Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa Jeffrey Feltman amesema katika kikao cha Baraza la Usalama kwamba ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu umekuwa na taathira hasi kwa mazungumzo kati ya Wapalestina na Israel.

Akielezea hali inavyojiri katika Mashariki ya Kati, Feltman amesema, mazungumzo ya kusaka amani kati ya Palestina na Israel baada ya kupita miezi minne tangu yaanze yamefikia katika hali tete ambapo pande mbili zinajadili maudhui muhimu. Ameongeza kwamba, mwenendo wa mazungumzo hayo unakwamishwa na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi likiwemo eneo la Quds Mashariki na kwamba Umoja wa Mataifa unafuatilia kadhia hiyo kwa wasiwasi mkubwa. Afisa huyo wa UN ameeleza kwamba, maafisa wa juu wa kimataifa akiwemo Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine wamesisitiza msimamo wao kwamba vitongoji vya walowezi wa Kizayuni si halali na kubainisha kuwa, ujenzi huo unakinzana na sheria za kimataifa na unakwamisha mwenendo wa amani.

Feltman amesema, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanataka Israel isimamishe mara moja ujenzi huo na kusisitiza ulazima wa kuundwa nchi huru ya Palestina kama njia pekee ya kustawishwa amani na usalama wa eneo hilo.

Sisitizo la jamii ya kimataifa kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina ni kinyume cha sheria na kwamba hatua hiyo ya Israel ni pingamizi kwa mwenendo wa amani, kwa mara nyingine limeweka wazi utambulisho usio wa amani wa utawala huo na kukinzana kwake na sheria na kanuni za kimataifa.

Ijapokuwa malalamiko ya kimataifa dhidi ya siasa za kupenda kujitanua za Israel hasa ujenzi wa vitongoji yameongezeka, lakini utawala huo ghasibu bila kujali malalamiko hayo unaendeleza hatua hizo kutokana na uungaji mkono wa madola ya Magharibi hasa Marekani. Matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Nyumba wa Israel yanaonesha kuwa, Tel Aviv sio tu haijasimamisha ujenzi wa vitongoji kwenye maeneo ya Palestina bali pia inaendelea kujenga nyumba mpya na kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huku mazungumzo hayo yakiendelea. Auri Ariel amesema kuwa, sehemu kubwa ya ujenzi wa vitongoji vya utawala huo katika maeneo tofauti ya Palestina haikusimamishwa na bado unaendelea hata wakati wakati huu wa mazungumzo. Hii ni katika hali ambayo, Bunge la Israel limetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli hizo.

Kung'ang'ania Israel kujenga vitongoji hivyo licha ya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa ni kinyume cha sheria, kunabainisha kwamba utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu hauheshimu sheria na maazimio ya kimataifa na unaendeleza siasa hizo za kujitanua ili ufikie malengo yake haramu.

Lengo la utawala wa Kizayuni la kujenga vitongoji vya walowezi katika maeneo ya Wapalestina ni kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa maeneo hayo na kuyafanya yawe na sura ya Kizayuni ili uendelee kukalia kwa mabavu maeneo tofauti ya Palestina. Vilevile Israel kwa kujenga vitongoji hivyo vya walowezi wa Kizayuni, inakusudia kuyatenganisha maeneo ya Palestina ili izuie kivitendo kuundwa nchi huru ya Palestina.

Itakumbukwa kuwa suala la kuundwa nchi huru ya Palestina linahesabiwa kuwa ni haki ya mwanzo kabisa na isiyokuwa na shaka ya wenyeji wa asili wa ardhi ya Palestina, haki ambayo inasisitizwa pia na viongozi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Jeffrey Feltman.

 
Axact

Post A Comment: