![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godyfrey Zambi akipewa Maelezo na Afisa Vipimo namna ya kutambua mawe sahihi ya Mizani yaliyo hakikiwa na Wakala wa Vipimo |
Akizungumza katika
banda hilo, amewataka Wakala wa Vipimo kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia matumizi
sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali, ili wakulima na Wananchi kwa ujumla waweze kunufaika
na mazao wanayolima pindi waendapo kuyauza wakati wa msimu.
Ameongeza
kuwa, maafisa wa vipimo ni muhimu kwa kushirikiana na maafisa waliopo katika ofisi
za wakuu wa mikoa katika kuhakikisha wakulima hawapunjwi pindi waendapo kuuza
mazao yao kwakuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, huchezea mizani yao kwa lengo
la kuwapunja wakulima kwa lengo la kupata faida zaidi.
Awali wakitoa
maelezo kuhusu kangomba maafisa wa wakala wa vipimo walimuelezea mkuuhuyo wa
mkoa namna kangomba inavyowapunja wakulima, kwa kuwa siyo kipimo sahihi
kinachopaswa kutumika kununulia mazao.
Kufuatia maelezo
kutoka kwa wakala wa vipimo ndipo ikamalazimu mkuu huyo wa kutoa tamko kali
dhidi ya wale wote wenye kutumia kangomba katika kuuza au kununua mazao ya
wakulima.
“Lazima
tuelewe falasafa ya Rais wetu, anataka mapinduzi ya viwanda lakini mwenye
kuzalisha malighafi ni mkulima hivyo lazima, katika mazao yake aone faida,
vinginevyo atauchukia ukulima na kukatishwa tamaa”, alinukuliwa mkuu wa mkoa.
Wakala
nchini imekuwa na jukumu la kuwapa wakulima elimu ya matumizi sahihi ya mizani
iliyo hakikiwa na kutambua alama zinazowekwa kwenye vipimo vilivyohakikiwa na
Wakala ambazo ni stika maalum, pamoja na kugongwa nembo ya
Taifa na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika. Mfano kwa mwaka huu 2017, itasomeka
namba 17.
Kwa upande
wake Afisa Vipimo wa mkoa wa Lindi bw.
Nyagabona Mkanjabi alisema, wamejipanga vizuri katika kusimamia matumizi ya
vipimo sahihi na kuhakikisha mizani zote zinazotumika katika vyama vya ushirika
vya msingi zinakaguliwa kabla ya misimu ya kuuza mazao kuanza huku aki wahakikishia kaguzi mbalimbali za
kustukiza zinafanyika kipindi cha msimu wa kuuza mazao unapofika.
Pia,
amewakaribisha viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi pamoja na wananchi
wote kutembelea banda la wakala wa vipimo katika maonesho ya nanenane mkoa wa
Lindi na kujionea Mizani mbalimbali zinazopaswa kutumika katika ununuzi wa
bidhaa mbali mbali na mazao ukiwemo mzani wa digital wa tani 2 ambao unapima
bidhaa/mazao na kutoa risiti hapo hapo
Akizungumza pembeni
mwa mkutano huo, kaimu Afisa Vipimo mkoani hapo, Andrew Mbwambo ametoa wito kwa
Wakulima, wafanyabiashara na Wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya
kuchezea vipimo kwani kwa sasa adhabu ni kubwa baada ya Sheria ya Vipimo Sura
namba 340 na Mapitio yake ya mwaka 2002 kufanyiwa marekebisho mwaka 2016.
Kila mwaka
wakala wa vipimo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inashiriki maonesho
mbalimabali ikiwapo ya Nanenane huku wakiwa na jukumu la kutoa elimu ya mara
kwa mara kwa wakulima na wanunuzi wa mazao na umuhimu wa kutumia vipimo sahihi.
Maonesho ya
Nane nane kitaifa yamefanyika mkoani Lindi kwa mara ya tatu mfululizo
huku yakiongozwa na kaulimbiu “Zalisha kwa tija mazao na biadhaa za Kilimo,
Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa kati”.
Post A Comment: