![]() |
MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DR.JAKAYA MRISHO KIKWETE, ALIPOKUWA AKIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA. |
Rais Jakaya Kikwete alibadili upepo wa
mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa
Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge
Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya
nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati
akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49
iliyokuwa na maneno ya 'kuuma na kupuliza' kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba, Rais Kikwete alisema suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama
katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio sahihi, nchi
inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge
hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake na
kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa
hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba
muundo huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM
inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.
Huku akichambua
kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa
vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema),
Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa za
kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
"Sababu ya kwanza ni kwamba muundo
huo ndiyo matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar. Sababu ya pili muundo
huo unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa
Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili."
Aliongeza, "Wapo wanaokubaliana na
tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa
msemo wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume
kwamba hazionyeshi ukweli huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu siyo
yangu." Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, "Watu
wanasema Watanzania waliotoa maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820 sawa na
asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu 303,844 sawa na asilimia
86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano na wala hawakuuzungumzia wakati
wa kutoa maoni."
Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje
asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya
kutaka Serikali tatu.
"Watu wanahoji mbona taarifa ya
tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa
maoni kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa
na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8,
Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7" alisema.
Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia
10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hawakuzungumzia
Muungano, bali mambo mengine.
"Watu wanahoji kama Muungano ni
jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa
hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili"
alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia sababu ya pili ya tume
kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili,
huku akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema;
"Nyinyi ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua.
Tume yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto
zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma."
Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa
kutafuta majibu mwafaka kuhusu changamoto za muundo wa Serikali tatu kwa sababu
maelezo ya tume kuhusu muundo huo hayana majibu.
Aliongeza, "Kupanga ni kuchagua.
Wanaounga mkono Serikali mbili wanasema mlolongo wa changamoto ulioanishwa na
tume kuhusu Serikali tatu hautapunguza matatizo bali utayaongeza kuliko ilivyo
sasa na wanasema changamoto hizo zinatatulika bila kuwepo Serikali ya
tatu."
Alisema kama mfumo wa Serikali tatu
ukipita ni lazima Serikali ya tatu ijengewe msingi imara kwa sababu haitakuwa
na chanzo cha uhakika cha mapato yake yatakayoiwezesha kusimama yenyewe na
haitakuwa na chombo cha kukusanya mapato zaidi ya kutegemea kukusanyiwa mapato
na nchi washirika.
"Kama tunataka Serikali ya tatu
lazima tuitengenezee misingi ya uhakika. Hivi nani atakudhamini kwa virungu,
pingu, magari ya kuwasha, majeshi au bunduki. Serikali hii ya tatu haidhaminiki
wala kukopesheka," alisema huku akitolea mfano jinsi mataifa kama Urusi
yalivyoanguka baada ya kujitenga.
Huku akifafanua jinsi kero za muungano
zilivyotatuliwa na kamati na tume mbalimbali mpaka kubaki kero sita, Rais
Kikwete alisema Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zimeamua kutumia
mchakato wa Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wakati Tanganyika na Zanzibar
zinaungana kulikuwa na mambo 11 ya muungano, baadaye kuongezeka hadi mambo 22
na kusisitiza kuwa mambo mengi yaliibuka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki mwaka 1977.
Alisema jambo ambalo Serikali hizo mbili
walikubaliana kuliondoa katika mambo ya Muungano ni suala la gesi asilia na
mafuta.
Ammwagia sifa Warioba
Alisema Jaji Warioba wa wajumbe wenzake
wa Tume ya Katiba wameandika Rasimu ya Katiba vizuri na kwa weledi wa hali ya
juu, na kwamba wametoa maoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha
Katiba tuliyonayo sasa.
"Katiba inayopendekezwa imejumuisha
dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tuliokuwa nao na
kuweka misingi mizuri kwa huko mbele tuendako," alisema.
Alisema Rasimu ya Katiba ni kitabu
kikubwa kilichosheheni mambo mengi kina kurasa 106, sura 17, hivyo wajumbe wa
Bunge la Katiba wanapaswa kusoma kila kitu na kuelewa na kuamua kwa utashi wao.
"Uamuzi wako siyo uamuzi wa
kuambiwa na mwenzako, unaulizwa na wenzako kwenye hilo tusemeje unasema na mimi
nimeambiwa, ebo! Umeambiwa, umefundishwa na mimi nasema akili za
kuambiwa..." alisema Rais Kikwete.
Mambo mengine
Pia Rais Kikwete aligusia suala la
mbunge kupoteza ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi kwa miezi sita mfululizo,
kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.
Alisema anaungana na wote wanasema jambo
hilo liangaliwe vizuri na kwamba anashauri kama akiwa kizuizi amepatikana na
makosa apelekwe mahakamani.
"Kwa mazoea ya duania ukomo
unawekwa kwa wakuu wa nchi, hawaweki ukomo kwa wabunge, Tanzania wanataka kuwa
wa kwanza," alisema Kikwete.
Kuhusu suala la ugonjwa alisema mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wake, hivyo siyo sahihi kumwekea
mgonjwa muda maalumu wa kuugua kwake.
Huku akicheka, Rais Kikwete alisema
kitendo hicho kitawafanya wabunge kuanza kutembea na dripu katika majimbo yao
kabla hawajapona vizuri.
Post A Comment: