Hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ENG.
EVARIST NDIKILO katika warsha ya maendeleo ya malengo ya milenia baada ya mwaka 2015 iliyofanyika Gold Crest Hotel Tar: 04/12/2012.



• Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka ESRF Dr. Kaino
• Mwezeshaji kutoka ESRF
• Wawakirishi wa Serikali za Mitaa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji
• Washiriki wa Warsha
• Wawakiriki wa Asasi za kiraia pamoja na walengwawao
• Waandisha wa Habari
• Mabibi na Mabwana
• Tumsifu Yesu Kritu, Bwana Yesu Asifiwe, Asalaam Alekum.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa uwezo wake
wa kunipa afya njema na kuweza kuwa nanyi siku ya leo katika
ufunguzi wa Warsha kuhusu maendeleo ya Malengo ya Milenia
baada ya 2015 iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya
Uchumi na Jamii (ESRF).

Vile vile napenda kuchukua fursa hii kuishukuru taasisi ya
ESRF kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza kuwa mwenyeji wa
kuendesha Warsha hii, maana nimeelezwa kuwa taasisi ya ESRF
inaendesha Warsha kama hii katika Kanda saba (7). Kanda
ya Ziwa inayoundwa na mikoa minne ya Kagera, Mara, Geita
na Mwanza, Mwanza ndiyo iliyochaguliwa kuwa mwenyeji wa
Warsha hii. Hivyo ninawakaribisha sana katika Jiji la Mwanza
na ninawahakikishia usalama wa kutosha kwa muda wote
mtakaokuwa hapa.

Kama nilivyoelezwa pia kuwa, Taasisi hii imepewa jukumu na
Serikali ya Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya
Rais - Tume ya Mipango kusimamia majadiliano ya Wadau kitaifa
kuhusu michakato ya Maendeleo baada ya kufikia kipindi cha
malengo ya Milenia, 2015.

Ndugu Washiriki: Malengo ya Milenia ni matokeo ya Mkutano
wa kilele cha Milenia wa umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi
Septemba, 2000 uliowakutanisha Wakuu wa nchi 147 waliokuwa
wakiwakilisha Mataifa wanachama 189 wa umoja wa mataifa.
Lengo kuu lilikuwa kufafanua mkakati wa pamoja wa vipaumbele
juu ya jinsi ya kukidhi mahitaji ya umasikini duniani.

Itakumbukwa kuwa Tanzania ni moja ya mataifa 189 ambayo
mnamo mwezi Septemba, 2000 ilishiriki kutekeleza na kuahidi
kuyafikia malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015.

Ndugu washiriki: mpango wa malengo ya milenia unatoa
wito kwa nchi zinazoendela na zilizoendelea kufanya kazi kwa
kushirikiana ili kufikia malengo ya kupunguza umasikini, njaa,
magonjwa, vifo vya mama wajawazito na watoto wenye umri
chini ya miaka mitano, kuhakikisha watoto wote wanapata elimu
ya msingi, kuhakikisha fursa sawa kwa wote, na kudumisha usafi
na ubora wa mazingira.

Ndugu washiriki: Tanzania imepiga hatua nzuri katika
kutekeleza makubaliano hayo ya mikakati ya ukuaji wa uchumi
na kupunguza umasikini. Hii ni kutokana na mipango ya milenia
kuwa katika mikakati ya kitaifa ya dira ya maendeleo 2025,
MKUKUTA kwa Tanzania Bara, na 2020 MKUZA kwa Tanzania
Zanzibar. Dira zote zinalenga kuibadili Tanzania kutoka katika
nafasi iliyopo ya nchi zinazoendelea na kuiweka katika nchi zenye
kipato cha kati.

Ndugu washiriki: Tanzainia imeweza kutekeleza sera na
mipango yake ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Mafanikio
makubwa yaliyofikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ada ya
shule za msingi ambapo imesaidia kuongezeka kwa watoto
wanaoandikishwa kujiunga na shule za msingi. Aidha, vifo vya
watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua, upatikanaji
wa huduma bora kama vile maji salama na vituo vya afya
umeongezeka na kuboreka.

Mbali na mafanikio hayo kuna changamoto nyingi katika
kutokomeza umasikini, njaa, kuboresha afya ya uzazi na huduma
za maji salama. Iwapo changamoto hizi zitapatiwa suluhisho,
basi kiwango cha umasikini nchini kitapungua kwa kiwango
kikubwa.

Ndugu washiriki: Kwa Kuwa utekelezaji wa malengo ya milenia
unaisha mwaka 2015, taasisi ya utafiti katika nyanja za uchumi
na jamii (Economic and Social research Foundation – ESRF)
imepewa jukumu na Ofisi ya Rais, Tume ya mipango kukusanya
maoni ya wadau mbalimbali kupitia warsha kutoka katika mikoa
yote ya Tanzania. Warsha hii imekutanisha Wadau na maafisa
wa Serikali za mitaa na asasi za kiraia na hivyo basi, ushauri na
mapendekezo yenu ya nini kifanyike kwa siku zijazo baada ya
2015 ni muhimu sana.

Ndugu washiriki: Kwa maneno haya machache nachukua fursa
hii kuwakaribisha rasmi katika mjadala huu na kuwaomba mshiriki
kikamilifu ili tuweze kupata kile tunachokihitaji katika kuleta
maendeleo nchini mwetu. Napenda kusema kuwa warsha hii
imefunguliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza
Axact

Post A Comment: