Raia wa Uswisi Magd Najjar (kulia) akifikishwa mahakamani mjini Nairobi kushitakiwa rasmi kwa kuwa na mafungamano na al-Shabaab. Najjar ni mmoja wa washukiwa wengi wa al-Shabaab wenye utaifa wa nchi mbalimbali wanaodhaniwa wapo Kenya. [Simon Maina/AFP]


Jamii ya Kisomali nchini Kenya imelaumiwa sana kwa mashambulizi ya al-Shabaab, lakini wachambuzi wa masuala ya usalama wanaonya kwamba kuwasingizia Wasomali kunaongeza hatari ya mashambulizi ya baadaye kwani wanamgambo wa jamii nyingine wanaweza kufanya shughuli zao za kigaidi bila kufahamika.

 Aden Duale, mbunge wa jimbo la Dujis, alisema Wakenya kwanza huwashuku watu kutoka jamii ya Kisomali popote panapofanywa mashambulizi nchini Kenya. "Mashambulizi hayo kawaida huleta dhana potofu na kuyahusisha na jamii ya Kisomali, ingawa hakuna mtu aliyeandikwa usoni pake kwamba ni mwanachama (wa kundi la kigaidi).
Kuwailenga jamii ya Kisomali ni kutafuta majina na chuki dhidi ya wageni," aliiambia Sabahi. Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya usalama vya Kenya vimejibu mashambulizi ya kigaidi kwa kuwasakama wakimbizi, ikiwemo kuwakamata kwa wingi watu wa jamii ya Kisomali. Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilitangaza kwamba wakimbizi nchini humo lazima warudi kwenye kambi, kwani usajili na huduma zitasitishwa mijini. Siku ya Alhamisi (tarehe 20 Disemba), Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa liliitaka Kenya kujiepusha kuwalaumu wakimbizi kwa vitendo vya vurugu nchini humo.

Wakenya wana jukumu kubwa kwenye ugaidi "Uwanachama wa al-Shabaab umevuka mipaka ya jamii ya Kisomali," alisema Meja Mstaafu wa Jeshi la Kenya Bashir Haji Abdullahi, ambaye anafanya kazi ya ushauri wa masuala ya usalama. Al-Shabaab imewapa mafunzo watu wasiokuwa na asili ya Kisomali kupunguza uwezekano wa wanachama wao kukamatwa, alisema, akiongeza kwamba Wasomali wanazidi kukataa kujiunga na kundi hilo kutokana na mateso ya kivita. Kwa mujibu wa Boniface Mwaniki, mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi cha Polisi ya Kenya, washukiwa 1,900 wamekamatwa wakihusishwa na mashambulizi ya kigaidi nchini humo tangu mwezi Juni -- 1,200 jijini Nairobi, 400 Mombasa na 300 Garissa. "Tunao kizuizini na tunawachunguza watu kutoka jamii za Wakikuyu, Wabajuni, Wajaluo, Waluhyia na hata Wakamba," aliiambia Sabahi. Mamlaka zinasema Elgiva Bwire, Mkenya kutoka jamii ya Waluhya, ambayo ni jamii ya Magharibi, ni mfano mkubwa wa wapiganaji wa al-Shabaab wasiokuwa Wasomali. Bwire, ambaye umaarufu wake ni Mohamed Seif, alikiri mbele ya mahakama ya Nairobi hapo mwezi Oktoba 2011 kuwa mwanachama wa al-Shabaab na kuhusika kwake na mashambulizi yaliyoua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 18 kwenye kituo cha mabasi cha OTC jijini Nairobi katika mwezi huo.

Ahmad Iman Ali, amiri mkuu wa Kituo cha Vijana wa Kiislamu (MYC) kinachonasibishwa na al-Shabaab, anawakilisha wanamgambo wengine wasiokuwa Wasomali. Ali, anayefahamika pia kama Abdul Fatah wa Kismayu, anatoka jamii ya Wameru Mashariki ya Kenya na amekuwa akifanya kazi zake nchini Somalia tangu mwaka 2009, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2011.
Ripoti hiyo inakitambua kituo cha MYC kama mkono wa al-Shabaab wa mafunzo na utafutaji fedha nchini Kenya. Wapiganaji wa kigeni wa al-Shabaab Mkuu wa wilaya ya Garissa Mohamed Maalim alisema mamia ya watu wasiokuwa na asili ya Somalia wameorodheshwa kupigana chini kwa chini sambamba na al-Shabaab nchini Somalia tangu mwaka 2006. Kwa hakika, Wakfu wa al-Katab ambao ni kituo cha habari cha al-Shabaab, hivi karibuni waliongeza juhudi zao za mafunzo kwa kutoa mkururo wa mikanda ya video kuwataka mujahidina wa kigeni kujiunga na mapambano nchini Somalia.
Maalim alisema kuwa katika mwaka 2011, vikosi vya usalama viliwakamata zaidi ya wageni 30 wakiwa njiani kuelekea au kutoka Somalia, na kuongeza kuwa watu wengi zaidi waliendelea kwenda na kurudi bila ya kugundulika. "Idadi kubwa bado imeshikiliwa na inasaidia katika uchunguzi, wakati wale walioachiwa huru huweko katika ufuatiliaji," aliiambaia Sabahi. Maalim alisema kwamba katika miaka miwili iliyopita, polisi wamewakamata au kuwaweka kizuizini watu wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na al-Shabaab wakiwa na pasipoti za Morocco, Iran, Saudi Arabia na hata Uingereza. "Kitisho tunachokabiliana nacho sio tu kwamba kinatoka nje ya mipaka yetu, bali kutoka ndani ya watu ambao mtu angeliweza kukataa (kuwashuku)," alisema.
Majina makubwa yanajumuisha kukamatwa hapo Disemba 2011 kwa raia wa Uingereza Jermaine Grant, ambaye alishitakiwa kwa kumiliki milipuko na kupanga mashambulizi mjini Mombasa. Kesi yake inaendelea. Raia wa Uingereza Samantha Lewthwaite, mjane wa Germaine Lindsay, mshukiwa wa mashambulizi ya tarehe 7 Julai 2005 jijini London pia anaaminika kujificha nchini Somalia, kwa mujibu wa polisi. Mwezi Septemba, Lewthwaite alituma taarifa mtandaoni kwamba anakusudia kushiriki kwenye mashambulizi ya kujitoa muhanga, akisifu kazi za al-Shabaab.

Hivi karibuni, polisi wa Kenya walimkamata raia wa Uswisi, Magd Najjar, hapo mwezi Mei na kumshitaki kuwa mwanachama wa al-Shabaab na kuingia nchini kinyume na sheria. Najjar alikana mashitaka hayo na anasubiri kesi yake. Adan Mohamed Salah, mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi mjini Baidoa, alisema kwamba al-Shabaab imetumia nyenzo kadhaa kuwavutia wageni. "Pamoja na kudai kwamba Somalia imevamiwa na makafiri, pia imeahidi fedha kwa wale wanaoungana kwenye vita vyao," aliiambia Sabahi. Alisema wageni waliosajiliwa hufanyiwa majaribio kuthibitisha kwamba si majasusi. "Majaribio hayo yanajumuisha kuwaua watu ambao al-Shabaab mara kwa mara wanawahukumu kupitia sheria zao.
Mauaji hayo ni ama kwa kuwapiga risasi au kutumia kisu au kuwapiga mawe," alisema. Ushirikiano wa raia ni muhimu kuwazuia al-Shabaab Wengi wa waliokamatwa ni kutokana na taarifa zilizotolewa na raia watiifu. Wapiganaji wengine wa al-Shabaab walitiwa nguvuni kwenye ardhi kame ya majimbo ya Kaskazini Mashariki na Pwani ambako walitelekezwa na viongozi wao, alisema mkuu huyo wa wilaya ya Garissa.
"Kunakucha taratibu kwa Wakenya kwamba mtu kutoka Jimbo la Nyanza, Kati au Bonde la Ufa sasa anaweza kujihusisha na kundi hilo la itikadi kali," alisema Maalim. "Al-Shabaab ina nyuso nyingi na serikali inauchukulia tahadhari sana ukweli huo."

Chanzo: Mtandao wa Sabahionline.com Mwandishi: Na Bosire Boniface, Garissa Desemba 28, 2012
Axact

Post A Comment: