Mwenyekiti wa Tume ya
Umoja wa Afrika, AU, Nkosazana Dlamini-Zuma, ameelezea kusikitishwa na hali
ilivyo Sudan Kusini, kufuatia kuzuka kwa mapigano katika mji mkuu wa nchi hiyo,
Juba, siku ya Jumapili.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na kuchapishwa katika
gazeti la Sudan Tribune, mwenyekiti huyo amesema ana wasiwasi hasa na hali ya
usalama wa wananchi.
Mapigano yalizuka katika mji wa Juba, Jumapili jioni kati
ya vikundi vyenye silaha katika kambi ya jeshi na mapigano hayo yaliripotiwa
kuendelea Jumanne, huku milioni ya bunduki ikisikika katika maeneo yote ya mji
wa Juba mbali na kuhakikishiwa na serikali ya Sudan Kusini kuwa imedhibiti hali
hiyo.
Dlamini-Zuma ameitaka serikali ya Sudan Kusini na makundi
mengine yanayohusika katika mapigano hayo kujizua na aina yoyote ya kuendelea
kwa mgogoro huo.
Pia amezitaka pande zinazohusika na mgogoro huo kutafuta
suluhisho la amani kutokana na tofauti zao, "kwa kuheshimu utawala wa
sheria, haki za binadamu na uhalali wa kikatiba", akisema AU iko tayari
kusaidia kutafuta suluhisho la hali ya sasa.
Wito wa AU umekuja wakati Marekani ikizitaka pande
zinazohusika katika mgogoro wa Sudan Kusini kujizuia na ghasia na kutafuta
suluhisho la amani.
Mjumbe maalum wa Marekani Donald Booth alitumia
mawasiliano ya Twitter siku ya Jumatatu akitaka kuwepo kwa hali ya utulivu,
akisema migogoro ya kisiasa lazima imalizike kwa njia ya mazungumzo na sio
vurugu.
Rais Salva Kiir amemshutumu naibu wake wa zamani, Riek
Machar, kwa kuchochea jaribio la kutaka kuiangusha serikali yake.
Mawaziri kadha wa zamani wamekamatwa, wakihusishwa na
jaribio hilo, ambapo mawaziri wengine hawajulikani walipo.
Bwana Kiir ametangaza amri ya kutotembea ovyo usiku
katika mji wa Juba, ambapo maeneo mengi yenye pilikapilika za kibiashara,
yamekimbiwa kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, mazingira ya jaribio hilo hayako bayana, huku
kukiwa na taarifa zinazokinzana na kauli rasmi ya serikali kuhusu tukio hilo,
zikidai kuwa msuguano wa uongozi katika chama tawala, SPLM katika wiki za
karibuni ulisambaa hadi katika jeshi, SPLA, na kuchochea mapigano kati ya
wafuasi wa Bwana Kiir na Machar.
Jumatatu, walinzi wa rais waliizingira nyumba ya Bwana
Machar katika eneo la Amarat, na kuharibu sehemu kubwa ya nyumba hiyo. Hakuwa
nyumbani wakati huo na mpaka sasa hajulikani alipo.
Maafisa wa afya wanasema watu wapatao 26 wamethibitika
kufariki dunia katika hospitali ya Juba, wakati zaidi ya watu 113 wametibiwa
kutokana na majeraha ya risasi.
Post A Comment: