![]() |
Barack Obama |
Bunge la Marekani linakutana tena leo kujaribu kutafuta suluhisho la mgogoro wa bajeti unaotishia kuitumbukiza nchi hiyo katika mdororo wa uchumi. Jee kuna matumaini yoyote?
Kizungumkuti cha bajeti bado kinaendelea nchini Marekani baada ya mazungumzo ya dakika za mwisho kumalizika bila ya makubaliano. Wajumbe wa vyama vya Demokratic na Republican jana walishindwa kufikia mwafaka licha ya mwito uliotolewa na Rais Obama.
Hata hivyo kiongozi wa Seneti inayodhibitiwa na wajumbe wa chama
cha Democratic Harry Reid amesema mazungumzo yataendelea kufanyika.
Amesema bado pana tofauti kubwa baina ya pande zote mbili.Lakini
mazungumzo yanaendelea. Ameeleza kuwa bado pana muda wa kufikia
makubaliano na wanadhamiria kuendelea na mazungumzo.
Hapo awali Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden alikutana na
kiongozi wa maseneta wa chama cha Rebulican Mitch McConnell kwa ajili ya
mazungumzo yaliyoashiria matumaini ya kuepusha hatua za kupandishwa
kodi kwa Wamarekani wote na kukatwa kwa mfuko wa matumizi ya kijamii kwa
kiwango kikubwa .Hatua hizo zitaanza moja kwa moja hapo kesho ikiwa
suluhisho halitafikiwa.Kwa usemi mwingine Marekani itaingia katika
mdororo wa uchumi na kusababisha athari katika uchumi wa dunia.
Rais Obama amewalaumu Republican kwa kuweka mkazo katika kuyalinda
maslahi ya matajiri kwa kulipinga pendekeo la kupandisha kodi kwa
matajiri.Obama amesema jambo la kipaumbele kwa Republican ni
kuishughulikia nakisi kwa uthabiti wote. Lakini ameeleza kuwa
wanachoonyesha ni kuhakikisha kwamba uamuzi wa hapo awali wa kuwaondolea
kodi matajiri kwa muda unaendelezwa. Rais Obama amewataka Republican
watoe pendekezo ili kuhakikisha kwamba kodi hazipandi juu kwa Wamarekani
wa tabaka la kati na pia kuhakikisha kwamba posho kwa ajili ya
wasiokuwa na ajira zinaendelea kulipwa kwa watu milioni mbili.
Hatavivyo kwa upande wao Republican wanataka nakisi ipunguzwe kwa
kuukata mfuko wa kijamii kwa kiwango kikubwa.Suala la utatanishi baina
ya Republican na Democrats ni iwapo viwango vya kodi vya sasa vidumishwe
au la kwa Wamarekani wote au kwa wale wenye vipato vya kati ya dola
laki mbili nusu hadi laki nne kwa mwaka.
Lakini kiongozi wa Maseneta wa chama cha Republican Mitch McConnell
ameeleza matumaini juu ya kufikiwa suluhisho .Seneta McConnell amesema
watafanya bidii kubwa ili kufikia mwafaka.
Ikiwa hadi hapo kesho makubaliano hayatafikiwa Rais Obama atatumia
njia ya kuitisha kura juu ya mpango utakaowezesha kuvidumisha viwango
vya kodi vya chini kwa familia zenye vipato vya chini ya dola laki mbili
na nusu kwa mwaka. Mpango huo pia utawezesha kuendelea kuwalipa posho
Wamarekani milioni mbili wasiokuwa na ajira.
Post A Comment: