PAMOJA na Serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutoa elimu ya kutumia njia za
kisasa za uzazi wa mpango kote nchini, baadhi ya wanawake katika wilaya ya Mbeya Vijijini
na Jiji la Mbeya wamekuwa wakitumia majivu kama njia ya kupanga uzazi na kutoa mimba
zisizotarajiwa.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii katika mji wa Mbalizi Mbeya Vijijini na
kata ya Manga na Foresti Jijini Mbeya umebaini kuwa wanaoongoza kwa kutumia njia hiyo ni
pamoja na wake za watu na wahudumu wa Bar.

Wanawake waliohojiwa wakiwemo wawili kati yao ambao wakawa na mahusiano na mwandishi
wa makala haya ili kukamilisha uchunguzi, walisema kuwa majivu hayo wanakunywa kikombe
kimoja kila baada ya kumaliza kufanya tendo la ndoa na wanaume ambao wana mahusiano nao
ya kimapenzi na wengine waume zao. ‘’Majivu unatakiwa unywe ndani ya masaa 12 baada
ya kutoka kufanya tendo la ndoa ili mimba isitunge’’ anasema Mama Angel mkazi wa eneo la
Mama John ambaye ni mke wa mtu.

Mama Angel anakiri kuwa amewahi kutoa mimba kwa njia za kisasa ambayo haikuwa
mimba ya mumewe na alipoambiwa kuwa kuna njia zingine za kujikinga ikiwemo kunywa
majivu baada ya tendo la ndoa ameendelea kutumia njia hiyo kwa miaka mitatu sasa. ‘’Kule
hospitali nilitundikiwa maji ya uchungu ambayo yanaongeza njia na ndani ya masaa matatu
mimba ikatoka’’ anasema Mama Angel bila kutaja hospitali aliyotolea mimba. Uchunguzi
huo uliofanywa mwezi Octoba na Novemba 2012, umebaini kuwa kwa sasa wanawake wengi
hawapendi kutumia njia za uzazi wa mpango wa kisasa mfano Sindano, vipandikizi na vidonge
kwa madai kuwa huduma hizo zina madhara. Wanawake 43 waliohojiwa wakiwemo wake za
watu 13 walisema kuwa madhara waliyoyapata baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango wa
kisasa ni pamoja na kupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Baadhi walisema kuwa wanaogopa kufanyiwa upasuaji (kusafishwa) kunakotokana na uvimbe
unaosadikika kutokea baada ya kutumia kwa muda mrefu huduma hizo za kisasa hasa vidonge
maarufu kama majira. ‘’Tarehe za Hedhi hubadilika na kutoeleweka baada ya kutumia dawa hizo
za uzazi wa mpango wa kisasa zikiwemo sindano na vidonge’’ anasema Naomi Haule ambaye ni
mhudumu wa Bar.

Wengine ambao waliomba hifadhi ya majina yao, wanasema mbali na kutumia majivu kama
njia ya uzazi wa mpango kuzuia mimba na utoaji mimba, baadhi yao wanatumia kisamvu,
Vidonge vya uzazi wa mpango maarufu kama (Majira) na majani ya mti unaojulikana kwa jina
la Songwa kutoa mimba zisizotarajiwa. ‘’Wake za watu wanaopata mimba ambazo si za waume
wao, wafanyabiashara na wahudumu wa Bar siyo siri tunaongoza katika kutumia njia hizi na
utoaji mimba kwa njia za kienyeji’’ anasema Rehema Mwakitalu akiwa na wenzake eneo la
Mwanjelwa ambaye pia ni muhudumu wa Bar.

Walipoulizwa kuwa kwanini wasitumie njia za kisasa katika utoaji mimba walisema kuwa
kikwazo ni gharama za utoaji mimba kwa njia za kisasa ambapo mwanamke mwenye mimba
ya mwezi mmoja hutozwa Shilingi 40,000 ili asaidiwe kutoa mimba hiyo. Walizitaja hospitali
ambazo zinahusika kutoa mimba hizo kwa siri kuwa ni pamoja na hospitali ya wazazi Meta na
zahanati zingine za madaktari binafsi zilizopo eneo la Nzovwe, Mama John na Uyole. Aidha
mbali na hospitali hizo, wanawake hao walisema kuwa pia kuna waganga na wakunga wa jadi
wanaowasaidia kutoa mimba hizo ambazo wanadai kuwa hazikutarajiwa na kwamba wakunga
hao wapo eneo la Mapelele wilaya ya Mbeya na Iwambi Jijini Mbeya. Kuhusu maambukizi ya
ugonjwa wa Ukimwi wanasema; ‘’

Ni bora kupata ukimwi kuliko mimba kwasababu ukipata ukimwi unajulikana baada ya muda
sana na unapata dawa za kurefusha maisha lakini mimba ukipata huwezi kuendelea na starehe
na ukijifungua unalazimika kulea mtoto kwa muda mrefu huku na wanaume wengi hawaeleweki
kwenye matunzo’’ wanasema wanawake hao.

Wanawake wahudumu wa Bar walipoulizwa kuwa kwanini wanatumia zaidi majivu kama njia
ya uzazi wa Mpango na utoaji Mimba walisema kuwa baadhi ya wanaume huwa hawapendi
kutumia mipira (Condom) wakati wa kujamiiana hivyo baada ya tendo la ndoa wanalazimika
kutumia njia hiyo kama moja ya njia rahisi ya kuzuia mimba kutotunga. Walipoulizwa kama
wanajua madhara ya kutumia huduma ya majivu na kisamvu kwa muda mrefu kama huduma ya
uzazi wa mpango na utoaji mimba walisema kuwa hofu yao ni kwamba wanaweza kupata kansa
au kutozaa tena. ‘’Ili kuepukana na kupata madhara ya kansa yanayoweza kutokana na majivu,
huwa mtu akinywa basi siku hiyo anatakiwa kunywa maji kwa wingi ili kupunguza kemikali
zitokanazo na majivu’’ anasema Asha Juma.

Anasema yeye ni Mama wa watoto watatu na tangu amepata mtoto wake wa kwanza mwaka
1998 amekuwa akitumia majivu kila baada ya tendo la ndoa. Na kwamba alipojaribisha
kutumia vidonge alisumbuliwa na nyonga na kukosa hamu ya tendo la ndoa hatimaye akaenda
kusafishwa na alipojaribisha sindano pia alipata madhara ya kukosa hamu ya tendo la ndoa
ambapo mpaka sasa anatumia Majivu kama njia salama kwake ya uzazi wa mpango Baadhi
ya madaktari waliohojiwa kwa sharti la kutoandika majina yao gazetini wamekiri kuhusika na
biashara ya utoaji mimba kwa njia za kisasa na kuzitaja njia wanazotumia. ‘’Wenzetu kuna

sheria za utotaji mimba lakini ajabu hapa Tanzania tunakataza wakati watu wengi wanatoa
mimba tena hasa wake za watu na njia ambazo wengi tunazitumia kwa usalama zaidi ni
kuwatundikia Drip za maji ya uchungu na vidonge vya uchungu vinavyoongeza njia kwa
mwanamke’’wanasema madaktari hao kwa nyakati tofauti.

Siku wanazotumia zaidi ni siku za Jumapili ambapo wanasema kuwa baada ya kumaliza
utoaji huo wa mimba wanawake hao wanatoka wakiwa salama na kuwapatia dawa za kutuliza
maumivu na kuwashawishi kula vyakula na vinywaji vya kuongeza damu. Uchunguzi zaidi
umebaini kuwa, katika sayansi ya akili watu wanaojamiiana huwa wanatumia kinga mara ya
kwanza na ya pili baada ya kuanza mahusiano na huwa hawatumii tena kinga baada ya kukutana
mara ya tatu na nne na kuendelea.

Sanjari na hayo imebainika kuwa wauguzi wengi huwa hawatumii njia za kisasa za uzazi wa
mpango licha ya kuendelea kuwashawishi wananchi wengine kutumia njia hizo kwa madai kuwa
vidonge hivyo huwa wakimeza haviyeyuki. ‘’Sisi wengi hatutumii kwasababu kuna madhara
makubwa ukitumia kwa muda mrefu ambapo ukitaka kuzaa unalazimika kwenda kusafishwa
kizazi na vidonge hivyo haviyeyuki na inatia hofu kuwa ukikwanguliwa unaweza usizae tena’’
walisema baadhi ya wauguzi wa hospitali za Ifisi Mbalizi na hospitali ya wazazi Meta kwa sharti
la kutotaja majina yao.

Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Mbeya Prisca Butuyuyu, anasema kuwa
mila na desturi ni tatizo katika utumiaji sahihi wa uzazi wa mpango na kwamba katika wilaya
ya Mbeya Vijijini mwaka 2011 vilitokea vizazi hai 38 kati ya 100,000 na vifo 113. Kwa upande
wa Jiji la Mbeya mwaka 2011 anasema vizazi vilikuwa 109 kati ya 100,000 na vifo vilikuwa
363 ambapo katika uzazi huo hospitali ya wazazi meta ndiyo inahusika zaidi na inahudumia
wanawake pia wanaotoka nje ya Jiji la Mbeya.

Habari hii ni kwa hisani ya Chama cha waandishi wa habari wa Vijijini.
Axact

Post A Comment: