![]() |
Pichani Mwenyekiti na Mkamu M/Kiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakiteta jambo hivi karibuni. |
Bagamoyo. Siku chache baada ya
kumalizika kwa Mkutano wa 13 wa Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe amesema kamati yake inashindwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na kubanwa na Ofisi ya Spika.
Kauli hiyo imekuja siku
chache baada ya Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigangwala kuongoza harakati
za kumng’oa Spika wa Bunge Anne Makinda kwa madai kuwa anaongoza Bunge kwa
upendeleo na hasa kwenye uendeshaji wa kamati. Alikusanya saini za wabunge
wapatao 30 ili waunge mkono hoja yake, ambayo kwa sasa inashughulikiwa na
Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Filikunjombe ambaye pia
ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya
kuwajengea uwezo Wajumbe wa PAC na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC),
yaliyohudhuriwa pia na Ndugai pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Alisema mara nyingi
kamati hiyo inapozihoji idara mbalimbali, Spika Makinda au Naibu wake, Job
Ndugai wamekuwa wakiwapigia simu na kuwataka kutoruhusu vyombo vya habari
kusikiliza majadiliano hayo, kitendo alichosema kuwa kinazorotesha uwajibikaji.
“Mara nyingi tumekuwa
tukipokea simu kutoka kwao zinazolalamikia utendaji wa kamati hii,” alisema na
kuongeza: “Hatua hiyo inatokana na kamati (PAC) kuwa na tabia ya kuruhusu
vyombo vya habari kuingia katika vikao vyetu wakati tunapokuwa tunahoji
watendaji wa idara mbalimbali. Wamekuwa wakitupigia simu na kututaka tusifanye
hivyo.”
Ndugai alisema kanuni za
Bunge zinaruhusu vyombo vya habari kushiriki katika vikao vya kamati za Bunge
lakini wanaandaa utaratibu wa ushiriki wao.
“Kuanzia sasa tunajaribu
kuangalia namna ya kuweka utaratibu ili kuvisaidia vyombo vya habari kupata
taarifa za matumizi ya fedha za umma bila ya kuathiri utendaji wa kamati,”
alisema.
Filikunjombe alipendekeza
kubadilishwa kwa kanuni ili vikao vya PAC na LAAC virushwe moja kwa moja katika
televisheni kama ilivyo mikutano ya Bunge ili kama kuna mtu anasema uongo
wananchi wamwone.
Alisema hali hiyo
itasaidia watendaji kuongeza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za
umma… “Inashangaza… maana tukiwaita watendaji kujieleza mbele ya kamati juu ya
matumizi ya fedha tunapigiwa simu na Spika Makinda au Naibu wake, hii inaondoa
dhana nzima ya uwajibikaji,” alisema.
Alisisitiza kuwa idara
hizo huwa zinaomba fedha za umma bila kificho kwa nia ya kuzitumia kwa mambo ya
msingi lakini ameshangazwa na hofu ya viongozi kuhojiwa wakati vyombo vya
habari vikiwapo.
Alisema umefika wakati
kwa Ofisi ya Spika kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini
ili kuwa na uwajibikaji.
“Ni vizuri kamati hizi
mbili zikaachwa zifanye kazi zake kwa sababu zina umuhimu mkubwa katika
usimamizi wa fedha za umma,” alisema Filikunjombe.

Post A Comment: