje ya Mipaka yake; na
Kumjenga Mwanamichezo kuwa mtu imara Kiakili
na Kiroho (kuanzia Utotoni hadi Utu Uzima). Kwa mtiririko huu, napenda
kusisitiza kuwa Shule zote, kuanzia za Awali, Msingi, na Sekondari, viwe na
Viwanja vya Michezo mbalimbali. Hii ni njia ya kuwatambua na kuwaendeleza
Vijana wenye Vipaji Maalum ili hatimaye Washiriki kwenye Mashindano ya Kitaifa
na Kimataifa. Aidha, Halmashauri zetu za Miji, Manispaa, Vijiji zihakikishe
kuwa maeneo yaliyotengwa kwa Shughuli za Michezo yanatumika kwa shughuli hiyo.
Aidha, Viwanja vilivyopo viimarishwe na vitunzwe ipasavyo. Ndugu Wanamichezo,
Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha
kwamba mnapofurahia kushiriki katika Michezo hii, ni lazima mkumbuke pia kuwa
furaha yenu itaweza kudumu kama mtatambua kuwa kuna mpinzani mkubwa kati yenu
aitwaye Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Kila mmoja wenu anaelewa vya kutosha juu
ya Adui huyu. Ni wajibu wangu kama Kiongozi na Mlezi wenu kuwakumbusha juu ya
hatari inayowakabili msipochukua tahadhari ya kutosha. Kumbukeni UKIMWI bado
unaenea kwa kasi kubwa sana hasa miongoni mwa Vijana wa Rika lenu kuliko Rika
lolote jingine. Niwakumbushe kwamba kataeni kumalizwa na Ugonjwa huu. Msikubali
kukatishwa masomo na msikubali kutenganishwa mapema na Familia zenu. Kwenu
ninyi, njia bora pekee ni kusubiri hadi wakati muafaka wa kuwa na ndoa zenu.
Wekeni bidii katika masomo, kwani muda ukifika yote yatajipanga vizuri.
Nitumie fursa hii kuwakumbusha
kuepukana na matumizi ya dawa za kulevya
kama vile bangi, mirungi na cocaine kwa imani ya kuwa dawa za kulevya
huwapatia nguvu na mzuka wa kushindana,
huko ni kujidanganya. Vijana wengi hasa
wanamichezo waliojaribu kutumia dawa za kulevya michezoni wameathirika na
wamekuwa mataahira. Shirikisho la vyama vya michezo duniani limekataza kabisa
matumizi ya dawa hizo na ukigundulika ni kufungiwa maisha na ushindi
kunyanganywa. Nawaomba walimu na wanafunzi kuwabaini wale wote watakaojihusisha
na utumiaji wa dawa za kulevya na kuwachukulia hatua kali za kiidhamu na
kisheria
Ndugu Wanamichezo,
Nimeelezwa kuwa baada ya Michezo
hii yapo Mashindano ya Kanda ya Ziwa ambapo Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu
hukutana ili kuimarisha mahusiano ya Vijana wa Shule za Sekondari na kuunda
timu moja ya Kanda. Ni muhimu Timu zetu zijipange kushiriki vizuri na kutuletea
undindi a kishindo. Ni Vizuri sasa Timu hizo ziandaliwe vizuri ili zikashiriki
kama Washindani na si Wasindikizaji.Kushiriki kwetu kunatujengea umahiri katika
kujenga upeo wa akili za Vijana wetu na kujenga mahusiano mazuri ya kikanda .Natoa
rai kwa Mashirika, Vyama vya Michezo na watu wengine kushiriki kwa
kuchangia kufanikisha ushindi wa timu zetu za Mkoa.
Ndugu Wanamichezo,
Mwisho napenda kukumbusha kuwa
umahiri katika jambo lolote lile hufikiwa kwa kujifunza na kufanya mazoezi
mengi, kwa bidii. Napenda kuwapongeza Walimu na Waamuzi na wote walioziandaa
Timu hizi ambazo leo zinashindana hapa. Nawapongeza sana Wanamichezo wa Timu
zilizoteuliwa kushindana hapa. Natumaini mliteuliwa kwa kustahili na katika
Michezo hii mtapata nafasi ya kuonyesha kuwa kuteuliwa kwenu hakukuwa kwa
Bahati. Onyesheni Umoja, Onyesheni Upendo, na Onyesheni“Fair Play” katika
mashindano haya. Kumbukeni kwamba Michezo ni Afya, Michezo ni Furaha na Michezo
ni Ajira.
Ndugu Wanamichezo, Wageni
Waalikwa,
Baada ya kusema hayo, napenda sasa
nitamke kuwa,Mashindano ya Umoja wa Michezo
Shule za Sekondari UMISSETA kwa mwaka 2014
yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni
kwa Kunisikiliza
Post A Comment: