JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo
mkoani Rukwa. Ugonjwa umedhibitika kuwepo baada ya Vipimo vya Maabara
kuonyesha uwepo wa vijidudu vya homa ya uti wa mgongo kwenye sampuli za
wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Sumbawanga. Hadi kufikia tarehe
08/10/2013 jumla ya wagonjwa 21 wameripotiwa katika hospitali
ya Mkoa na kati yao wanne ( 4) wamefariki dunia
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania
hususani mikoa iliyo mpakani na mkoa wa Rukwa na vile vile wasafiri
wanaotarajiwa kwenda mkoani Rukwa.
Homa ya Uti
wa Mgongo inasababishwa na bakteria aitwaye Neisseria meningitidis.
Bakteria huyu ndiye anayeleta milipuko mikubwa ya Homa ya Uti wa mgongo.
Ugonjwa huu hatari unaathiri zaidi meninji na husababisha athari kubwa kwa
ubongo. Ugonjwa huu unapatikana kwa binadamu tu. Asilimia 50 za wagonjwa
hupoteza maisha iwapo matibabu hayataanzishwa mapema.
Dalili kuu ni Kukakamaa kwa
shingo, Homa kali, Kutokupenda mwanga mkali, Kuchanganyikiwa, Kichwa kuuma
pamoja na Kutapika. Ugonjwa huu unaweza kuathiri ubongo na kupelekea
kupoteza uwezo wa kusikia au kupoteza kabisa uwezo wa kuelewa na kunyambulisha
vitu mbalimbali. Iwapo ugonjwa huu utaathiri ubongo na meninje kwa kiasi
kikubwa, umauti hutokea. Dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2
hadi 10 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa huu
unaenezwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu kwa njia ya hewa au kwa
kugusa majimaji/mate kutoka kwa mtu ambaye tayari ni mgonjwa. Ugonjwa huu
unaenea kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine kwa urahisi na kwa kasi sana iwapo
mtu atakuwa karibu na mgonjwa mwenye maambukizi kwa muda mrefu. Uambukizo
unaweza kutokana iwapo mgonjwa atapiga chafya au mate ya mgonjwa huyu kuguswa.
Aidha kasi ya maambukizi pia inatokea iwapo mtu ataishi kwa karibu ndani ya
nyumba moja na mgonjwa na kushirikiana naye kwa kula chakula kwenye chombo
kimoja.
Ugonjwa huu unatibika iwapo mgonjwa atawahi
hospitalini na kupewa dawa.
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
- Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa
Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara hususan mikoa inayopakana na Rukwa.
Aidha taarifa hii pia imewakumbusha waganga wakuu warejee miongozo yao ya
kudhibiti Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo yaani namna ya utambuzi wa
mgongwa na, uchukuaji wa sampuli
- Kuimarisha
ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa,
Wilaya na maeneo ya mipakani.
- Kutuma
Timu ya Taifa ya Maafa ambayo imeenda kuungana na timu za Mkoa na Wilaya
za Rukwa katika kukabilana na ugonjwa huu. Aidha timu hiyo imeondoka
tarehe 10.10.2013
- Kutuma
chanjo pamoja na dawa na vifaa Kinga kwa mkoa wa Rukwa ili kuweza
kukabilana na ugonjwa huu
- Elimu
ya Afya inaendelea kutolewa katika maeneo ambayo yamekumbwa na
mlipuko na pia mashuleni, vyuoni, magerezani, nakwenye mikusanyiko na
msongamano wa watu. Aidha wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora zenye
madirisha yanayoingiza hewa na mwanga wa kutosha
- Kufungua
kambi maalamu mkoani Rukwa kwa ajili ya wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo
Wananchi
wanashauriwa kutoa taarifa pindi kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya
kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za
ugonjwa huu.
Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii na Wadau wengine wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha
ugonjwa huu unathibiwa mkoani Rukwa na kwa mikoa mengine.
Nsachris
Mwamwaja -Msemaji
12 Oktoba
2013
Post A Comment: