PAZIA la michuano ya Kombe la Mapinduzi, linafunguliwa leo kwa michezo miwili kwa Simba kuivaa Jamhuri ya Pemba, huku Tusker ya Kenya wakipepetana na Bandari mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri ya mchezo, lakini amesisitiza mashindano hayo yatasaidia kujenga timu imara itakayoiwakilisha Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Nafikiri mashindano haya yamekuja wakati mwafaka.
Pia, tumepata kocha mpya Mfaransa Patrick Liewig.
Ni wakati wetu sasa kushirikiana naye kujenga timu na kufanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa.”
“Nadhani mashindano haya tutayatumia zaidi kupata picha halisi ya kikosi chetu. Pia, kutambua uwezo wa kila mchezaji, kiuchezaji,” alisema Julio.
Hata hivyo, kocha huyo ametamba kuwa Wekundu hao wana nafasi kubwa kutwaa kombe hilo, kulingana na ubora wachezaji wanaounda kikosi cha Simba kwa sasa.
Naye, kocha wa Tusker ya Kenya, Robert Matano amesema baada ya kuzifunga Simba na Yanga katika mechi za kirafiki, anafikiri timu yake ina nafasi kubwa kulitwaa kombe hilo kwenye nchi ya Tanzania.
“Nafikiri kuzifunga Simba na Yanga, timu yangu ni nzuri. Sizifahamu vizuri timu nyingine. Lakini naamini tutafanya vizuri na hata kurejea na kombe nchini Kenya.” alisema Matano.

Bingwa watetezi, Azam FC itashuka dimbani kesho usiku kupepetana na Coastal Union huku ukitanguliwa na mchezo kati ya Mtibwa Sugar ya Morogoro na Miembeni ya Zanzibar.
Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanaifunga Coastal Union kwenye mchezo huo wa ili kulitetea taji lao kwa mara nyingine.
“Hali ya timu kwa jumla ni nzuri. Kila mchezaji ana hari kuhakikisha timu inafanya vizuri na kutetea taji kwa mara nyingine.”
Kocha huyo alisema; “Kila mchezaji ameahidi kucheza kwa kujituma ikiwa ni lengo la timu yake kufanya vizuri na kutetea ubingwa huo.”
“Ni jambo zuri kwangu nikiwa kama mwalimu wa timu kusikia maneno hayo kutoka kwa wachezaji wangu.
Nafikiri ni hatua moja ya mafanikio yetu katika mashindano hayo.” aliongeza.Naye, kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco alisema anafikiri mchezo huo utakuwa mgumu na ushindani hivyo hawezi kusema kuwa timu yake itaibuka mshindi isipokuwa dakika 90 ndizo zitakazoamua.
“Nafikiri tumejianda vya kutosha. Tunachosubiri muda ufike tuweze kuwathibitishia mashabiki tulichokuwa tukikifanya kwa wakati wote.” alisema kocha huyo.
Axact

Post A Comment: