JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS

TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

 


 
MKOA WA MWANZA

Anwani ya Simu: “REGCOM”                                            OFISI YA MKUU WA MKOA,

Simu Na:028-2500686/2500690                                          S.L.P. 119,

Fax 028- 2501057/2541242                                                            MWANZA
 
                 TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ya Jiji, Manispaa na Wilaya za Mkoa wa Mwanza kuwasilisha Hati za Malipo ya Mishahara (Pay roll) za watumishi wao wote waliopo kazini kwa ajili ya kuanza zoezi la uhakiki watumishi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, wakati alipokutana nao kwa ajili ya kujitambulisha, alisema katika agizo hilo amewataka Wakurugenzi kuwasilisha Pay roll hizo ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa tarehe 05 Aprili, 2016 kabla ya saa 6:00 mchana.

Amesema mara baada ya kuwasilishwa kwa hati hizo za malipo, zitakabidhiwa kwa Kamati maalum ambao ataiunda kwa ajili ya kupita kwenye halmashauri zote kuwahakiki watumishi wote waliopo kazini hata wale ambao wapo masomoni au nje ya vituo vyao vya kazi.

Zoezi hili la uhakiki wa watumishi wote ni muendelezo wa ufuatiliaji wa watumishi hewa katika mkoa wa Mwanza kufuatia zoezi la awali kukamilika na kubainika kuwa na watumishi hewa wapatao 334.

“Katika zoezi hili, tutakuwa tukihakiki wafanyakazi wote waliopo kwa kuonana  ana kwa ana kamati nitakayoiunda na kabla ya kuanza wakurugenzi watapaswa kuwataarifu watumishi walio nje ya kazi kama; likizo, safari, masomoni au nje ya nchi kurejea wakati wa zoezi hilo kwa ajili ya kuhakikiwa wakiwa na nakala tatu za picha za Passport Size.

“Nimesha muagiza Katibu Tawala wa Mkoa, kuwafahamisha haya wakurugenzi wote kuwasilisha Pay roll zote mezani kwake ili kamati nitakayoiunda kwenda kufanya uhakiki, kukutana nao moja kwa moja (physical),” alisema Mongella.

Alisema zoezi hilo litachukua muda wa siku saba kwa kila halmashauri na baada ya hapo ripoti kamili itatolewa. Aidha alisema hatoshangaa kuona idadi ya watumishi hewa ikiongezeka au kupungua kwani katika uhakiki huu watapitia kwa kina watumishi wote

Katika hatua nyingine Mongella, amewataka waandishi wa habari katika mkoa wa Mwanza kutoa ushirikiano wa kutosha pale wanapokuwa na taarifa za kusaidia kufichua uhalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa.

“Mwandishi wa habari hatofautiani na kachero wa Polisi, sasa tusaidiane kuongoza huu mkoa kwakupeana taarifa, maana mkoa huu ni mkubwa, sio rahisi kwa Mkuu wa mkoa kujua yote yanayoendelea hadi ngazi ya kijiji lakini kwa kuwa ninyi wenzangu mnao wigo huo basi tusaidiane ili watu katika mkoa huu waweze kufanya kazi zao kwa amani na salama. Amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza.

Imetolewa;

Atley J. Kuni

AFISA HABARI NA UHUSIANO

OFISI YA MKUU WA MKOA WA MWANZA

 Aprili 04, 2016.

 
Axact

Post A Comment: