ZOEZI ZA UKAGUZI WA MIZANI LIKIENDELEA

Wakala wa Vipimo (WMA) wa Vipimo Tanzania imeendelea na zoezi la utoaji wa elimu  pamoja na uhakiki wa mizani kwenye vyama  mbalimbali vya  wakulima ( AMCOS) Wilayani Masasi Mkoani Mtwara ikiwa ni maandalizi ya msimu wa korosho pamoja na mazao mengine kama vile choroko, mbaazi pamoja na ufuta. Akizungumza na Kaimu Meneja  Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John  alisema kwa muda wa siku nne tayari wametembelea vyama vya msingi  35 na kukagua jumla ya mizani 105, kati ya hizo mizani iliyokutwa sahihi ni 72 na jumla ya mizani 33 ilikutwa na mapungufu hivyo hazitaruhusiwa kwa biashara mpaka zitengenezwe na mafundi na kuhakikiwa upya na Wakala wa Vipimo ili ziweze kuruhusiwa kwa ajili ya kutumika kibiashara.

Bi. Iren, alitaja baadhi ya  majina ya vyama hivyo kuwa ni Temeke, Tuaminiane, Mshikamano, Mpindimbi, Chamali, Chigugu, Mkaramani, Mumbaka, Masunge, Chamaka pamoja na Nami. “ kila kituo tunatoa elimu inayohusu matumzi sahihi ya mizani, namna ya kutunza mizani pamoja na kuhakiki mizani inayotumiwa na vyama vya wakulima ( AMCOS) ili vyama hivyo vitakapotoa zabuni kwa mafundi mizani iwe ni ile tu iliyopimwa na kuonekana na hitilafu na siyo kupewa zabuni ya mizani yote  yaani iliyosahihi na isiyosahii, na hii itampunguzia mkulima gharama “ alisema bi. Irene.

 Katika hatua nyingine, bi Iren amewasihi baadhi ya wakulima wanaolalamikiwa kuweka mawe, kokoto pamoja na mchanga kwenye Korosho, Ufuta, Mbaazi pamoja na Choroko kwa ajili ya kuongeza uzito  waache tabia hiyo mara moja sababu Sheria ya vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi wote kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara.

 Irene alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo  kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara pia Wakala wa Vipimo imeongeza stiker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.

Alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani  kwa ajili ya kuwaibia wakulima adhabu ni kuanzia laki moja hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa, endapo kesi itafika mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja shabaha ikiwa ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha  na siyo kupunjwa  na wafanyabiashara wajanjawajanja.

Tunaimani Tanzania ya viwanda itafanikiwa tena sana endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumzi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokea wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao yenyewe , hivyo vyote vikizingatia matumizi ya vipimo sahihi viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima na mfanyabiashara  kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli  na mleta haki katika biashara ni kipimo sahihi  kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo vinginevyo.
 
 

Axact

Post A Comment: