Kiongozi wa Albino asema hukumu ikishindikana Duniani, itatolewa Mbinguni.
Watu 15 Wanashikiliwa na Polisi, nayo pikipiki iliyotekeleza mpango yabambwa na polisi, uchunguzi unaendelea.
WANANCHI WA NDAMI TARAFA YA MWAMASHIMBA WAKIMSIKILIZA MKUU WA MKOA WA MWANZA. |
WAANDISHI WA HABARI SHEILA SEZI NA GRACE CHILONGOLA WAKIWA NA MAMA PENDO EMMANUEL, AMBAYE HIVI SASA ANA MAJONZI BAADA YA MTOTO WAKE KUTWALIWA NA WATU HAO. |
Serikali mkoani Mwanza imesema hakuna kulala hadi mtoto Pendo Emmanuel miaka 4(Albino) apatikane, kufatia tukio la kutekwa na watu wasio julikana toka tarehe 27, Desemba, 2014 katika kijiji cha Ndami, Tarafa ya Mwamashimba Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza na kisha kutoweka naye kwenda kusiko julikana hadi sasa.
ALFREDY KAPOLE MWENYEKITI WA ALBINO MKOA WA MWANZA AKIONGEA KATIKA KIKAO HICHO |
SUNGU SUNGU KWENYE KIKAO. |
MWENYEKITI WA CHAWATA MKOA WA MWANZA NA MWENYEKITI WA ALBINO MKOA WA MWANZA WALIPOKUWA WAKIONGEA NA MAMA YAKE NA PENDO EMMENUEL. |
MKUU WA
MKOA.
MKUU WA MKOA WA MWANZA MAGESA MULONGO. |
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magesa
Mulongo, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kijijini hapo na kuwahusisha wananchi wakijiji hicho pamoja
na uongozi wa Wilaya na Mkoa huku akitaka kujua hatua iliyofikiwa na wana nchi
hao katika kuwabaini walifanya unyama huo.
Mtoto Pendo alitekwa na watu wasiojulikana mnamo usiku
wa tarehe 27.12.2014 majira ya saa nne usiku akiwa amelala na wazazi wake huko
Nyumbani kwao na kisha watekaji kutoweka naye na kwenda kusiko julikana hadi
sasa, huku taarifa za Polisi zikionesha jumla ya watu kumi na watano (15),
wakiendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Akihutubia wananchi wa kijiji hicho Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza, alisema ni tukio la kusikitisha kwani toka mwaka 2007 hakuna tukio
la namna hiyo lililo wahi kutokea katika Wilaya hiyo na tukio la mwisho lililotokea
lilimkumba mwananchi wa Wilaya hiyo aliyekuwa amesafiri kwenda Mkoani Shinyanga
kwa shughuli zake.
Amesema kiburi walicho nacho watekaji hakiwezi
kuwa nje ya mipaka ya kijiji hicho cha Ndami bali mpango mzima unajulikana kwa
wenyeji na ndio maana ilikuwa rahisi kufanya unyama huo “Kiburi cha watekaji
kimo humu humu haiwezekani mtu kutoka mbali aje atekeleze tukio hapa kijijini
bila yakuwa na wenyeji lazima kuna mtu au watu walioshirikiana na wahalifu hao”,
alisema Mulongo na kuongeza “ kwa mazingira ya Nyumba ya kina Pendo ilipo kule
hakuna sehemu yakutokea na kama mliona pikipiki inaranda randa mchana,.. iweje
mshindwe kuitilia shaka? Hapana, hii haikubaliki!
mimi nimekuja kuwaambia nataka Pendo apatikane na sio vinginevyo, nawapa siku
tano ijumaa nitarudi hapa mniambie Pendo yuko wapi! Alisema mkuu huyo wa Mkoa
akionesha kusononeshwa na tukio hilo.
“Mbona mifugo inapo ibwa inapatikana”? Aliwahoji viongozi
wa sungu sungu na kusema haiingii akilini kusema wakati wa tukio la utekaji
sungu sungu wote walikuwa wamekwenda kula chakula na ndipo kadhia hiyo
ilipotokea, mkuu wa mkoa, alihoji kufatia kauli iliyotolewa na kiongozi wa
sungu sungu kuwa wakati wa tukio askari wote wa sungu sungu walikuwa wamekwenda
kula majira ya saa tatu na tukio kutokea saa nne.
MWENYEKITI
WA ALBINO MWANZA.
Awali akielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo,
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa Ngozi mkoani hapa Alfred Kapole,
alisema inasikitisha kuona wanadamu wakiwauwa binadamu wenzao kama vile wanyama
bila hata woga na vyombo vya maamuzi vikishindwa kutoa hukumu kwa wakati huku
akielekeza lawama zake kwa mahakama na Mkemia Mkuu. “Mh. Mkuu wa mkoa
inasikitisha kuona miongoni mwa kesi 72 zilizokuwa mahakamani, ni kesi 3 tu
ndizo zilizokwisha kutolewa hukumu” alisema Kapole, na kuongeza ingekuwa ni
kesi ya Wabunge wameshindana kwenye masuala ya uchaguzi ingekuwa imekwisha
hukumiwa lakini kwakuwa ni mlemavu wa ngozi,
basi kupuuzia kumekuwa kwingi
mno. Alisema kapole.
Akinukuu maneno kutoka katika kitabu cha Biblia,
Kapole alisema hata kama hukumu zitashindwa kutolewa na wanadamu hapa Duniani, naamini
Mungu wa Mbinguni kuna siku haki itatendeka kwa kuwa “Kitabu cha Mika 3.3-7 kinaeleza
juu ya hukumu watakayo ipata watu walao nyama za watu bila woga. Kesi
zinaendeshwa Polisi wanajitaihidi sana lakini mkemia watendaji wa ofisi ya
mkemia mkuu wanatuhujumu kwa kuita nywele zetu albino ni za Midoli, aling’aka Kapole wakati
akielezea kusikitishwa na ofisi ya Mkemia mkuu wa serikali pindi inapo pelekewa
Nywele.
Mwenyekiti Kapole pia aliomba kwa yeyote aliye na Mtoto
huyo kumrejesha na kama wamemdhuru basi warejeshe hata mwili wake ili matanga
yaweze kufanyika, akatumia fursa hiyo kumomba Rais wale wote waliohukumiwa
kunyongwa wanyongwe ili kuepusha kuendelea kula chakula cha serikali bure.
RC ITIKADI
KATIKA KAZI.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa aliwataka wanachi
kuweka mbali itikadi zao za namna yoyote na kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha zoezi zima la kuwasaka walio
husika na utekaji wa mtoto Pendo Emmanuel, ambao unasimuliwa kuleta siamanzi
kubwa ndani ya jamii ya wana Kwimba na watanzania lakini pia kuchafua taswira ya nchi mbele ya
mataifa mengine ya Dunia . Huku akiwaonya watu wa haki za binadamu kuacha kupaza
sauti za kuwatetea wahalifu. Tanzania inatajwa kuwa kinara cha ukatili huo
tangu mauwaji hayo yalipo zuka mwanzoni mwa miaka ya 2006/2007.
TAKWIMU ZA
KIMATAIFA.
Kwa Mujibu wa takwimu za kimataifa zinaonesha ni
asilimia 2% tu ya watu ambao huzaliwa na ulemavu wa ngozi ndio hufikia na
kusherekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao, huku pia takwimu zikionesha katika nchi
za Afrika mtu mmoja (1) kati ya elfu mbili (2000) huzaliwa wakiwa na ulemavu wa
ngozi wakati katika marekani ni mtu mmoja kati ya elfu kumi na saba ndio huishi
na ulemavu wa ngozi.
Mauaji ya Albino katika Tanzania yanaonekana
kushamiri katika Mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo imani za kishirikina zikitajwa
kuwa chanzo kikubwa cha mauwaji ya hayo lakini pia yale yalio wahusu vikongwe yanayo
husishwa na masuala ya kujipatia utajiri
wa haraka suala ambalo sio la kweli, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mauwaji
yalianza siku nyingi japo kuripotiwa
katika mamlaka za serikali na vyombo vya habari ilianza mwaka 2006/2007.
Hivi sasa zipo asasi za kiraia zinazo jihusisha na
harakati za kupinga mauwaji hayo ikiwapo asasi ya Under The Same Sun ya Nchini Canada
na kwa Tanzania imeshakuwa na tawi toka mwaka 2008.
KAMANDA WA
POLISI.
Awali akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo
kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mulowola alisema tayari watu 15
wanashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani humo kwa mahojiano zaidi akiwapo baba
mzazi wa Pendo, lakini pia jeshi hilo limefanikiwa kuipata piki piki
iliyotumika kufanya unyama huo. “Hivi sasa tunawashikilia watu wapatao kumi na
watano na wanaendelea kuhojiwa na Polisi” alisema Mlowola na kuongeza kuwa huo
sio mwisho kwa kuwa jinai haina mwisho hata miaka ishirini tukio hili
litaendelea kuchunguzwa”, na kusema hata kama yeye atahamishwa au kustaafu
kijana atakayekuja ataendelea na kesi hiyo, hivyo wananchi waendelee kutoa
ushirikiano kwa kile wanacho kifahamu, alisema Mlowola na kusema tayari Jeshi
hilo mkoani hapa limetangaza kuto Milioni tatu 3 kwa atakayefanikisha
kupatikana kwa mtoto Pendo.
Mtoto Pendo alikuwa ni miongoni mwa alibino 74
waliopo katika wilaya ya Kwimba na alikuwa namba 9 katika suala la kupatiwa
ulizi.
Imeandaliwa
na Afisa habari Mwanza- Atley Kuni.