![]() |
KATIBU WA UENEZI WA CHAMA CHA MAPINDUZI NAPE MNAWIYE, AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MSIMAMO WA CHAMA, HII NI BAADA YA HOTUBA YA JAJI WARIOBA ALIYO ITOA TAREHE 18.3.2014. |
Tarehe 18/03/2014 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba nchini Jaji Joseph Sinde Warioba aliwasilisha kwenye Bunge maalum la
Katiba rasimu ya pili ya katiba.
Toka awasilishe rasimu ile bungeni , kumekuwa na
maombi mengi sana ya kutaka kujua kama msimamo wa CCM juu ya baadhi ya mambo
hasa muundo wa muungano bado ni uleule.
Kwasababu ya maombi hayo CCM imeona bora kueleza kwa
mara nyingine tena msimamo na imani ya CCM juu ya swala zima la Muungano na
muundo wake.
Kimsingi CCM ndio waasisi wa
Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar. CCM inamasilahi makubwa na mapana na
Muungano huu kama waasisi pengine kuliko taasisi nyingi ndani na nje ya nchi
yetu.
Bado CCM inaamini changamoto za Muungano huu suluhisho
lake sio kubadili muundo wa Muungano bali ni kuufanyia maboresho muundo wa
muungano tulionao wa serikali mbili. Hivyo basi CCM bado inaamini muundo bora
kwasasa utakao dumisha muungano wetu ni muundo wa SERIKALI MBILI.
Kwakuwa kazi ya Warioba na Tume yake sasa imekwisha
rasmi, kuisha kwa kazi yao ni mwanzo wa awamu nyingine ya mchakato huu. Mwisho
wa kazi ya Tume sio mwisho wa mjadala juu ya Katiba tuitakayo bali ni mwanzo wa
awamu nyingine ya mjadala mpana na maboresho kama sio marekebisho ya kuondoa
mapungufu kwenye rasimu iliyowasilishwa.
Mwanzo wa awamu hii nyingine ni furusa nzuri ya kupima
kama kweli yaliyomo kwenye rasimu na maelezo ya ziada yaliyotolewa na Jaji
Warioba yana akisi maoni ya Watanzania walio wengi.
CCM ina amini awamu mbili zilizobaki kwakuwa
zinahusisha wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge maalum la Katiba, na hatimaye
itawahusisha wananchi wenyewe moja kwa moja kupitia kura yao, zitatumika vizuri
kutupa ni nini hasa matakwa ya Watanzania juu ya Katiba waitakayo na sio maoni
au matakwa ya wachache.
Wakati haya yote yakiendelea CCM bado tunaamini
Muungano huu ni muhimu ukadumishwa na kuimarishwa. CCM tunaaamini ili Muungano
huu udumu njia pekee kwasasa ni kufanya marekebisho kwenye Muundo wa serikali
mbili ili ujibu vizuri zaidi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na kukidhi
mazingira ya sasa.
Tunawaomba wanaCCM na watanzania kwa ujumla kuwa
watulivu katika kipindi hiki. Ni vizuri Watanzania tukavumiliana,tukashindana
kwa hoja tukitanguliza mbele uzalendo na masilahi ya kweli ya nchi yetu.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi
20/03/2014
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi
20/03/2014
(MM)
Post A Comment: