HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO MHE. DKT. FENELLA MUKANGARA (MB), WAKATI WA KUFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA MAWASILIANO MKOANI TANGA TAREHE 3 FEBRUARI, 2014

Mhe. Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Fenera Mukangara alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa maafisa wa habari mkoani Tanga. ( Kaulimbiu ya Mkutano huo ni " MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA KUIMARISHA NA KUTANGAZA SHUGHULI ZA SERIKALI".
 

Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, akisalimiana na Mkurugezi wa idara ya habari maelezo Bw. Assa Mwambene, wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa mwaka wa Maafisa Habari wa Serikali, unaofanyika Mkoani Tanga.
Ndugu Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,

Ndugu Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO,

Wakurugenzi , Wakurugenzi Wasaidizi na Mameneja mliopo hapa,

Maafisa Mawasiliano,

Wageni Waalikwa,

Waandishi wa Habari,

Mabibi na Mabwana,

Habari za Asubuhi!!!

 

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma kwa kutuwezesha kusafiri salama kutoka katika vituo vyetu vya kazi nchini kote na kunikutanisha nanyi siku hii ya leo tukiwa na afya njema.  Naomba pia wote tutakiene Heri ya Mwaka Mpya wa 2014.

Kabla sijaendelea kuzungumza nanyi leo hii, kwa heshima naomba wote tusimame  na tukae kinya kwa sekunde chache tuwakumbuke na tuwaombee kheri kwa Mwenyezi Mungu, wenzetu – wana-mawasiliano na wanahabari waliotangulia mbele ya haki

 

Ndugu Naibu Katibu Mkuu na Washiriki wote,

Kwa kumbukumbu nilizonazo, hii ni mara ya tatu nakutana nanyi katika kikao kama hiki. Lengo kuu likiwa ni kutaka kukumbushana utekelezaji wa majukumu yetu yanayotukabili kila siku

Ninyi ni watu muhimu katika kuunganisha Serikali na Umma.na kufanikisha utendaji wenye tija ndani ya Serikalini Hili ni jukumu kubwa na la msingi sana, na sina shaka kwenu katika kulitekeleza. Nafahamu fika kuwa mnao uwezo wa kukidhi matarajio ya kile  tunachokihitaji.  Na huu ndio ni wajibu wenu hasa.

 
 
 
                                                                                      Naibu Katibu Mkuu wa Wizara HVUM,
                                                                                         Pro. Elisante Olle Gabriel. Jijini Tanga.

Ninyi nyote ni mashahidi na mnafahamu teknolojia ya mawasiliano inakua kwa kasi    kubwa. Swala la kujiuliza hapa ni kwa kiasi gani, sisi tunakwenda na kasi hiyo?  Natambua kazi nzuri mnayoifanya; lakini ni muhimu kutambua kuwa teknolojia haitusubiri kiutekelezaji. Kama ambavyo tumekuwa tunaelekezana  na kukubaliana kila tunapokutana Tumieni muda huu kuleta mabadiliko ya kiutendaji kwenye maeneo yenu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa malengo chanya.

Ndugu Washiriki,

Kama mnavyofahamu, kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Matumizi ya Tehama na Mitandao ya Kijamii katika kuimarisha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma”. Nina hakika mtakubaliana na mimi kwamba, Mitandao ya kijamii imekuwa mashuhuri na ina ufanisi  katika mawasiliano na ndiyo maana mmechagua kauli mbiu hii.

 

 
Mitandao ya Kijamii kama Facebook, twitter, Blogs, U-tube na mingine mingi imeonyesha kuwa na watumiaji wengi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, yakiwemo ya mijini na hata Vijini.  Hivyo basi nashawishika kusema wakati umefika sasa kwa Serikali hasa kupitia kwenu kuongeza maradufu matumizi ya mitandao hii ili kuendana na mahitaji ya jamii katika utoaji wa Taarifa kwa wananchi.

 

Katika hili, wahimiza mtumie pia fursa ya sms za mitandao mbalimbali ya simu kufikisha ujumbe sahihi na kwa wakati muafaka kwa wananchi

 

Nimeambiwa kuwa zaidi ya Maafisa Mawasiliano thelatini ( 30) kutoka katika Wizara na taasisi  za Serikali walipatiwa mafunzo juu ya namna ya kutumia mitandao ya Kijamii katika kipindi cha mwaka 2013 chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Wizara yangu.

 

Hali hiyo ni kiashiria kuwa, tayari juhudi hizi zinatakiwa kuendelezwa zaidi ili hatimaye sote tuweze kutumia vyema mitandao  ya Kijamii katika kutoa taarifa na kuwasiliana na umma.

Nihimize kila Wizara,Idara na Taasisi za Serikali taasisi kuhakikisha wasemaji wake wanapata mafunzo hayo kwa muda stahiki.

 

Kwa mara nyingine tena, natoa pongezi kwa  wale wote waliokwisha pata mafunzo ya namna bora ya Kutumia Mitandao ya kijamii na wale ambao wamekuwa wakiitumia kwa juhudi zao nikiamini kuwa watakuwa chachu kwenu nyote katika kuongeza hamasa ya matumizi yake katika kutoa taarifa kwa  wananchi kwa malengo chanya.

 

Nimeambiwa kwa wale mliopata mafunzo haya, baadhi yenu ndiyo mtakuwa walimu katika kikao kazi hiki, ambapo pamoja na mambo mengine mtajifunza kwa vitendo namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi.

 

Aidha, napenda kutoa wito kwa Maafisa Mawasiliano wa Serikali wote katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuendelea kujifunza kwa weledi mambo mbalimbali yatakayosaidia kuleta tija katika kutekeleza majukumu yenu ya kusimamia mawasiliano katika maeneo yenu ya kazi.

 

 

 

 

Ndugu Washiriki,

Jukumu kubwa mlilopewa ni kuwezesha  Serikali kupitia Ofisi zenu kufanya mawasiliano na Umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu  Sera na Miradi inayotekelezwa na Serikali yenye lengo la kustawisha maendeleo ya Watanzania

 

Kimsingi nyinyi ndiyo wasemaji wa Wizara, Idara na Taasisi zenu badala ya watendaji wakuu wa sehemu zenu za kazi.  Kwa kufanya hivyo, Serikali inatimiza wajibu wake wa kutoa haki ya msingi ya wananchi ya kupata habari hususan zinazohusu utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Serikali.

 

Napenda kutoa pongezi kwa wasemaji wa taasisi mbali mbali za Serikali mlioshiriki katika ratiba za Serikali kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya Habari kuhusu utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ambapo Wizara yangu ilishiriki kuratibu mikutano hiyo.

Nimeambiwa kuwa mikutano Mia moja na Hamsini (150) ya Taasisi za Serikali ilifanyika kati ya Mia moja na Tisini na mbili (192) iliyopangwa katika kipindi cha Julai - Desemba 2013 ikiwa ni utekelezaji wa maazimio mliyojiwekea katika mkutano wenu wa Dodoma uliofanyika Februari, 2013. Hongereni sana.

 

Nawapongeza sana mlioshiriki, kwani Umma umeweza kupata haki yao ya kikatiba ya kufahamu serikali yao inafanya nini katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya wananchi. Nimeambiwa kuwa ratiba ya mikutano ya Mawaziri inaendelea tangu Januari 17, 2014 ambapo hadi leo hii tunakutana, tayari mikutano 6 ya Mawaziri imefanyika.

 

Nawashukuru kwa kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya mikutano hiyo.  Napenda kutoa wito kwa Wasemaji wa Taasisi ambao hamkushiriki katika mizunguzoko ya awali ya mikutano yenu na waandishi kufanya hivyo, kwani mtakuwa mmetimiza wajibu wenu na maazimio mnayojiwekea katika kutekeleza shughuli zenu.

 


Maafisa habari wa RS Mza, na EAC, Wakifatilia
Jambo katika mkutano huo.
Kumekuwa na malalamiko ya kutokuridhika na namna ambavyo Serikali inatoa taarifa kwa umma ili kutosheleza mahitaji ya wananchi ya kupata habari zinazohusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambazo huchangiwa na fedha za walipa kodi. Mikutano ya aina hii ambayo inawahusisha nyie wasemaji wenye taaluma ya masuala ya mawasiliano pamoja na viongozi wa Taasisi zenu itasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa taarifa za Serikali kwa Umma.
 

Ndugu Washiriki,

Kama kauli mbiu ya Kikao chenu inavyosema “matumizi ya mitandao ya Tehama na Mitandao ya Kijamii katika kuimarisha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma” Napenda kuchukua nafasi hii kuwaasa kuwa tumieni fursa hii ya Kuwepo kwa mitandao ya Kijamii ili kukidhi kiu ya jamii ya kupatiwa taarifa mbalimbali za kuelimishwa na kuburudishwa.

 

Mkifanya hivyo,mtaweza  kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, natoa rai kwenu; kwa kila mmoja wenu na kwa  kwa nafasi yake ionyesheni jamii kuwa mnamudu majukumu yenu mliyopewa na mnao uwezo wa kuleta mabadiliko tarajiwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu iko katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Hili litawezekana tu pale mtakavyoendelea kujituma na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, na  pale mtakapo jibu hoja za wananchi kwa usahihi na kwa wakati na kwa tangaza mafanikio ya Serikali siku zote bila kuchoka na kuhakikisha wale waliojikita katika  kutangaza mapungufu tu hawafanikiwi.

Maelekezo yangu kwenu ni kwamba  kuanzia sasa ni vema tukawa na mfumo wa wazi wa kufanya tathmini ili kufahamu ni Wizara ipi au Taasisi ambayo hatuisikii kabisa katika kutimiza majukumu haya.  Maafisa Mawasiliano lazima muwe na “roadmap” ya nini kifanyike katika kuhakikisha kwamba tunauandaa Umma wa Watanzania kujadili na kufanya uamuzi kutokana na uelewa mpana na sahihi wa masuala yaliyo mbele yao ili kujiletea maendeleo.lakini pia kutekeleza  wajibu wao pia kama wananchi.

 

Nasisitiza pia toeni ushauri ulio sahihi, kwa haraka na wakati  ili kutoa majibu muafaka kwa Umma  hasa pale ambapo Vyombo vya Habari vinakuwa vimepotosha taarifa zenu. Hili lifanyike kwa vyombo vyote vya Habari vikiwemo Radio, Televisheni, Magazeti na Mitandao ya Kijamii pale inapolazimu ili kuondoa upotoshaji wa taarifa za Serikali unaosababishwa na ukuaji wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano. 

Hatuwezi kuwa na nchi ambayo kila mtu anaandika kile anachokijua bila kufuata misingi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji.  Taarifa zisizosahihi zikiachwa bila kujibiwa kwa wakati, zinaweza kuleta uchonganishi kati ya Serikali na Umma na hivyo kusababisha sintofahamu isiyokuwa na ulazima. Ili kufanikiwa katika hili, lazima nyinyi wenyewe muwe wenye weledi na ufahamu wa hali ya juu.

 

Ndugu Washiriki,

Nafahamu kuwa mna changamoto mnazokabiliana nazo. Wizara yangu imetoa Mwongozo wa Vitengo vya Mawasiliano ya Serikali ambao pamoja na mambo mengine umeeleza majukumu ya Vitengo hivyo na umuhimu wa Taasisi husika kutoa mahitaji ya raslimali watu, vitendea kazi na bajeti ya kutosha kutekeleza majukumu waliyopangiwa . Natoa rai kwa Watendaji Wakuu wa Serikali kuusoma Mwongozo huo na kusimamia utekelezaji wake.

 

Ndugu Washiriki,

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote mliofika katika kikao kazi hiki ambacho ninatukumbusha majukumu ya kiutendaji,ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuongeza tija katika mfumo wa Mawasiliano Serikalini.

Natoa Shukrani kwa Taasisi za Serikali zote zilizoweza kufadhili mkutano huu kwa namna moja au nyingine hususan TCRA, NSSF, PPF, TPA, PSPF,  TSN, SUMATRA, TANAPA, SSRA na TBC.

 

Ndugu Washiriki,

Mwisho niwatakie Kikao kazi chenye tija na kitakachowapa Dira katika utendaji wenu mkitilia maanani matumizi bora ya mitandao ya kijamii katika kutoa taarifa/habari kwa Umma kuhusu yale yanayo tekelezwa na Serikalikatika jitihada za kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Naomba sasa nitamke kuwa kikao cha Maafisa Mawasiliano kimefunguliwa rasmi. Nawatakia kila la heri na mafanikio mema.
 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Axact

Post A Comment: