• Atolea majibu Juu ya Wajumbe wa Bunge la Katiba Mme na Mke.
ikulu picha
IKULU YA DAR ES SALAAM.
Baada ya kuwepo malalamiko toka kwa baraza la maaskofu wa kipentekoste Tanzania PCT kama taasisi rasmi kutopata ushiriki kwenye bunge la katiba la Tanzania ambalo limeanza wiki hii,Ofisi ya Rais wa jamhruri ya Muungano wa Tanzania imetoa taarifa rasmi ikiwa ni kujibu hoja iliyoibuliwa na baraza hilo siku chache zilizopita.
 
Ofisi ya Rais, Ikulu, imesema uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, haukuwa na nia ya kulibagua Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania,na kusema kua kuna kila sababu ya kuamini kuwa mapendekezo ya wajumbe kutoka baraza hilo hayakuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kama sheria ilivyohitaji. 
Pia, imesema pamoja na baraza hilo kutowasilisha mapendekezo yao kama ilivyotakiwa, litawakilishwa vyema na wajumbe walioteuliwa ambao wanajumuisha mjumbe aliyeteuliwa kutoka moja ya madhehebu yanayounda baraza hilo. 


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ikulu mjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florence Turuka, alisema tamko la Baraza la Maaskofu kuwa linabaguliwa na serikali halina ukweli wowote. 


Dk. Turuka alitoa ufafanuzi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, na kuongeza kuwa kama mapendekezo ya baraza hilo yengewasilishwa kwa mujibu wa sheria, yasingeachwa. 


Alisema uchunguzi uliofanywa na Ikulu, haujathibitisha kuwa baraza hilo liliwasilisha mapendekezo yake na kwamba ni vyema baraza likajiuliza kwanini kama kulikuwa na mapendekezo hayakufikishwa kwa wakati kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Zanzibar. 


Dk. Turuka, alisema iwapo mapendekezo ya baraza hilo yangefikishwa kwa makatibu wakuu hao, Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Alli Mohammed Sheni, wangechagua mwakilishi kutokana na mapendekezo hayo. 


Alisema uchambuzi wa majina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba umebaini kati ya wajumbe 13 kutoka taasisi za kidini wa Tanzania Bara walioteuliwa, Respa Adam, ameteuliwa kutoka Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Patmos Vission, Kigamboni, ni moja ya madhehebu ambayo maaskofu wake wakuu wanaunda baraza hilo. 


Kwa mujibu wa Dk. Turuka, Februari 11, mwaka huu, baraza hilo lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa limebaguliwa na serikali wanayoiheshimu, kuiombea na kuipenda katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. 


Alisema anawahakikishia Watanzania hususan waliolengwa na taarifa ya baraza hilo kwamba serikali haikupuuzia kundi lolote lililoanishwa kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba.
Dk. Turuka alisema serikali inaliheshimu baraza na inalishukuru katika juhudi inazozifanya kwa kushirikina na serikali katika kuwaendeleza Watanzania.


Alisema makundi 850 yaliwasilisha mapendekezo ya majina 3,636, ambapo makundi ya kidini yalipendekeza majina 429.
Katibu Mkuu huyo, alisema uchambuzi wa mapendekezo 52 yaliyowasilishwa nje ya muda, haukubaini kuwepo kwa mapendekezo kutoka baraza la maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.


Katika hatua nyingine, Dk. Turuka amesema hana uhakika kuwa wajumbe waliochaguliwa kutoka Chama cha NLD ni mtu na mke wake.
Axact

Post A Comment: