MBUNGE
wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu,
kuwaeleza waliokuwa wanachama wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for
Community Initiative (DECI) fedha zao zilizotaifishwa na serikali kutoka kwenye
taasisi hiyo ziko kwenye akaunti gani.
Mnyika
alisema kuwa wakati sakata la DECI linaanza mwaka 2009, serikali ilitaifisha
jumla ya sh bilioni 19, sawa na asilimia 40 ya fedha zote ambazo wanachama wa
taasisi hiyo iliyokuwa ikiendesha na kusimamia mchezo wa upatu walikuwa
wakidai.
Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara juzi Mtaa wa Mavurunza, Kata ya Kimara baada ya
kuulizwa swali na mmoja wa wananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha zao, Mnyika
alitoa tahadhari kuwa danadana inayotaka kufanywa na serikali inaweza kutia
shaka kuwa fedha hizo hazipo.
”Sasa
naomba nimjibu yule mwananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha za DECI.
Mtakumbuka hili suala nimekuwa nikitaka majibu yake bungeni, lakini kila mara
wanatumia kisingizio kuwa suala hili liko mahakamani.
“Juzi
baada ya hukumu kutoka tumemsikia Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu
akisema hawawezi kuwalipa wananchi walioweka fedha zao DECI,” alisema.
Kama
wanasema waliocheza DECI nao ni watuhumiwa, walipaswa kuhukumiwa, Gavana hasemi
hizo fedha sh bilioni 19 ambazo serikali ilizitaifisha na kuwekwa BoT ziko
kwenye akaunti gani.
“Kwa
sasa mahakama imesema mlipwe, serikali ndio walizitaifisha na kuziweka kwenye
akaunti BoT, wanapata wapi kigugumizi cha kuzilipa hizo asilimia 40 ambazo
tayari zipo?” alihoji.
Mbunge
huyo alisema kuwa wananchi waliopanda fedha zao wana haki ya kulipwa kwa sababu
zipo, zimeshikiliwa kwenye akaunti na serikali.
Alisema
kuwa fedha hizo zinapaswa kurejeshwa kwa msingi kwamba pamoja na mahakama
kuwahukumu waendeshaji wa DECI kuwa wahalifu, haikuwahukumu washiriki.
Aliongeza
kuwa DECI ilisajiliwa na serikali kupitia viongozi wake akiwamo Waziri wa Fedha
na Uchumi wa wakati huo, Mustafa Mkulo na kuhamasisha watu kujiunga.
Katika
mwendelezo wa ziara yake jana, Mnyika alimtaka Diwani wa Kata ya Msigani,
Logart Mbowe (CCM) kufuatilia haraka nyaraka zinazoonesha gharama za manunuzi
ya vifaa vya ujenzi (BOQ) wa daraja lililoko Mtaa wa Msigani, wilayani
Kinondoni.
Mnyika
alitoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Rems
Lutumo (CCM) kuwa ujenzi wa daraja hilo anautilia shaka kwa kuwa hadi unafikia
hatua hiyo hajui gharama zake.
“Ifuatilieni
hiyo BOQ haraka, pia ni lazima kuwekwe kibao kinachoonesha kuwa daraja hilo
lina uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa tani ngapi,” alisisitiza Mnyika.
Awali,
Lutumo alisema hadi sasa ofisi ya mtaa huo haijui gharama halisi za ujenzi huo,
huku wananchi wakihitaji kujua kwa sababu ni haki yao.
Mkazi
wa mtaa huo, Said Msati, alisema daraja hilo limejengwa chini ya kiwango, bali
viongozi hao walishindwa kumueleza mbunge ukweli, hatua aliyodai inatokana na
tofauti zilizipo kati ya diwani na mwenyekiti wa mtaa huo.
Alisema
miradi mingi ya maendeleo inakwama kukamilika kutokana na tofauti zao hizo,
huku akitolea mfano wa ujenzi wa kisima, aliodai unakwenda taratibu huku diwani
akidaiwa kukalia fedha.
Kuhusu
kero ya maji, Katibu wa kamati ya maji ya Msigani na Malambamawili, Evetha
Nchunga, alitoa taarifa kuwa wakazi wapatao 65,000 wamekuwa wakikabiliwa na
tatizo la maji tangu kujengwa mabomba ya Mchina miaka minne sasa.
Alisema
hivi sasa wakazi hao wamekuwa wakitumia maji ya mifereji ambayo si salama kwa
afya zao hususan watoto ambao hawana tahadhari.
Post A Comment: