BISMARK ROCK MWANZA.
Ndugu Wananchi napenda kuwataarifu kupitia vyombo vya habari juu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2014 ambayo Mkoa wa Mwanza umechaguliwa kuandaa maadhimisho hayo kitaifa.

 

Ndugu Wananchi, Maadhimisho ya Siku ya mazingira Duniani hufanyika kuanzia tarehe 01 hadi 05 ya mwezi Juni kila Mwaka. Maadhimisho haya huwa na Kauli mbiu iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili kuhimizana juu ya umuhimu wa uhifadhi wa Mazingira yetu.

 

Kwa mwaka huu 2014, shirika la Umoja wa mataifa linalo shughulikia mazingira limetangaza Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kuwa ni “RAISE YOUR VOICE BUT NOT THE SEA LEVEL” kwa tafsiri ni “CHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA  TABIANCHI. Kitaifa, kauli mbiu yetu ni ”TUNZA MAZINGIRA ILI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.

 

Ndugu wananchi

Kama nilivyotanguliwa kusema, Mkoa wa Mwanza umeteuliwa kuwa mwenyeji wa kitaifa, wa maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani mwaka huu. Katika juma hilo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo yote, kuhamasisha wananchi kuhusu utunzaji wa Mazingira  kwa njia ya Makongamano, kupanda miti, kuzoa takataka, maonesho ya utunzaji na mazingira, kuondoa magugu katika Ziwa Victoria na ufugaji wa nyuki pamoja na kufanya ziara kwenye maeneo tofauti yanayo jishughulisha na utunzaji wa mazingira ikiwemo viwanda.

 

Ndugu wananchi,

Ufunguzi wa maadhimisho haya kitaifa utafanyika tarehe 02 Juni, 2014 kuanzia saa 1.00 asubuhi katika Viwanja vya Furahisha, Ufunguzi huo utafanywa na Waziri nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Mheshimiwa Dkt, Binilith Mahenge  na siku ya kilele itakuwa tarehe 05 Juni, 2014 ambapo Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal.

 

Ndugu wananchi,

Shughuli zitakazo fanyika siku ya tarehe 05 Juni 2014 (Siku ya kilele)  ni pamoja na:- kukabidhi vyeti kwa wadau mbali mbali wa mazingira, zawadi na tuzo ya Rais ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na zawadi nyinginezo kwa washindi wa kuhifadhi mazingira.

 

Ndugu waandishi wa habari,

 

Natambua kwamba ninyi ni wadau wakubwa sana wa mazingira hasa katika jukumu lenu la kuuelimisha umma, juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, kwa nafasi ya pekee niwaombe muweze kuipeleka taarifa hii kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani ili waweze kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Furahisha kwa muda wote ambao elimu kuhusu utuzaji wa mazingira itakuwa ikitolewa na wadau mbali mbali.

 

Aidha  Mkoa unategemea kupokea Wageni wa Kitaifa na  Kimataifa, ambao watatembelea  viwanda na kuona utunzaji wa Mazingira na jinsi ya kutenga taka ngumu na zisizo ngumu.

 

Nichukue fursa hii kutoa rai kwa wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi na kushirikiana na wageni wetu kama ilivyo ada ya Wana Mwanza. Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi na kuwalaki wageni wote watakao tufikia katika juma zima kuanzia tarehe 01 hadi 05 Juni 2014. Kama ilivyo desturi yetu wana Mwanza tuonyeshe ukarimu wetu kwa wageni wetu na pindi watakapo ondoka waikumbuke Mwanza.

 

Nimalizie kwa kusema nawashukuru sana kwa kuitika wito wangu.

 

“TUNZA MAZINGIRA, KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI”

 

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA

 

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.

 

IMETOLEWA NA MKUU WA MKOA WA MWANZA.
Axact

Post A Comment: