Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa mauaji yaliyofanywa
katika mji wa Mpeketoni, Pwani ya Kenya hayakufanywa na kundi la wapiganaji wa
kiisilamu la Al Shabaab.
Kauli ya Rais Kenyatta inakuja kupitia kwa televisheni siku moja baada ya
kundi hilo kukiri kufanya mauaji yaliyotokea Mpeketoni Jumapili usiku.
Kenyatta emesema kuwa kuna ushahidi kuonyesha kuwa shambulizi hilo lilipangwa
vyema na kwamba wanasiasa walihusika nao.
Al Shabaab lilikiri katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ndilo lilifanya
mauaji hayo Jumatatu jioni.
Alisema kuwa ujasusi ulitolewa kuwa mashambulizi hayo yangefanyika lakini
hawakuchukua hatua zozote kuzuia mashambulizi hayo.
Rais amesema kuwa maafisa waliohusika tayari wameachishwa kazi na kwamba
watashitakiwa. Amesema kuwa kwa sasa wanachunguza wanasiasa waliohusika na mauaji
hayo ili sharia iweze kuchukua mkondo wake.
Mauaji zaidi yalifanyika usiku wa kuamkia leo licha ya taarifa ya Al Shabaab
kusema kuwa washambuliaji walioshambulia Mpeketo walikuwa wamerejea salama
nchini Somalia.
Uharibifu mkubwa ulishuhudiwa katika mji huo huku washambuliaji wakichoma
hoteli na kituo cha polisi pamoja na kuteketeza magari waliyoyatumia kwa usafiri
wao.
Kenyatta amesema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanaochochea uhasama miongoni
mwa jamii.
Hata hivyo Kenya katika siku za hivi karibuni imekuwa katika hali tete ya mashambulio ya kigaidi likiwepo shambulio kubwa lililowahi kutokea katika Jengo kubwa la Westgate la Jiji Nairobi na kusababisha vifo vya watu kadhaa na mamia wengi kujeruhiwa.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kipigo wanachokipata nchi hiyo ni kutokana na kupeleka wanajeshi wake Nchini Somalia kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi
Post A Comment: