RAIS Jakaya Kikwete jana alizindua matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, yanayoonyesha kuwa Tanzania sasa ina watu 44,929,002, kati yao 43,625,434 wakiwa wa Tanzania Bara na 1,303,568 Zanzibar.
Akitangaza matokeo ya Sensa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jana, Rais Kikwete alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu.
“Kwa kasi hii, hadi kufikia mwaka 2016 tutakuwa jumla ya watu 51 milioni. Idadi hiyo yaweza kuonekana kuwa haina tatizo kwa nchi kama Tanzania, lakini huo ni mzigo kwa taifa, jamii na kwa uchumi,” alisema.
Alisema kuwa kwa kasi hiyo ya ongezeko la watu hapana budi kuwa na mikakati madhubuti na mipango mipya ya maendeleo kuanzia sasa.
“Kuna umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itazidi kushuka na ushindani katika rasilimali hizi chache tulizonazo utazidi kuwa mkubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lazima tulipe uzito stahiki suala hili la kupanga uzazi. Lazima ujue utazaa kipindi gani na watoto wangapi ili uweze kuwahudumia.”
Alisema takwimu za matokeo hayo zina maana kwamba Serikali ianze kujipanga kwa ongezeko hilo la watu na jamii kwa upande wake, ianze kujipanga kukabiliana nalo.
“Tukizingatia haya tutaweza kupiga hatua. Sisi serikalini tutaanza kupanga mipango yetu kwa kuzingatia matokeo haya. Nanyi wenzangu anzeni kujipanga kuchukua hatua,” alisema Rais Kikwete.
Alisema matokeo mengine yatatolewa Februari ambayo ndiyo yataonyesha mchanganuo wa jinsia, umri kiwilaya, kikata na kishehia.
Rais Kikwete alisema Sensa ya mwaka 2012, ni ya tano kwa Tanzania, ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na kulikuwa na watu 12,313,054; Tanzania Bara watu 11,958,654 na Zanzibar 354,400.
Sensa ya mwaka 2002 ilionyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya watu 34 milioni. Alisema tangu Sensa ya kwanza ilipofanyika hadi ya sasa, kuna ongezeko la watu zaidi ya 33 milioni.
Alisema hatua ya mwisho ya matokeo ya Sensa ya 2012 yanatarajiwa kutolewa Juni, 2013 ikiwa na mchanganuo wa taarifa zote muhimu zikiwamo za kiuchumi kwa kaya.
Axact

Post A Comment: