Mshambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana
Samata.
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa
kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samata alifunga bao pekee na kuiongoza TP Mazembe
ya DR Congo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mabingwa
watetezi Al Ahly wakiaga mashindano kwa kuchapwa 3-2 nyumbani na Al Ahly
Benghazi ya Libya.
Samata aliingia akitokea benchi na
kufunga bao hilo dakika ya 68 na kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Sewe Sport ya
Ivory Coast na kusonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo ya
jumla kuwa 2-2 baada ya awali Mazembe kutunguliwa mabao 2-1 jijini Abidjan.
Samata ndiye aliyefunga bao la
kufutia machozi Abidjan wiki moja iliyopita pamoja na bao pekee la Jumamosi
jijini Lumbumbashi. Sasa Mazembe itasubiri kujua wapinzani wake katika droo
itakayopangwa Aprili 29 mjini Cairo.
Nao mabingwa watetezi Al Ahly ya
Misri wameaga mashindano hayo baada ya kuchapwa mabao 3-2 nyumbani na Al Ahly
Benghazi katika pambano la marudiano lililopigwa mwishoni mwa wiki jijini
Alexandria.
Kipigo hicho kinaifanya Al Ahly
iondolewe mashindano hayo kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya mechi ya kwanza
iliyopigwa jijini Tunis, Tunisia ambako Benghazi wanatumia kama uwanja wa
nyumbani kutokana na machafuko kushinda 1-0.
Kutoka: Mwananchi.
Post A Comment: