Faith Kabura Makena alivunja kikwazo cha kijinsia kwa madereva wa kike wa bodaboda mjini Garissa. [Bosire Boniface/Sabahi]
 Picha ya teksi ya pikipiki ya Faith Kabura Makena kwenye barabara za Garissa nchini Kenya inatoa taswira ya nadra sana.

Makena, mwenye umri wa miaka 30, alisema anajua kwamba kuchagua kwake biashara hii kumesababisha utata na mara kadhaa huwashangaza wakaazi wa huko anapowapita.

Teksi za pikipiki, zinazojulikana kama bodaboda nchini Kenya, ni njia maarufu ya usafiri kwa wasafiri wanaotaka kukwepa foleni kubwa za magari mijini. Wakati inatoa fursa ya kupata maisha mazuri kwa waendeshaji wake, hii ni biashara ambayo imekuwa ikitawaliwa na wanaume tu.
Hata hivyo, Makena alisema aliamua kuipa changamoto imani iliyopo na kuwa dereva wa bodaboda kwa sababu ni chanzo kizuri cha mapato ya kumuhudumia mtoto wake wa kiume wa miaka 6 na wazazi wake, ambao ana jukumu la kuwatunza kifedha.

Grace Ruwa Asar, mwanamke wa kwanza kuwa dereva wa bodaboda Kenya, akimbeba abiria kwenye eneo la Tana River Delta.
"Mwanzoni nilikuwa ninakerwa na namna watu walivyonichukulia lakini kutokana na uungaji mkono wa familia yangu na marafiki, nilisonga mbele," aliiambia Sabahi. "Wiki za mwanzo zilikuwa ngumu kwa sababu sikuweza kupata wateja. Mteja mmoja hata aliwahi kuniambia kwamba nilikuwa ninatania na asingeliweza kuamini usalama wake barabarani kwenye mikono ya dereva mwanamke."
Makena alisema kwamba binamu yake alimfundisha kuendesha pikipiki kwa nia ya kujifurahisha tu. "Kutokana na uchache wa ajira, ilinipitikia kwamba kile nilichojifunza kwa kujifurahisha kinaweza kuwa fursa za kuzalisha kipato," alisema.
Makena, ambaye mwanzoni alikuwa akimiliki duka, amekuwa dereva tangu mwezi Januari, akiwa kwa wastani anapata shilingi 20,000 (dola 233) kwa mwezi. Kwa sasa anafanya kazi na dereva mwingine lakini anatarajia kuweka akiba hadi shilingi 80,000 (dola 931) kufikia mwezi Februari ili aweze kununua pikipiki yake mwenyewe na kuwa dereva anayejitegemea.
Lengo lake kuu, hata hivyo, ni kuwa mwalimu wa sekondari ya juu. Makena alisema amekuwa akiweka fedha kila mwezi kulipia shule, ambako ataanza mwezi Juni ujao.
Mwenyekiti wa Chama cha Boda Boda wa Garissa Joseph Musili aliiambia Sabahi kwamba waendeshaji wengine wengi walikuwa na mtazamo mbaya wakati Makena alipoanza kuingia kwenye biashara hiyo.
"[Kusitasita huko] kulikuja kwa sababu yeye ni mwanamke," aliiambia Sabahi. Lakini jumuiya hiyo iliwaelimisha wanachama hao kwamba ikiwa wanaume wanaweza kuwachukua wanawake kwenye bodaboda, basi wanawake pia wanaweza kuendesha. "Hilo [hatimaye] liliingia kwenye akili zao na kila mtu anafahamu na anamkubali mmoja wetu."
Ben Njogu, mwenye umri wa miaka 31, mkaazi wa Garissa, aliiambia Sabahi kwamba mwanzoni aliamua kubebwa na bodaboda ya Makena kwa udadisi tu. "Udadisi ukawa tabia, na sasa mara kwa mara humtafuta kunipeleka safari zangu, labda awe hayupo [kazini]," alisema.
Ifrah Ali Masha, mkaazi wa Garissa mwenye umri wa miaka 24, aliiambia Sabahi kwamba alishituka alipomuona mwanamke akiendesha bodaboda.
"Kwa mwanamke kuanzisha hatua hama hiyo ya kibiashara ni dalili kwamba kile wanaume wanachoweza kukifanya, wanawake wanaweza pia kama wakipewa nafasi," alisema. Pamoja na hayo, Makena anatoa huduma kwa wanawake ambao wanaogopa madereva wa kiume aidha kwa sababu za kiusalama au kimila, alisema Masha.
Makena anaripotiwa kuwa mwanamke wa pili kuingia kwenye biashara ya boda boda nchini Kenya, baada ya Grace Ruwa Asar wa Tana River Delta.
Asar, aliyeanza kuendesha boda boda mwaka 2010, aliiambia Sabahi kwamba alilazimika kupambana na hofu zake dhidi ya mitazamo ya watu ili kujiwezesha kiuchumi.
"Ni biashara nzuri sana ambayo naweza kupata zaidi ya shilingi 50,000 (dola 582) kwa mwezi baada ya kutoa gharama kama za mafuta na matengenezo," aliiambia Sabahi.
Jamii ya Kenya yenye kuelemea ubabani ina fursa chache za kibiashara kwa wanawake, alisema Asar. "Wanawake wanapaswa kuchukua jitihada zao wenyewe na kujiamini," alisema.
Kutokana na kipato chake cha boda boda, Asar anaweza kujihudumia mwenyewe na kaka zake wawili ambao bado wanasoma.
Ufunguo wa kuingia kwenye biashara hii, anasema, ni kuwa na maadili sana, hasa kuwapuuzia wateja wa kiume ambao wanamfananisha mwanamke aliyeingia kwenye biashara iliyotawaliwa na wanaume na mwanamke asiye na maadili.
"Wanaume wengine hudhani kwamba huna heshima unapowabeba," alisema. "Nililazimika kumpiga kibao mmoja wa wateja wangu wa kiume ambaye alinitomasatomasa." Hata hivyo, alisema kuwachukulia wateja wake kidiplomasia kulimsaidia kuwa na mahusiano mema na wateja.

CHANZO:
Makala hii iliandikwa kwa mara ya kwanza katika mtandao wa SABAHIONLINE.COM

Na Bosire Boniface, Garissa

Desemba 27, 2012
Axact

Post A Comment: