HILI NI SHAMBA LA MZALENDO AITWAE SEBASTIAN NGONGOSEKO LILILOPO MKOANI MWANZA KATIKA WILAYA YA MAGU MAARU KWA ULIMAJI WA MBOGA MBOGA TU.

UCHUMI WA TEGEMEZI: NI SAWA NA KUJARIBU KUVUKA BAHARI
KWA MTUMBWI ULIOTOBOKA.

Na: Atley Kuni – Mwanza.

Je, umewahi kusikia, au kushuhudia urafiki wa kweli kati ya paka na panya; au kati ya simba na mbwa mwitu na mwanakondoo? Kama umeshuhudia utakuwa mtu wa pekee, kwasababu hilo si jambo la kawaida.

 Tunasoma katika vitabu vya dini kwamba litaweza kutokea tu baada ya siku ya kiama, ambapo Dunia ya sasa itaharibiwa na ndipo simba na mbwa mwitu watacheza na mwanakondoo, na mtoto mdogo ataweza kuchezea tundu la nyoka bila hofu ya kudhurika.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa enzi zetu, kama kutatokea urafiki wa aina yoyote baina ya wanyama hawa hasidi, basi jua wazi kuwa huo si urafiki wa kweli; bali ni urafiki wa kuwindana kwa mbinu, ili mnyonge kati yao aweze kuliwa.  Hata mamba hulia machozi anapotaka kumla binadamu kana kwamba anamhurumia.

Hivyo ndivyo tulivyo uhusiano katika ubia wa maendeleo kati ya nchi tajiri na nchi zetu masikini, ambapo kwa mtazamo wa juu juu tu utafikiri ni ubia wa kweli, wakati sivyo.

Sii ubia wa kweli kwasababu tangu kale, dhana inayotawala katika nchi tajiri ni kwamba umaskini wa nchi za dunia ya tatu ni matashi na sharti kuu kwa maendeleo ya nchi tajiri.  Iweje leo nchi hizi ziruhusu kwa hiari nchi maskini ziendelee?

Urafiki wa ki “paka na panya” kati yetu na nchi tajiri unatokana na umaskini wetu katikati ya utajiri wa rasilimali tusizozitumia, na ambazo zinanyemelewa na nchi hizo, pamoja na jasho letu kwa maana ya nguvu kazi.

Kama mamba hawa wala watu hakuna njia nyingine ya kuupata utajiri huo isipokuwa kwa njia ya kujipendekeza ili waweze kukata hatamu za udhibiti wa mali hizo, wazipore kwa ahadi ya misaada yenye masharti magumu yanayotupokonya uhuru wetu katika nyanja zote muhimu za maisha.

Hatujasahau jinsi watemi wa zamani walivyodanganywa wakauza nchi kwa kupewa zawadi ndogondogo kama vile shanga, vioo, bunduki na hata pombe wakasaini mikataba iliyowapokonya haki ya nchi na haki ya utawala.  Shanga na pombe ya leo ni misaada ya fedha kwa njia ya ufadhili ili “kuinua” uchumi au “kupiga vita” umaskini.

Zawadi ya fedha (misaada) tunayoahidiwa kupewa au kupokea siku hizi inaambatana na masharti mageni kwetu, ambayo ni pamoja na kubinafsisha sekta ya Umma, kupunguza thamani ya fedha, kupunguza matumizi ya serikali kwa kuondoa ruzuku kwa bidhaa muhimu na huduma za kijamii kama vile tiba, elimu n.k.

Kuhusu soko huria na kufungua milango kwa wawekezaji kuvushwa nje ya nchi; kudumisha utawala bora kwa vigezo vya nchi za Magharibi kama njia ya kujenga, kutetea na kulinda demokrasia na Uhuru wa mtu binafsi nchini.

Tunafananishwa na mitumbwi iliyokwama mchangani baada ya bahari kupwa, na kwamba misaada tunayopewa na kupokea ni sawa na kujaa kwa bahari na kuifanya mitumbwi yote iliyokwama ielee.  Kwa lugha yao ni kuwa, “arising tide floats all boats”

Lakini ukweli unabakia palepale, kwamba kwa mitumbwi yenye matundu, au kwa watu masikini wasio na uwezo wa kununua mitumbwi, kujaa kwa bahari kunaashiria kifo cha majini bahari itakapojaa.  Na anayetuzamisha ni yuleyule tunayemwomba ushauri, msaada na mikopo, kwasababu hatapenda nasi tuvume baharini kama avumavyo yeye.

Tujiulize, chini ya sera hizi, tumepata nini tangu tuzipokee miaka ya 1990? Tumejifunza nini?

Hatujaona bahari kujaa wala mitumbwi yetu kuelea; badala yake tunanyang’anywa makasia na mitumbwi yetu kupondwa pondwa na sisi kuvunjwa miguu ili punde bahari itakapojaa tushindwe kuelea wala kuogolea kujinusuru, tumezwe na maji na kufa.

HAYA NDIO MAZAO YAPATIKANAYO KATIKA SHAMBA HILI.
Angalia jinsi tunavyopondwa pondwa kwa ulaghai mkubwa; chini ya sera hizi, kati ya mwaka 1981 idadi ya nchi masikini sana duniani (LDSs) imeongezeka kutoka 21 hadi 38 barani Afrika badala ya kupungua; idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imeongezeka kutoka watu 124 mwaka 1961 hadi milioni 168 barani Afrika, katika zama hizi za “sayansi na teknolojia”, huku tukijidanganya juu ya kukua kwa uchumi (kama uchumi umekuwa kwanini basi vitu kama kupunguza wafanyakazi?)

Afrika inazidi kupinda mgongo kwa mzigo wa deni la nje (linalotokana na misaada ya kukomoa) ambalo limeongezeka kutoka dola billioni 48.9 za Marekani 1978 kufikia dola 230 mwaka 1988, dola bilioni 265 mwaka 1999 na dola bilioni 366 mwaka 2002.

Kwa Tanzania pekee, deni hilo limeongezeka kutoka dola 1,500 miaka ya 1970 hadi bilioni 8 mwaka 2002, mbali na riba inayoambatana na deni hilo .

Sii hivyo tu, ufa kati ya maskini na matajiri nchini umepanuka kwa asilimia 40 na kujenga matabaka katika jamii ya “walio nachi, na wasio nacho” (kuna watu nchini hii wanaishi kama vile wapo ahera na wengine hawana uhakika wa mlo wa siku moja)

Vivyo hivyo, idadi ya maskini barani Afrika inaongezeka kwa kasi ya kutisha, kutoka watu milioni 271.2 mwaka 1987 hadi watu milioni 306.6 mwaka 1997.

Katika hali kama hii, kuna nini cha kushangilia? Kwanini tumekubali kutendewa hivyo?

Njia moja ya kumteka na kumdhibiti mtu mstaarabu (asiyependa vurugu kama sisi) ili akutii na kukusujudu ni kumpa mkopo ambao una hakika hataweza kuurejesha mara moja ili aendelee kuwa mdeni wako.

Kwa njia hii utakuwa umefanikiwa kumfanya mtumwa na kuweza kumdhibiti kiasi cha kumfunga kamba kama mfugaji amfungavyo kamba mbuzi shingoni kumpeleka mnadani kuuzwa.

Vivyo hivyo, nchi tajiri, kwa kutumia mashirika ya Kimataifa kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimebuni mtindo wa kuziteka nchi maskini uitwao “mtego wa Deni” na kuzamisha makucha yake kwa kuzilazimisha kupokea masharti magumu yanayoambatana na mikopo hiyo.

Maelezo kuhusu jinsi utumwa huo mpya unavyoendeshwa yanatolewa na mwandishi Chery Payer, katika kitabu chake kiitwacho “Mtego wa Deni” kwa kusema:-

“Mfumo huu unaweza kufananishwa na utumwa kwa ngazi ya mtu binafsi.  Katika mfumo huu wa Utumwa wa Deni, Mtumishi (Nchi/ mateka) hawezi daima kuruhusiwa kutumia Uhuru wake kujinasua kutoka utumwani, kwasababu mwajiri huyo huendelea kumkopesha mahitaji yote (ili kumpumbaza na kumdumaza asifikiri wala kujipeleleza), na mara nyingi kwa riba kubwa, juu ya mshahara wake ndogo (pato dogo la nchi) usiokidhi mahitaji yake ya maisha”.
MCHE MMOJA WA PILIPILI HOHO HUZALISHA KILO GRAM NANE NA HUDUMU KWA MWAKA MMOJA.

“Lengo la mwajiri huyo si kukusanya au kulipwa deni lote mara moja, wala si kuruhusu mtumishi huyo afe kwa njaa (kwani atapata wapi mwingine wa kumkamua?) bali ni kumfanya aendelee kuwa kibarua mdaiwa wa kudumu aliyekata tamaa ya kuwa huru siku moja kutokanana na uzito wa deni asiloweza kulipa na mshahara mdogo usiokidhi maisha, licha ya kupinda mgongo kuzalisha kile kikubwa asichokula na kula kike kidogo asichozalisha.”

Mtindo huu ndio unaotumika katika ngazi ya kimataifa ambapo nchi huru masikini zinashindwa kulipa madeni yake ya nje kutokana na bei ndogo ya bidhaa zake katika soko la nje na kuzifanya watumwa wa wakopeshaji.

Hii ni kwasababu nchi zinazotoa misaada ndizo hizo hizo zinazopanga bei za mazao yetu katika soko la dunia zipendavyo.  Na kwa hila za kuendeleza utumwa wetu, bei hizo zinakuwa ndogo makusudi tusiweze kulipa mikopo tunayopewa.  Tutaendelea kukumbatia nchi zetu zitabaki maskini daima, huku wakulima wetu wakiendelea kupinda migongo mashambani kukidhi matakwa ya WB na IMF badala ya kukidhi mahitaji yao na ya uchumi wa nchi.

Ni kujidanganya, na ni umbumbumbu, kudhani kwamba tunapendekeza kwa taasisi za fedha za kimataifa kutokana na taasisi hizo kutoa machozi ya mambo tukiangalia.

Ni vipi tumeingia katika mtego huo? Nitaelezea kwa Ufupi:-

“Mtego huo unawekwa pale amfungavyo kamba mbuzi tunaposhauriwa kununua kwa fedha za kigeni bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi  kama vile, teknolojia, vipuri vya viwandani na kilimo; vifaa vya kuunganisha vitu vilivyotayari na visivyo tayari, mipango, wataalam, washauri, mafundi na wengineo, kana kwamba nchi haina wasomi katika nyanja hizo.

NGONGOSEKO KATIKA UTUNZAJI WA MAZINGIRA HAWAPO NYUMA HII NI SEHEMU YA MANDHARI SAFI SHAMBANI.
Vyote hivyo lazima vinunuliwe katika soko la dunia kwa fedha za kigeni.  Biashara ya kubadilishana badhaa kupigwa marufuku wa madai ya mtindo huo kupitwa na wakati.

Kwa jinsi mfumo wa soko la dunia ulivyo, na kutokana na bei ndogo ya mazao yetu tunayopewa kwa hila katika soko hilo, ni wazi kwamba nchi zetu zitaendelea kuwa na migogoro ya upungufu wa fedha za kigeni na hivyo madeni hayatalipika, huku riba yake ikiongezeka.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Zamani wa Zambia , Keneth Kaunda, waliwahi kuzishauri nchi masikini zikatae kulipa madeni hayo ya uonevu, ambapo wadai walitikisika kwa kiwango Fulani.  Leo kinyume chake tunasema kulipa madeni (hayo) ni uungwana huku tukifa na tai shingoni.  Hivyo ni nidhamu ya woga; na kama alivyosema Julius Kaisari (Ceasar), waoga hufa kabla ya kifo chao.  Tumepoteza nguvu ya kudai haki zetu kutambuliwa, tutakufa kabla ya vifo vyetu.  Na pale rushwa inapokithiri (na hata bila rushwa), ndivyo tatizo linavyozidi kukua.

Hapo, tunalazimika kukopa zaidi bila kupenda kwa masharti magumu zaidi yanayokaribia kuuza uhuru wa nchi.  Mradi wa Umeme IPTL – TANESCO ni mfano mmoja kati ya sakata nyingi zenye utata nchini.

Lakini potelea mbali; unamwendea mkopeshaji wako ambaye ndiye pia mshauri wako juu ya kufufua uchumi wa nchi.

Anachekelea na kukupatia fedha na vifaa, lakini kwa sharti kwamba utalipa mkopo huo kutokana na kilimo (kwasababu huna viwanda) kwenye ardhi ambayo bado unaiita ni ya mababu zako.

Unapokubali kuchukua mkopo huo; tayari umekuwa mtumwa kwenye ardhi yako mwenyewe.  Na kwa kuwa deni ni kubwa, lisilolipika na gharama za kulihudumia, masharti yake na bei kubwa ya bidhaa unazoagiza na kulazimishwa kulipa, kamwe huwezi kulipa deni hilo katika uhai wako.

Tumefikia njia panda kutokana na mkanganyiko huu.  Tufanye nini?  Baadhi ya wasomi wanaona pengine njia pekee ya kujinasua ni kufuata mfumo wa uchumi mchanganyiko wenye udhibiti makini.  Hata hivyo, tatizo la mfumo huu ni kwamba, si rahisi kudhibiti uchumi kama huo ndani ya sekta ya uchumi inayotawaliwa na wawekezaji kutoka nje wenye nguvu, kwani sera za soko huria zinawapa uhuru wa kupuuza udhibiti huo bila kudhurika, na wakati mwingine wako radhi kukataa kudhibitiwa na Serikali iliyotia sahihi bila kudadisi mikataba ya kimataifa kuhalalisha uendeshaji wa shughuli zao nchini.

Mtazamo mwingine ni ule wa kupunguza nguvu ya wawekezaji kutoka nje kwa kuwalazimisha waingie ubia na wazawa, na pengine serikali yenyewe.

Licha ya mfumo huu kuwa mzuri, hauwezi kutekelezwa, kwanza ni kwasababu serikali imepiga marufuku dhana ya uzawa; pili, masharti ya soko huria na ya wawekezaji yanaitaka serikali kujiondoa katika shughuli za biashara.

Hata kama kusingekuwa na vizingiti kama hivi, ugumu unakuja kwamba si rahisi kuelewa ni nani atamdhibiti mwingine katika ubia wenye pande mbili zisizo na nguvu sawa – yaani kati ya serikali au wazawa dhaifu na wawekezaji wenye Nguvu.  Kama ilivyotokea katika nchi za Magharibi huko nyuma, na kama asemavyo mchumi mashuhuri Keneth John Galbraith katika kitabu chake, “The Industrial State ” ni kuwa “…katika dunia ya sasa nguvu, kauli na udhibiti wa biashara na viwanda umehama kutoka kwa washika dau kwenda kwa mameneja wa vyombo vya fedha ambavyo mameneja hao wanapaswa kuvifurahisha”

Hapa kwetu, mifano hai ni pamoja na menejimenti za Mgodi wa Almasi Mwadui na Shirika la Umeme nchini TANESCO ambapo Serikali, licha ya kuwa na hisa, haina sauti; wala maagizo yake kuhusu uendeshaji wa taasisi hizo hayasikilizwi.

Ukweli ni kwamba, katika hali tuliyonayo, nchi maskini ni wabia chekechea kwa mashirika makubwa ya kuhodhi ya kimataifa yanayotuzidi uwezo kwa kila hali.  Mashirika hayo yanayowakilisha Serikali za nchi mama, ni nguvu tosha kuweza kupambana na serikali mwenyeji.

Ni kwasababu hii matakwa ya mashirika hayo yataendelea kutawala uchumi bila kujali kilio chetu kwa vile yanasaidiwa na nguvu ya fedha, siasa na diplomasia za nchi mama.  Kama asemavyo Reginald Mengi wa Makampuni ya IPP, “Ukoloni safari hii hautakuja kwa mtutu wa bunduki, bali kwa kuteka akili zetu”

Bila kuelewa nini kilicho mbele, tunaweza kufurahia kujengwa kwa barabara za lami nchini kwa fedha za misaada na mikopo kutoka nje; lakini ni kazi bure kama juhudi hizi hazitaenda sambamba na juhudi za kuwezesha mwananchi wa kawaida kuingia katika ulingo na kuwa mtumiaji wa barabara hizo katika kuinua maisha yake.

Kwasababu zisizofahamika, juhudi hizo hazipo kwa sasa.  Barabara hizi si kwa matumizi ya kusafirishia mazao ya wakulima walio wengi kutoka shambani, bali ni kwa ajili ya biashara za wenye uwezo unaovuka mpaka wa nchi moja hadi nyingine.

Vivyo hivyo, hatuna viwanda vya kutosha (vingi tumeviua tukawa tegemezi) vya kutengeneza bidhaa kutoa matumizi makubwa ya barabara hizi.

Tunachosema ni kwamba bila kuwawezesha wakulima wawe washiriki wazuri katika shughuli za uchukuzi, barabara hizi kwa sasa zitawanufaisha wafanyabiashara wachache wa kigeni na wenyeji wenye uwezo, lakini deni la mkopo wa barabara hizi litaendelea kulipwa na wakulima wasiozitumia.

Maendeleo, (wakopeshaji wetu wanatuambia) ni kwa watu (si kuabudu miradi) kwa ajili ya watu wenyewe; na kwamba maendeleo ya uchumi na maendeleo ya jamii hayawezi kutenganishwa.  Kwa hiyo mipango ya maendeleo ni lazima ianze na watu, mahitaji yao , matarajio ya uwezo wa kuwaendeleza vinginevyo ni maendeleo bandia.

Kwa maneno mengine ni kwamba, mipango ya maendeleo katika nchi maskini kama Tanzania lazima ianze na mahitaji muhimu ya wananchi kama vile maji, ardhi, chakula, afya, makazi na elimu.

Kwa bahati mbaya tunavipa vitu hivi kiti cha nyuma katika maendeleo; tunajali miradi zaidi kuliko maendeleo ya watu, hasa wale wa vijijini.  Aidha, dhana ya “uchumi wa mitumbwi kuelea” haitufikishi mbali kwani wanaoifanya bahari kujaa ndio hao hao wanaotoboa mitumbwi yetu ili, kwa hofu ya kuzama, tuendelee kuwatetemekea na kuwasujudia.

Ni dhana potofu ambapo kuipokea na kutumia ni sawa na kutaka kuvuka bahari kwa mtumbwi uliotoboka.  Kama alivyosema mwandishi mashuhuri wa riwaya, Ayi Kwei Armah, katika kitabu chake “The beautiful ones are Not Yet Born” hapajatokea watu wenye moyo wa kuwaokoa wengine isipokuwa wao wenyewe, sii hapo kale, sii leo.

Tuige ujanja na ujasiri wa ndege Eneke wa kitabu cha Mwanariwaya mkongwe barani Afrika Chinua Achebe, “Things Fall Apart” aliyehofia uhai wake kwa kuzungukwa na wawinda ndege na kusema; “kwa kuwa binadamu amejifunza kupiga shabaha bila kukosa, nimejifunza kuruka bila kutua” (Since men have learnt to shoot without missing, I have learnt to fly without perching)

Kwa kuwa nchi tajiri na mashirika yake mumiani zimezigeuza nchi masikini uwanja wao wa kupiga shabaha, hatuna budi kujifunza kuruka bila kutua, vinginevyo tutaangamizwa.  Na hili liwe changamoto kwa viongozi wetu.

© Right to   0718 086171 au Email:kuniatley@yahoo.com na mmiliki wa kuninews.blogspot.com





Axact

Post A Comment: